Lucas Masunzu – TABORA
Shule ya Sekondari Urambo iliyoko mkoa wa Tabora imeendelea kutia fora katika ubunifu baada ya kufanya mahafali ya kidato cha nne kwa mwaka 2025. Mahafali hayo yalifanyika tarehe 9 Oktoba 2025 yakihudhuriwa na wazazi, walimu, wanafunzi, na wageni waalikwa kutoka pembe mbalimbali za Tanzania.
Tukio hilo la mahafali lilibua taswira ya pekee kuwa shule hiyo ina ubunifu wa aina yake. Kwa hakika, siku hiyo iligeuka kuwa jukwaa la ubunifu na maarifa, huku macho ya wengi yakivutwa na onesho adimu la panya weupe wanaotumiwa katika maabara ya shule hiyo wakati wa kujifunza kwa vitendo.
Onesho hilo liliandaliwa na wanafunzi wanaosoma somo la Baiolojia shuleni hapo. Wanafunzi walionesha namna panya weupe wanavyoweza kutumika katika majaribio ya somo la Baiolojia. Walifafanua kuwa panya hao ni nguzo muhimu katika ulimwengu wa utafiti. Wakiongeza kuwa panya hao huwapasua ili wajifunze vizuri mifumo mbalimbali ukiwamo mfumo wa upumuaji, mfumo wa uzazi na mfumo wa chakula. Zaidi ya hayo, onesho hilo lilivutia hadhira kwa kuonesha namna ya kuwatunza panya hao kwa ustadi kwa kuwapatia lishe bora, kuwahifadhi katika mazingira tulivu na salama ambapo paka hawezi kuwafikia, vilevile mazingira salama huwazuia panya hao kutorokaIlifafanuliwa kitaalamu kuwa panya hao wakipatiwa lishe bora na wakaishi Katika bila hofu idadi yao huongezeka. Wafafanuzi hao waliongeza kuwa panya hao hawapaswi kuishi kwa hofu kwa sababu hofu ikiwazunguka kuzaliana kwa woga na idadi yao hupungua. Akizungumza katika hafla hiyo, Ibrahim Omary Kagete ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisifu ubunifu huo na kueleza kuwa;
“Wanafunzi wa Urambo Sekondari wameonyesha kuwa elimu ya vitendo ndiyo injini ya maendeleo. Hawa ndio wataalamu wa baadaye watakaoibua tiba na suluhisho kwa changamoto tele za dunia yetu.”
Kwa upande wake, Fundi Sanifu wa maabara wa shule hiyo, George Mollel alieleza kuwa shule imeweka mkakati kabambe wa kuimarisha mafunzo kwa vitendo licha ya kuwepo kwa changamoto ndogo ndogo. Fundi sanifu huyo aliongeza kuwa lengo kuimarisha mafunzo kwa vitendo ni kuwaandaa wanafunzi kuwa watafiti, wabunifu, na wagunduzi wanaoweza kuchochea maendeleo ya taifa hapo baadaye.
Pamoja na onesho hilo, siku hiyo ilipambwa na burudani kabambe zilizoandaliwa na kuratibiwa na mwalimu Hashimu Kavindi akisaidiana na Agata Penford ambao ndiyo washika usukani wa burudani shuleni hapo. Nyimbo, na utumbuizo uliyojaa ucheshi na mafunzo ulifunika anga la shule hiyo na kuunda hali ya shangwe, furaha, na kumbukumbu zisizofutika kwa kila mhudhuria. Nakutakia siku njema, Karibu Shule ya Sekondari Urambo.
theheroluke23@gmail.com |
0762 665 595.













Post a Comment