UNAWEZA KUDHANI HAUJAFIWA KUMBE UNA KILIO

 






Adeladius Makwega.

“Hali ni mbaya sana, risasi zilifika kwangu, kwa bahati tu mimi sikuwepo mbele ya biashara yangu, kaka nilikuwa nyuma ya nyumba yangu. Hali itakuwa mbaya sana kama huyu mama asipokaa na watu wenye nafsi nzuri, watu wake hawana nafsi nzuri, Watanzania wametulia tu kwa kuwa wanauwawa .”

Huyu ni Mtanzania ambaye tukio hili maandamo na mauwawaji limemkuta akiwa Dar es Salaam, anayasimulia haya yote kwa uchungu mno. 

Swali ni je huyu aliyekuwa anarusha risasi katika makazi ya watu alikuwa anataka nini? 

Kwa faida ya nani? 

Je mtu aliye nyumbani mwake nayeye alikuwa anaandamana?

Hata kama ndiyo alikuwa anaandamana je ulizungumza naye?

Je kwa sasa Watanzania hakuna mazungumzo baina ya raia na viongozi?

Haya ni machache tu maswali Mwanakwetu huku malalamiko juu ya vyombo vya habari vya Tanzania vikituhumiwa sana, hali hii inaonesha kuwa vyombo vingi vya Habari vya Tanzania vimepoteza Imani na vitakosa wa kuwatazama, wakusoma na hata kusikiliza kwa kuwa vimesaliti umma wa walio wengi umma wa masikini walioshambuliwa katika maandamano haya.

 

“Hali hii imeongeza chuki, 

watu wameandamnaa kuonesha hasira zao, matajiri wamekumbatiwa sana kipindi hiki, masikini wamechukia na wameandamana, tunajua kwa sasa matajiri wamekimbia, wamebaki vibaraka wao tu.

Sasa vibaraka wao wanatuuwa sisi masikini.

Kiongozi usipokuwa mpatanishi unajipotezea mamlaka ya kuongoza, kiongozi unayelalia upande mmoja, wewe siyo kiongozi, kiongozi mzuri huwa mpatanishi na hachagui upande.”

Kwa hakika hakuna mtu mwenye dhamiri safi anayeweza kusimama hadharani na kusema Watanzania hawajafariki katika seke seke hili, kama yupo mtu huyu , kama yupo mtu huyo na kama yupo mtu huyo dhamiri yake imekufa na lazima tuwe naye makini. 

Watu wamefariki huku wapo wengine wanaitafuta miili ya wapendwa wao, wapo waliyoipata miili hiyo na wapo wengine ambao hawafahamu kama wapendwa wao wamefariki au la na itachukua muda kujua kama wamefariki.


 

Kujua ndugu amefariki kunatokana na sababu nyingi; mojawapo ni kuwepo na mawasiliano mazuri baina na ndugu na ndugu, kwa zile familia za kimasikini sana zenye mawasiliano hafifu Mwanakwetu ana hakika itachukua muda kutambua vifo hivi maana Unaweza Kudhani Haujafiwa Kumbe Una Kilio.

Katika hoja ya miili ya wafu hawa Mwanakwetu alifuatilia namna miili ya ndugu hawa ilivyohifadhiwa katika mochwari zetu, katika hoja hii Mwanakwetu anataka kutazama namna ya kuhifadhi maiti kulivyokuwa katika hospitali zetu.

Mara nyingi maiti zilizofia nyumbani au hospitalini ndiyo huifadhiwa vizuri katika friji za hosptalini, kumekuwa na utaratibu kwa kutokujali maiti ziilizofia katika vurugu, maandamano na matukio ya fujo. Mara nyingi maiti hizi zinahifadhiwa tu sakafuni katika mochwari zetu. Kama matukio ya vifo ni mengi maiti hizi zinahifadhiwa chini sakafuni na holela tu mochwari na zinaweza hata kuoza.

Hali hii inasikitisha sana huku kukiwa kemikali za gharama nafuu katika kuhifadhia maiti.

Ukitaka kupima jamaa ya wastaarabu angalia namna wanavyohifadhi miili ya wafu wao.

“Katika Hospitali zetu ipo dawa moja inaitwa FORMALINI ambayo inaweza kununuliwa kwa ujazo wa lita 5 hadi lita 20, hiki kimiminika ambacho kinachotumika hospitalini kwa matumizi kadhaa ikiwamo kutunza maiti isioze.

Maiti moja ikishawekwa vizuri inaweza kudungwa kati ya CC 5 –CC 10 huku mtaalamu wa maabara lazima ausike wakati kimiminika hicho kinachanganywa na maji kabla ya kudunga maiti.

Maiti kuharibika hospitalini kunatokana na uzembe wa watu wasiojali ubidamu na baadhi ya watu wasio wataalamu wa afya kuingilia masuala ya afya kwa maslahi ya kisiasa.Maiti hata kama haipo katika friji watu makini wanaweza kuidunga FORMALINI na maiti ikabaki salama.”

Mwanakwetu wakati wa kadhia hii inaendelea aliwasiliana na daktari mmoja na yeye aliyasema haya ;

“Formalini hutumika katika mchakato wa  uhifadhi wa maiti (embalming) ili kuhifadhi kwa muda miili ya wafu kwa kuzuia kuoza, kuua bakteria, na kufanya mwili uonekane vizuri kwa ajili ya kuangaliwa. Kemikali hii hufanya kazi kwa kufunga tishu za mwili na kuzuia bakteria kusababisha kuoza. Formalini husafisha mwili, hapa kemikali hii huua bakteria na vijidudu vingine vinavyosababisha kuoza. Hufunga tishu:

Huvunja na kubadilisha protini za seli, na kuzifunga katika hali ambayo huzuia uharibifu. Hupunguza kuoza: Mchakato huu husitisha kuoza kwa kawaida, hivyo kuruhusu mwili kuonekana kwa muda mrefu zaidi. Huboresha mwonekano: Husaidia kudumisha umbo la asili la mwili na inaweza kuchanganywa na kemikali nyingine ili kuufanya uonekane kama bado una uhai.

Sababu za matumizi yake-Kuangalia maiti na mazishi: Kuhifadhi maiti kwa formalini huruhusu mwili kuonwa na ndugu na marafiki, na kuwapa muda wa kuaga na kuomboleza kwa heshima na utulivu. Hutumika kuhifadhi miili inayosafirishwa kwa umbali mrefu. Wakati mwingine formalini hutumika kuhifadhi miili kwa ajili ya masomo ya anatomia na utafiti wa kisayansi. Formaldehyde inajulikana kuwa kemikali inayoweza kusababisha saratani, hivyo matumizi yake yanahitaji tahadhari na kanuni kali za usalama ili kupunguza athari za sumu. Athari kwa mazingira: Maji ya kuhifadhia maiti yana kemikali ambazo zinaweza kuhatarisha mazingira.”

Kwa utafiti wa Mwanakwetu bei ya lita tano za kemikali hii ya FORMALIN hapa Tanzania kwa Oktoba –Novemba 2025 ni kati ya shilingi 50,000- 75,000 kama hesabu ya mwili mmoja ni kudungwa CC 10 maiti kuharibika nchini Tanzania ni jambo ambalo halikubaliki.


 

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Unaweza Kudhani Haujafiwa Kumbe Una Kilio.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 





 

 




 


0/Post a Comment/Comments