Novemba 21, 2025 Mwanakwetu alifuatwa katika dawati lake, ofisini anapohudumu na Afisa Biashara Mkoa wa Mara Timoth Gambalesi na kumpiga kijembe;
“Mwanakwetu maisha yako siyaelewi kabisa, mara zote upo mwenyewe mwenyewe, ukiangia ofisini unakaa katika ofisi ulipo, unatua begi lako unakaa katika kompyuta yako, ukipewa jukumu unafanya, ukimaliza unarudi katika kompyuta hadi jua linazama, kisha kurudi nyumba kwako.
Kaka leo nakuomba tuambatane na mimi twende Ziwani Victoria ukaone wavuvi wangu wanavyouza samaki kutoka katika vizimba vyao.”
Mwanakwetu akajibu sawa mkubwa natamani kuja huko ziwani lakini leo katika Kitengo cha Mawasiliano Serikalini hapo ofisini nipo mwenyewe inawezekana Mkuu wa Mkoa wa Mara mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi anaweza kuwa na wageni kisha akaagiza watu wa Mawasiliano Serikalini tuwepo, sasa nikiwa mbali hilo litakuwa shida na mara zote huwa sipendi kumkwaza kabisa huyu kiongozi.
Timoth Gambalesi ambaye ni Mkuu wa hii idara akasema hapana kiongozi nakuomba leo twende na wewe ziwani, simu za mawasiliano zipo kama utahitajika utarudi na kwanza ziwani siyo mbali.
Kwa hakika hali ilikuwa hivyo.
Siku hii Mwanakwetu alipata bahati siyo ya kulifahamu Ziwa Victoria hapa Musoma Mjini na pia alipata fursa hata ya kulifahamu vizuri eneo jirani na Ziwa Victoria hapa hapa Musoma Mjini na hii ndiyo siku Mwanakwetu amekula samaki sana kuliko siku yoyote katika maisha yake.
Kwa faida ya msomaji wa Mwanakwetu nakuomba nikuchukue hapo ulipo hadi mwaloni wa Ziwa Victoria hapa Musoma Mjini ambapo hali ilikuwa hivi;
“Mandari hii ilionesha jamaa kadhaa wasiozidi 10 wakiwatoa samaki katika mtumbwi kisha kuwaweka katika kibanda kidogo. Kuwahesabu huku wakiwapima katika mzani mmoja.
Kwa mbali ziwani vilionekana vizimba vya samaki kadhaa huku mjadala hapa mwaloni ulikuwa juu ya samaki tu. Wateja mmoja mmoja walifika na kununua samaki hao na kuweka katika bodaboda au ndoo kisha kwenda zao.”
Mwanakwetu akiwa hapa hapa kuna jamaa mmoja aliyetambulishwa kuwa mnunuzi wa samaki alisema kuwa yeye anafanya biashara hiyo ya samaki kwa miaka zaidi ya mitano tangu 2020 huku biashara hii imemsaidia kupata kipato mara tatu kuliko alipokuwa akifanya kazi zingine ikiwamo ualimu na hata ukarani huko benki, huku akiwa na shahada ya kwanza na Elimu.
“Naomba samaki wangu usimchane mshazali mchane sambamba maana wateja wanapotaka kumnunua samaki au kumla wanataka awe kwa namna nnuri anavyooneka kama mahitaji yake mteja.”
Mwanakwetu hapa hapa akajifunza namna bora ya kumchana samaki kuwa ukimchana sambamba unatumia muda mchache hata kuutoa uchafu wa ndani yake lakini ukimchana mshazali samaki huyu huyu, jamaa anayemtoa uchafu samaki huyu na hata na kumpaa anatuamia muda mwingi maana uwazi unakuwa mdogo. Hapa inategemea wateja wa mnunuzi wanataka samaki wao wamchane vipi?
Je wewe msomaji wangu samaki wako ukimnunua iwe ziwani au baharini unataka uchaniwe vipi? Je sambamba au mshazali?
Jamaa huyu alinunua samaki wake kilogramu 300 samaki aina ya Sato akilipa shilingi 2,550,000/- kwa kilogramu moja, kwa bei ya shilingi 8500/-@ Kilogramu.
Akiwa hapa Mwanakwetu alinunua Kilogramu mbili za samaki Sato ambapo aliuziwa kwa rejareja kwa kilo moja shilingi 10,000/- na alipewa samaki wawili aina ya Sato yaani samaki mmoja alikuwa gramu 1000.
