Ni majira ya asubuhi, huku jua likiwaka vizuri sana, upepo ukivuma kwa KM 14 kwa saa, hali joto ni sentigredi 26, ujirani na mvua ni asilimia 65 huku unyevunyevu ni wa asilimia 35. Mandhari mbele ya msimuliaji ni vijana wa tatu; wakike mmoja na wakiume wawili, hapa wakipata kifungua kinywa katika mkahawa mmoja wa watu wa wastani, huu siyo mkahawa wa matajiri wala makabwela.
Kijana mmoja wa kiume aliyevalia koti maridadi ambaye alionekana kuwa ni mpingaji mkubwa wa kila kilichokuwa kinaongewa na wenzake mara gari la mazungumzo likageuka na kijana huyu kusema haya;
“Lakini niache ubishi, ngoja niwaambieni tukio la kweli kabisa ambalo nimelishuhudia mwenyewe JUMAPILI HIII.
Tulikuwa tumekaaa KIJIWENI, mimi mwalimu mmoja na fundi, tukiwa pale mara tukasikia kishindo cha ajali.
Kwa bahati mbaya mimi na mwalimu hatukuweza kuona kilichotokea kutoka upande tuliokuwa tumekaa, huku sauti ya kishindo ikisikika vizuri sana.
Fundi kando yetu akawa anacheka, kisha tukawa tunasikia maneno ya watu wakipitia kando ya tukio na kuendelea na mambo yao, huku wengine wakfyonya, hawa jamaa wametuumiza sana, muacheni hapo hapo wala msiende kumnyanyau abaki hapo hapo mtaloni.
Fundi hapa tulipo akasema
Jamani pale kuna mtu mmoja na pikipiki yake kaangukia katika mtalu, jamani nyie watumishi ebu nendeni mkamuokea mtumishi mwenzenu ameanguka na pikipiki sasa hivi…”
Msomaji wangu kumbuka jambo moja kubwa kuwa hapa Mwanakwetu anasikiliza mazungumzo ya vijana watatu wakiume wawili na binti mmoja katika mkahawa ambapo kijana wa kiume mwenye koti nadhifu ndiye anayesimulia kisa hiki.
Kumbuka pia kijana wa kiume anasimulia na sasa wameshatoka mgundini na wanakwenda kumnyanyua mtaloni yule jamaa aliyedondoka na pikipiki yake.
“Tulipofika pale pikipiki bado inaunguruma na imetapakaa tope mtu hatumuoni, kwanza tukaizima pikipiki na kisha kuinyanyua kutoka mtaloni na kuiweka kando, alafu tukamtoa huyu jamaa aliyekuwa ndani ya mtalu na kumwambia pole sana kwa ajali hii uliyopata.”
Jamaa huyu anasimulia kuwa wakamuuliza jamaa huyu kama ameumia au la a…majibu yalikuwa ameumia kidogo na kupata mikwaruzo kiasi.
“Unajua jamaa kwa kuwa alikuwa ametapakaa na vumbi na matope awali sikuweza kumtabua vizuri lakini baadaye nikagundua kumbe ni POLISI KATA, nikasema pole afande, jamaa akashukuru sana alafu pikipiki yake akaiweka sawa, akajikumuta vumbi na matope kidogo na kisha kuendelea na safari.”
Vijana hawa watatu wakawa wanajadili pamoja kuwa jamani sasa hivi kweli nitaweza kuitisha mkutano wa KIJIJI juu ya Kilimo Bora wananchi wakaja kwa haya yaliyotokea tangu Oktoba 29, 2025 nchi nzima? Mmoja wao akasema kwa sasa ushauri ule wa Profesa Lipumba ni sahihi tuwe na serikali ya MPITO kuelekea Katiba Mpya kwa hali hii Mwenyeviti wote wa Vijiji CCM, Madiwani wote CCM wabunge wote CCM hakuna kitakachofanyika;
“Kukaa kimya kwa sasa ni kuwatesa watumishi wa umma wa ngazi za chini wakiwamo na POLISI wenyewe mbele ya wananchi. Wakubwa wasione wao wapo salama, wakumbuke usalama wa wengi ni muhimu zaidi ya usalama wa kundi la wachache.”
Mwanakwetu alimaliza kunywa chai kusimama na kutoka hapa mkahawani kisha kurudi zake alipokuwa.
Mwanakwetu upo? Kumbuka;
“Usalama wa Wengi Muhimu Kuliko Usalama wa Wachache.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
















Post a Comment