Adeladius Makwega-MBAGALA
Mwanakwetu nimekuwa nikimtafakari sana Jenerali Jacob John Mkunda kisha ninakuwa na masikitiko makubwa juu ya udhaifu mkubwa wa Jenerali huyu wa kulinda Uhai wa Binadamu, tangu awe Mkuu wa Majeshi, huku jamii ya Watanzania ikishuhudia kutekwa, kuteshwa , ulawiti , ubakaji na kuuwawa kwa watu mithili ya Tanzania haina Jeshi la lake la Ulinzi.
Ndugu yangu Jenerali Jacob John Mkunda naomba nikusimulie kisa hiki cha Nyerere na Karume watawala wa hili Taifa.
“Siku moja Mwalimu Nyerere alialikwa JWTZ huko Zanzibar kufunga mafunzo , Mwalimu Nyerere akaamua kumtuma Makamu wa Rais Sheikh Abeid Amani Karume kwenda huku, Mzee Karume ambaye alikuwa mbabe sana alipofika huko akawaambia JWTZ maneno haya:
‘Hili siyo Jeshi la Sultan, hili siyo jeshi la vibaraka, jukumu lenu nyinyi kuhakikisha punde vinapoibuka vitendo vya kishenzi mnashugulika navyo mara moja maana wadogo zenu wanawaangalia, kama matendo mabaya wakifanyiwa kisha nyinyi mkafumbata mikono sasa hili JWTZ litakuwa ni jeshi la nani?’
Mnatakiwa kuonesheni ukakamavu wenu kwa kuzuia vitendo vya udhalilishaji unaofanywa na mtu mmoja mmoja, kikundi au vikundi vya madhalimu.’
Hapa JWTZ wenyewe wakawa wanapiga makofu kwaaa kwaa kwaa kwaaa kuonesha uimara wa maneno haya, Mzee Karume akamalizia kwa kusema haya:
‘Hilo ndilo jukumu la JWTZ yakifanyika hayo na nyinyi mkifumbata mikono hilo litakuwa jeshi la nani…..! ‘
Haya ni Sheikh Abeid Amani Karume na JWTZ enzi ya uhai wake.”
Msomaji wangu unapotazama mwaka aliyozaliwa Jenerali Jacob Mkunda ni 1968, kipindi hiki Mkuu wa Majeshi alikuwa ni Mirisho Sarakikya ambaye aliliongoza JWTZ tangu mwaka 1964 -1974.
“Usalama wa Jacob John Mkunda akiwa kichanga tangu sekunde hadi miaka sita Jenerali Sarakikya alifaya kazi nzuri , kama Jenerali Sarakikya angeacha watu wa Kilosa wauwawe hovyo Jenerali Mkunda angeweza kukalia hiki kiti? Je leo angetajwa ?
Huu mzigo huu wa lawama angebebeshwa mwingine.
Kwa kazi nzuri iliyofanywa na akina Jenerali Sarakikya leo hii lawama ni zako Jenerali Mkunda. Kwa hoja moja tu unalipwa mshahara na umma wa Watanzania. Kwanini Jenerali Mkunda unashindwa kulipa fadhili kwa Watanzania waliokulinda wewe ukiwa kichanga?
Maana wapo hata ndugu wa Jenerali Sarakikya huku Arusha wamefariki kwa haya haya ya Oktoba 29,2025 na siku zilizofuata, Jenerali Mkunda umeshindwa kutulinda Watanzania.”
Jenerali Mkunda unawajibu wa kujiuliza nani anayekulipa mshahara? Kama siyo wananchi hawa hawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Je hauoni kuwa wewe binafsi umewadhulumu nafsi za Watanzania waliofariki Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata kwa kushindwa kutumiza wajibu?
“Mpaka sasa kuendelea kukalia kiti hiki hauoni kuwa ni kuendelea kujiingiza katika moto wa milele? Haoni kuwa ni kuendelea kuchafua jina la vizazi vyako na jamaa zako?
Binafsi nakushauri Hekima Jiuzulu, urudi nyumbani na hili litaonesha kuwa umeumizwa na vifo vya Watanzania huku ukitambua kuwa UKOO WA MKUNDA bado utaendelea kuishi katika ardhi ya taifa hili.
