UNACHAGUA KOROMA UNAACHA MBATA!

 

Adeladius Makwega-MBAGALA.

“Ahahahahaha… yule Waziri wa Mwalimu Julius Nyerere? Yule Mbunge wa Kisarawe ?Namkumbuka sanaaa… anaitwa  Kighoma Malima , ndiyo mwanangu nilifanya naye kazi kijijini kwao kabisa kunaitwa Mkerezange kwao ni Kata ya Mkamba.

Wewe ulikuwa mdogo sana nadhani hata darasa la kwanza ulikuwa haujaanza, ile ni mwaka 1981/ 1982.

Unajuaaaa…! nilifanya kazi Mpwapwa tangu mwaka 1974 sasa mwaka 1981 mwishoni nikasema nikikaa sana Dodoma, kule nyumba Dar es Salaam nitakuwa sina maendeleo, ebu nirudi nyumbani Mbagala. Nikakata shauri kuuza mbuzi zangu 300, kondoo zangu 100 na ng’ombe zangu 50 nikaziswaga hadi Gulwe pakiza katika treni hadi Vingunguti Dar es Salaam na hawa baba zenu wadogo Primus Makwega na Edegari Kavuruga zikashushwa na Vingunguti nikaziuza hapo hapo nikafuatili uhamisho nikapata… hawa jamaa wa elimu wajinga sana …washenzi kabisa wakanipangia Wilaya ya Kisarawe Kijiji cha Mkerezange na kuwa mwalimu Mkuu, madarasa yenyewe ni makuti na juu yamefunikwa viungo…

Yule Waziri wa Nyerere alikuwa msomi mzuri, waziri mzuri lakini udhaifu wake alikuwa anahangaika sana na akina mama tu…na akijipenda mwenyewe tuu…lakini mwanangu huu ni ubinadamu  na shida ya wanaume wengi ni udhaifu wa akina mama …”

Msomaji wangu haya ni maelezo ya mazungumzo ya simu baina na Adeladius Franicis Fidelis Makwega akiwa Musoma Mkoani Mara na baba yake mzazi mwalimu Franicis Fidelis Makwega akiwa Dublin Ireland mwishoni mwa mwaka 2024.

Siku hii baba na mwana walizungumza mengi ikiwamo hali halisi ya ukanda ya Ziwa Victoria ulivyo kwa mwaka 2024 na hali ya Ukanda ya Ziwa Victoria ilivyokuwa mwaka 1974 maana Francis Fidelis Makwega na Doroth Hezron Mlemeta (wazazi wa Mwanakwetu) walifunga Ndoa Takatifu Parokia ya Nasio Murutunguru Ukerewe Mwanza huku hata Mwanakwetu (Adeladius Makwega ) alibatizwa katika parokia hiyo hiyo.

Msomaji wangu haya ni historia tu, kikubwa Profesa Kighoma Ali Malima alikuwa ni waziri mwenye uzoefu mkubwa na uwezo mkubwa, huku Waisilamu wa Tanzania Bara (Tanganyika waliamini kuwa Profesa Malima alikuwa ni mtu ambaye angeweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awali akishika nyadhifa kadhaa kubwa na za Uwaziri kamili ikiwamo Wizara ya Elimu ambayo iliyoongozwa na watu makini kama yeye na akina David Mwakawago, Jackson Makweta na wengine wengi.

 

Mara baada ya ujio wa Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1985 kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitokea Zanzibar baada ya kung’atuka Julius Nyerere, miongoni mwa Mawaziri waliopotea katika medani ya siasa ni Profesa Kighoma Malima yule yule aliyetajwa na baba wa Mwanakwetu awali katika makala haya ndani ya yale mazungumzo ya simu ya mwishoni mwa mwaka 2024.

Ali Hassan Mwinyi mwenyewe anajua kwanini jina la Profesa Kighoma Malima halikushamiri baada ya ujio wake huku wakati alikuwa Muisilamu mwenzake, huku kwa asili wakitokea wilaya moja ya KISARAWE kwa asili Ali Mwinyi akitokea Tarafa ya Mkuranga huku Kigoma Malima akitokea Tarafa ya Mkamba.

 

Huku baadaye Profesa Kighoma Malima hadi anafariki dunia.

Msomaji wangu kipindi hiki hiki , hiki hiki ndicho Jakaya Khalifani Kikwete anaibuka na kuanza kupanda ngazi haraka haraka, tangu waziri mdogo hadi waziri kamili na baadaye kutia nia na Benjamin Mkapa urais mwaka 1995.

“Hili ni jambo la kushangaza sana Benjamin Mkapa Waziri makini alipaswa kupambanishwa na magwiji wenzake wa kisiasa , inafahamika Mkapa alikuwa Mkatoliki mtoto wa KATEKISTA , magwiji wenzake ni akina Profesa Kighoma Malima watoto wa MASHEKHE,Wandengereko wanawafahamu vizuri WAMAKONDE kuliko WAKWERE lakini mwaka 1995 anapambanishwa na Bwana Mdogo ambaye hakuwahi kuteuliwa na Julius Nyerere kwa hata kwa Ukuu wa Wilaya?

Wakati huo Profesa Malima ameshalala kaburini kwao Mkamba, nalo kaburi lake likiwa limezungukwa na miti ya ndimu, minazi mikorosho na miembe ya baba na babu zake, likiwa kaburi lisilo na thamani tena katika ulimwengu wa siasa za Tanzania.”

Kupotea kwa Profesa Kighoma katika medani ya siasa na hata katika ulimwengu wa wanasiasa kutoka kutoka Pwani ya Tanzania na hata wanasiasa Waisilamu wa Tanzania ndipo kuliposaidia kuibuka kwa jina jipya na kipenzi cha Rais Ali Hassan Mwinyi huyu ndugu Jakaya Khalifan Kikwete.

Msomaji wangu naomba niseme hivi;

“Kama kwa maamuzi haya Rais Ali Hassani Mwinyi alifanya kosa basi wa kulaumiwa ni yeye huko huko alipo… na lawama hizi zimfikie.

Watu wa Mkuranga huwa wana msemo huu, hauweza kuchagua KOROMA na Kuiacha MBATA.Mama Koroma hauwezi kuingia mboga?Ukipikia Koroma watu wataumwa matumbo , nani atakula chakula hicho?

Koroma ni hatua ya ukuaji wa nazi baada ya dafu ambayo haifai kupikia baada ya Koroma ndipo inakuja nazi na kisha MBATA

Je Tanzania Hodari wa kuchagua KOROMA badala ya MBATA?”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Nakuomba msomaji wangu pata picha yaliyomo katika makala haya, huku ukitilia maanani kuondoka kwa jina la Seleiman Jafo(PHD) katika Uwaziri huku jina la waziri wa Kutoka Jimbo la Chalinze linapandisha ngazi haraka haraka. Je kisa hiki hakilingani kabisa na kile kile cha Ali Hassan Mwingi na Profesa Kighoma Ali Malima miaka ile ya tisini?

 

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Tanzania Hodari Kuchagua Koroma Badala ya Mbata.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius @gmail.com

0717649257

 NB Makala haya ni maalumu kwa Wakazi wa Kijiji cha Mkerezange ambapo Mwanakwetu alisoma Shule ya Msingi Mkerezanga darasa la Chekechea mwaka 1982.






















 


0/Post a Comment/Comments