Adeladius Makwega-MBAGALA
Ndugu Jally Willy Mongo wanachuo wa Shahada ya Uzamili ya Sheria aliyejitambulisha kuwa anatoka Chuo KIkuu cha Tumaini Iringa kuna wakati fulani aliandika andiko lake ambalo lilipewa anuani hili-Domestication of the Rome Statute in the United Republic of Tanzania ambapo kwa Tafsiri ya Kiswahili cha Mbagala cha Mwanakwetu tunaweza kusema kuwa Uhalalishaji wa Mkataba wa Roma katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndugu Jally Mongo katika andiko lake hili aya yake ya pili wakati akilipiga chapuo la utangulizi aliyasema maneno haya;
“Uhalilishaji wa Mkataba wa Roma hutimiza madhumuni makuu mawili: Kwanza, unaipa mamlaka Nchi Wanachama kutumia uwezo wao wa msingi wa kuchunguza na kushtaki makosa ya kimataifa yaliyobainishwa—ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa uchokozi—kwa lengo la kuzuia kutekelezwa kwa makosa hayo.
Pili, unaipa Nchi Wanachama uwezo wa kisheria wa kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC’) ambayo inakamilisha mamlaka ya mahakama za kitaifa katika kuchunguza na kushtaki makosa ya kimataifa.”
Ndugu Jally Mongo akaongeza kasi ya mapigo ya chapuo lake na kusema haya;
“Kuna mauaji mengi nje ya utaratibu wa
kisheria, mateso, utekaji, na kuwakamata watu kiholela—hasa watu wenye ualbino,
viongozi wa dini wa hata wa kisiasa—yanayodaiwa kutekelezwa katika maeneo
mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inaripotiwa kuwa mwaka 2018,
takribani Waislamu 380 hawakuweza kupatikana tangu mwaka 2017, hivyo wabunge wa
Tanzania walikuwa wakisukuma kufanyika kwa uchunguzi kuhusu tuhuma hizo kwa
kuwa maafisa wa serikali (vyombo vya ulinzi na usalama) walishukiwa kuhusika
katika utekaji wa ndugu hao.
Mauaji na mateso ya kikatili kwa kuwakatakata viungo watu wenye ualbino—hasa
watoto na vijana—yalianza kusambaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
mwishoni mwa miaka ya 2000…”
Ndugu Jall aliongeza na hili,
“Shirika la Amnesty International liliitaka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchunguza mauaji nje ya utaratibu wa kisheria pamoja na vitendo vya mateso na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria kwa viongozi na wafuasi wa vyama vya upinzani kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020. Asasi za kiraia na makundi mengine yaliwatuhumu maafisa wa usalama kuua watu 22 nje ya utaratibu wa kisheria. Pia iliripotiwa kuwa viongozi na wafuasi 77 wa vyama vya upinzani walikamatwa na kuwekwa kizuizini kimakosa tangu siku ya uchaguzi. Zaidi ya hapo, baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka wa 2020, malalamiko ya uhalifu dhidi ya ubinadamu unaodaiwa kufanywa na maafisa wa juu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya raia yaliwasilishwa huko ICC yakitaka uchunguzi maalum. ICC ilithibitisha kupokea barua mbili rasmi zilizodai ukiukaji wa haki za binadamu. Barua hizo mbili zilitoka kwa Chama cha ACT-Wazalendo—chama cha upinzani—na nyingine kutoka kwa Maria Sarungi Tsehai, mwanaharakati huru wa haki za binadamu…”
Pia ndugu Jally katika nadiko lake aliongeza na hili;
“Ripoti za Human Rights Watch zinaeleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haijafanya uchunguzi kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa 2020. Ripoti ya Haki za Binadamu ya Tanzania ya mwaka mmoja baadaye yaani 2021 inaonyesha kuwa, kwa mujibu wa viongozi wa upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali, kulikuwa na angalau wanaharakati na wafuasi 100 wa upinzani waliowekwa kizuizini kinyume cha sheria au kutekwa katika Tanzania Bara… kabla na baada ya uchaguzi mkuu wa 2020.
Mifano hii michache ya ukiukaji wa haki za binadamu
inaangukia katika uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari. Hivyo,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalazimika kutunga sheria ya kuuhalilisha
Mkataba wa Roma ili:
Kwanza, kutekeleza wajibu wake wa kimataifa kwa nia njema kama ilivyoainishwa
chini ya Mkataba wa Roma, kama njia ya kutambua wajibu wake chini ya Mkataba wa
Roma na sheria ya kimataifa ya mikataba. Pili, kuhalalisha makosa hayo matatu
na kuyaingiza katika sheria za Tanzania kutakuwa ni ishara ya kujitoa
kikamilifu kuyatekeleza, kulinda, kuhifadhi na kuendeleza haki za binadamu.ata,
kuingiza makosa hayo katika sheria za Tanzania kutakuwa ni kutekeleza matakwa
ya ibara ya 63(3)(d) ya Katiba ya Tanzania inayohitaji uhalilishaji wa mikataba
ya kimataifa, ikisisitizwa na ibara ya 13(6)(c) ya Katiba ya Tanzania
inayokataza matumizi ya sheria kwa mwendo wa nyuma (retroactive application).