Mwanakwetu alifanya utafiti je bei ya samaki Sato mwaloni wa Ziwa Victoria hapa Musoma kwa reja reja ni shilingi 10,000 lakini kwa jumla ni shilingi 8500. Je bei hii ya samaki haiwezi kushuka? Majibu ya swali hili yalikuwa haya;
“Unajua kwa sisi wafugaji tunaotumia vizimba ziwani tuna changamoto kubwa na wazabuni wanatoa vifaa na bidhaa za uvuvi kama vizimba, nyavu na vyakula vya samaki .
Ebu fikiria mathalani katika kizimba kimoja hadi kukamilika na kukiweka ziwani kiziba kidogo na karibu milioni tisa za Kitanzania lakini hii ni kupitia mzabuni lakini baba kwa gharama za haki inaweza kuwa milioni 4.5 hadi 6 tu na hali hii ndiyo inayopandisha bei ya samaki kwa mlaji.Kwa bidhaa hizi za wazabuni zingekuwa nafuu Kilogramu moja ya samaki ingeuzwa hata shilingi 3500/-”
Kwa upande wake Afisa Biashara Mkoa wa Mara Timoth Gambalesi alisema kuwa wafanyabiashara wanazo changamoto kadhaa zinapatia majibu.
“Hawa ni wadau wa samaki hapa mkoa wa Mara, hawa ni wafanyabiashraa wa ngazi ya kati. Ninapenda kuwatia moyo. Jambo la msingi kuna umuhimu wa biashara kurasimishwa na zitambulike. Huku tuongeze matumizi ya Ziwa Victoria maana sasa tunalitumia kwa kiwango kidogo mno.”
Mwanakwetu alipomaliza haya alibeba samaki wake na kutoka nao hadi kwa mtu wa kuwatengeneza ili akawakaange.
Alifika katika mkahawa mmoja na kuomb samaki hawa watengenezwe vizuri na kuambiwa kuwa Kilogramu mbili hizo za samaki ili kuweza kutengenezwa vizuri alipe shlingi 5000/-Mwanakwetu alianza kulia kulia maana gharama ya kutengeneza samaki hao ilikuwa sawa na kununua tena nusu kilo ya samaki.
“Unajua mzee gharama ya kuwakaanga samaki hawa wawili tunatumia nusu lita ya mafuta ambapo ni shilingi 3000/ kisha 2000 ya mtu anayeifanya kazi hii.”
Mwanakweu akalipa shilingi 5000/ na kisha kutengenezewa samaki wake vizuri .Kijana aliyemkabidhi samaki aliulizwa swali juu ya hekima ipi ipo katika ulaji wa samaki?
Kijana akajibu kwa maneno haya,
“Samaki kwa mkoa wa Mara n ahata eneo lote la Ziwa Victoria, KICHWA Kinaliwa na wanaume huku mkia na kipande cha katikati ndicho kinacholiwa na wanawake na watoto. Wageni wengi wanadhani UTAMU wa samaki ni minofu, hapana UTAMU wa Sato Kumkichwa.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo ?
Hii ni sehemu tu ya safari ya Mwanakwetu kutoka ofisini kwake kwenda Mwalo wa Ziwa Victoria Novemba 21, 2025.
Msomaji wangu unapotazama duniani bei ya Kilogramu moja ya mnofu wa samaki ni kati ya senti 50 hadi senti 70 ya dola, huku hapa nchini Tanzania bei ya uzito huo ni kati ya dola mbili hadi dola tano. Jambo hili la bei ya juu ya samaki linasababisha wanaokula samaki hawa ni watu wachache, wenye uwezo wa kifedha huku sehemu kubwa ya jamii masikini ambazo zinakaa jirani na Ziwa Victoria wanakula dagaa ambapo kipimo chake kinaanzia shilingi 500/- na ndiyo maana ukizunguka katika mji wa Musoma utakuwa watu wengi wameanika dagaa hao jirani na nyumba zao na vigumu kuona mtu ameanika samaki wake hadharani iwe mbele ya nyumb au katika kichanja chake n ahata minofu ya samaki wakubwa inauzwa sokoni Musoma Mjini huku mitaani jambo hili ni adimu sana.
Mwanakwetu mpaka sasa anapokamilisha makala haya bado anakula samaki wake, huku mmoja keshammaliza, akijaribu kuonja utamu wa samaki Sato kutoka Ziwa Victoria. Kumbuka Mwanakwetu ana mwaka mmoja hapa Musoma Mini lakini hakuwahi kula samaki kama alivyobahati kuwapata hawa wa Novemba 21, 2025
Mwanakwetu Upo? Kumbuka
“UTAMU WA SATO KUMKICHWA.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257














Post a Comment