UTEKAJI NI UDONGO WA SIASA CHAFU

 

 

 Profesa Issa Shivji Dar es Salaam Tanzania

Mateso haya yanoyotendwa kwa mabavu na vyombo vya dola ni udhalilishaji wa hali ya juu wa utu wa binadamu. Hayasahauliki, hayasameheki wala hayakubaliki.

Ni udhalilishwaji wa utu mara mbili. Moja ya yule aliyeteswa - utu wake unakanyagwa, unasagwasagwa na kutupiliwa mbali. Pili ni utu wa mtesaji mwenyewe.

Anajisusha utu wake - anajifanya sio binadamu. Anajigeuza jitu, sio mtu tena. Nafsi yake haiwezi ikawa na amani. Hawezi akawa na raha. Nafsi yake itamsuta hata kama yeye mwenyewe hayajui. Mbele ya binadamu wenzake atajihisi, hata kama hakiri, yeye sio yeyote wala lolote.

Anatembea akiwa ameinamisha kichwa chake kwa aibu. Utu ni msingi na kiini cha haki zote za binadamu na awali ya yote ni uti wa mgongo wa dhana ya usawa wa binadamu.

Kiongozi yeyote anayevumulia mateso ya raia wake sio muumini wa usawa wa binadamu, hata kama akihubiri na kuimba amani kiasi gani.

Mnamo mwaka wa 1976 lilitokea jambo nchini mwetu liliotuachia doa nene katika historia yetu. Kulikuwa na mauwaji, yaliyosambaa kwa kasi kubwa, ya biwazee maeneo ya Shinyanga na Mwanza kwa imani ya ushirikina kuwa walikuwa wachawi.

Viongozi wa ngazi za juu wa usalama na siasa walikaa pamoja na kuamua kwamba jambo hilo lazima likomeshwe.

Vyombo vya usalama vikapanga mkakati ulioitwa operesheni mauaji ambao uligeuka kuwa “mradi” wa mateso na mauaji na udhalilishwaji wa hali ya juu ambayo nchi ilikuwa haijawahi kuona.

Mwalimu hakujua kichokuwa kinaendelea mpaka mabibi walioteswa wakafunga safari kwenda kumuona kwake Butiama alikofikia kwa mapumziko ya Krismasi. Mbele ya Mwalimu wakavua nguzo zao kumuonyesha majeraha waliyoyapata sehemu zao za siri. 


 

Mwalimu alishindwa kuyaangalia - akafunga macho yake kwa mikono yake yote miwili.

Aliwaita mara moja mawaziri wahusika. Waziri wa Mambo ya Ndani wakati ule, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Waziri wa Usalama Bwana Peter Siyowelwa. Mwalimu akawashinikiza kujiuzulu. Wakuu wa vyombo vya usalama wakafukuzwa kazi na kushtakiwa mahakamani.

Ni kweli kwamba tumekuwa na matukio ya mateso katika awamu zote lakini popote pale yalipogundulika hatua ya aina moja au nyingine ilichukuliwa.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio kama haya lakini bahati mbaya hayajakaripiwa wala kulaaniwa hadharani.

Mara nyingine tumesikia wakuu wachache wakitoa matamshi ambayo yanaweza yakashawishi maafisa chini yao kutenda mambo kama haya dhidi ya watuhumiwa au wapinzani. Hii sio sawa hata kidogo. Katika jamii na Taifa kama letu ambalo waasisi wetu walijenga misingi ya usawa na utu, hatuna budi sisi sote, pamoja na viongozi wa siasa, wakuu wa vyombo vya usalama na hata viongozi wa dini kulaani na kutokuvumilia matukio ya utesaji wa raia yeyote. Matukio ya utesaji sio ya kawaida, yasizoeleke, yasipuuzwe wala yasihalalishwe.

 

Katiba zetu zote mbili ya Muungano na ile ya Zanzibar zina vifungu vinavyo piga marufuku tendo la utesaji ama kwa tafsiri au moja kwa moja. Juu ya hili Katiba ya Zanzibar imeweka wazi bila yakumung’unya maneno.Ibara ya 13(3) inasema:

“Ni marufuku kwa mtu kuteswa,  kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu za kudhalilishwa au zinazomtweza utu wake. “

Ibara Hii iliwekwa katika marekebisho ya 2002 (Sheria Nam 2/2002)  ya Katiba ya Zanzibar kutokana na mapendekezo ya jopo la wataalamu kutoka jumuiya ya madola na Watanzania wengine nikiwemo mimi mwandishi wa makala haya.

Ni mazoea ya muda mrefu wa kimahakama, kukataa katakata kupokea ushahidi wowote uliopatikana kwa kutumia mabavu na mateso. Ni matumaini yangu kwamba desturi hii nzuri itaendelea kwenye mahakama zetu na Majaji wetu watakuwa na ujasiri wa kutosha kutupilia mbali ushahidi wowote uliopatikana kwa njia ya kutumia mabavu na mateso.

Vilevile polisi na ofisi ya Mkurungezi wa Mashtaka (DPP) wanatakiwa kuwa makini. Wakinusa tu dalili za utumiaji wa mateso wafanye uchunguzi mara moja badala ya kusubiri taarifa kutoka kwa mlalamikaji.

Utekaji pia ni utesaji. Ukizoeleka tutakuwa tumezama katika udongo wa siasa chafu ambayo haina ukomo.

 







 

0/Post a Comment/Comments