Nne, kutochunguza na kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi ya makosa hayo kutailazimu ICC kuingilia kati, jambo ambalo linaweza kuathiri usalama na mamlaka ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Bila ya shaka msomaji wangu umeelezwa vizuri kilichopo katika andiko la ndugu Jall Mongo andiko lake la miaka mingi nyuma juu ya hali hii ya Tanzania na ICC.
Mwanakwetu anasema nini Siku ya leo?
Kwa hakika Mwanakwetu anaomba kugusia jambo moja tu katika makala haya ambapo ndugu Jall Mongo anasema maneno haya;
“…kutochunguza na kutochukuliwa hatua za kisheria dhidi ya makosa hayo kutailazimu ICC kuingilia kati, jambo ambalo linaweza kuathiri usalama na mamlaka ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Unapokuwa kiongozi jambo linaposemwa lifanyie kazi, lisipofanyiwa kazi huwa ni kosa kunaweza zaliwa makosa mengine makubwa kupitia namna mlivyofanyia kazi jambo kama hili awali na hiki ndicho kinachokuja kutokea Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu nchni Tanzania na matokea yake baada ya uchaguzi huo.
Kwa kumalizia msomaji wangu nakuomba nikukumbushe maelezo haya ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Juni 3, 2009 miaka 16 iliyopita namna ailivyokuwa ikitazama masuala haya ya uhalifu wa kimbari uhalifu wa kimataifa.
“We have UN-standards prison facilities and courts in Arusha,”
Waziri wa Sheria na Katiba wa Tanzania, Mathias Chikawe, aliieleza Shirika la Habari la Hirondelle kupitia mahojiano ya simu kutoka Dar es Salaam.Bw. Ndugu Chikawe alitoa ofa hizo wakati wa mkutano wake na Rais wa ICC, Sang-Hyung Song, aliyekuwa ziarani siku ya Jumanne.
“Tulikuwa na mazungumzo ya uwazi na ya moja kwa moja,”
Akijibu kauli ya waziri, Chaikawe Rais wa ICC Sang-Hyung Song alisema mahakama ingetafakari ofa ya serikali ya Tanzania
“Tutaiangalia Arusha kwa shughuli zetu zijazo,”
Alisema Rais wa ICC, ambaye aliandamana na Phakiso Mochochoko, mshauri mwandamizi wa masuala ya kisheria wa ICC. Kiongozi huyo wa ICC pia alifanya mazungumzo na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, kabla ya kuondoka nchini usiku wa Jumanne.
Kwa hakika Umoja wa Mataifa na washirika wake wametumia mamilioni ya dola kujenga mahakama na magereza huko Arusha kwa ajili ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994. Magereza hayo, yaliyopo pembezoni mwa mji wa Arusha, yana uwezo wa kuchukua wafungwa 90 kwa wakati mmoja. Pia yana ukumbi wa mazoezi, maktaba, ukumbi wa kulia chakula, chumba cha matibabu na vyumba vya ziara za kifamilia. ICTR imejenga mahakama nne za kisasa katika jengo la Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC) katikati ya jiji la Arusha. ICTR pia imeweka eneo kubwa la maegesho kwa ajili ya majaji na maafisa waandamizi wa mahakama na imeweka mifumo ya mawasiliano na teknolojia ya habari ya kiwango cha kimataifa. Pia imeanzisha maktaba na kituo cha kompyuta chenye vifaa vya kutosha.
Msomaji wangu mwaka wa 2009 wakati Serikali ya Tanzania inatoa ofa hii kwa ICC kuyatumia majengo na magereza ya Arusha dhana ilikuwa kama wakosaji ni wengine.
Ndugu yangu Mateo Chikawa kwanza shikamoo.Mwanakwetu ninatambua ungamo la Mateo Chikawe kwa Rais wa ICC mwaka wa 2009.
Msomaji wangu tambua kuwa unaweza ukatoa eneo ikajenga mahakama na hata kujengwa gereza kisha mahakama hiyo hiyo , gereza hili aliyetoa eneo akawa miongoni mwa watakaokaa na kuishi humo.
Mwanakwetu upo? Kumbukal
“Tanzania ina Mahakama na Magereza Viwango Vya Umoja wa Mataifa ,”
Nakutakia siku njema.
0717649257























Post a Comment