Jenerali Mkunda unapaswa kufahamu kuwa Ukoo wa MKUNDA ulikuwepo na utaendelea kuwepo, unaliachajiejina la ukoo wako?”
Jenerali Mkunda lazima ujiulize hata kama ni mkakamavu kiasi gani, hata kama utapiga saluti namna gani, ndani ya vyombo vya Ulinzi na Usalama wapo ambao wamepoteza ndugu zao katika kadhia ya Oktoba 29, 2025 jiulize swali upo mbele ya gwaride wanakuangaliaje? Wanakutazamaje?
Wapo ambao ndugu wametekwa na wanakungaliaje? Wapo ambao ndugu zao hawajui walipo wanakutazamaje? Wapo vijana wenyewe kutoka vyombo vya Ulinzi na Usalama walioshiriki zoezi hili je wao walikuwa vyuma ambavyo vilikuwa havidhuliki? Wote wapo salama? Hakuna waliofariki?Hakuna waliumia , kumbuka hawa ni ndugu zetu sisi ndiyo walipa mshahara Wanawafahamu haya ndani ya vyombo vya Ulinzi na Usalama wanakutazamaje?
“Jenerali ‘pavu au ‘liti.”
Ngoja twende mbali zaidi:
“Kwa haya yaliyotokea Oktoba 29, 2025 unadhani familia ya MKUNDA itaaminiwa na taifa hili kwa nafasi kubwa kama yako kwa leo hapo baadaye? Kwa namna Watanzania walivyo Jenerali Mkunda umeibebesha mzigo mkubwa familia yako.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kuna umuhimu wa Jenerali Mkunda na Wakuu wote wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wote iwe Polisi, Usalama, Uhamiaji, Zimamoto , Magereza na wote watupishe mara moja.
Hoja ni hiii:
“Wapo Watanzania wengi wamefungwa magerezani, wamefungwa maisha, wapo Watanzania walionyongwa, wapo Watanzania Mahabusu na wapo Watanzania wengi wanafanya safari za kwenda nakurudi kutoka mahabusi, na mahakamani kwa kosa na mauwaji ya mtu mmoja tu. Hapa hapa yule anayemlinda iwe mfungwa iwe mahabusi ametoka kufanya kosa lile lile ambalo linamfanywa mwanzake awe mahabus, anyongwe afungwe maisha lakini haguswi, hii ni Tanzania ya namna gani?Hili ni taifa la namna gani?Hili ni taifa la namna gani?
Aliyetekeleza, aliyeagiza, aliyefanya kikao, Aliyependeza wote ni watuhumiwa wa mauwaji na lazima wawajibike mara moja.”
Mwanakwetu kwa muda mrefu nimelitafakari hili jambo hadi nikajiuliza kama hali ni hii. kuna haja gani kuwa na wafungwa wa makosa mauwaji? Wafungwe wote wa mauwaji kama hali ni hii basi waachiwe huru.
Hivi ndugu zangu Majaji, Mahakimu,Mawakili, Waendesha Mashtaka, Wanasheria, Makarani wa Mahakama mnaoendesha keshi za mauwaji, kuna haja gani ya nyinyi kuendelea kuifanya kazi hii kwa sasa wakati watu wameuwa bado wanazunguka mitaani?
Mwanakwetu ningekuwa Jaji ningemwambia Jaji Mkuu maneno haya:
“Kwa sasa hakuna umuhimu wa sisi kuendelea kutoa hukumu za kesi za mauwaji maana wauwaji wengi wapo mitaani kama Jaji Mkuu ukitaka niendelee na kazi hii timizi hili kwa kuiambia mamlaka husika iwalete wauwaji wote tangu Mkubwa hadi Mdogo wa Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata mbele ya mahakama yako tukufu.”
Mwanakwetu Upo?
Je Makala haya yaitwaje ?
Kama Ningekuwa Jaji, Mahakama Isiendelee na Kesi za Mauwaji au Jenerali ‘Pavu ‘Liti.Mwanakwetu anachagua Kama Ningekuwa Jaji.
Nakutakia siku Njema.
0717649257
















Post a Comment