Adeladius Makwega
Tangu mwishoni mwa mwaka wa 2015 hadi Machi 2021 Tanzania ikiwa chini ya marehemu John Pombe Magufuli kwa nafasi ya urais, taifa hili ilionekana kuna mapambano baina ya utawala huo na matajiri.
Kuliona hili unaweza kupitia majina kadhaa ya matajiri wa Tanzania ambayo yalitembelea vizimba vya mahakama, mahabusu na hata magerezani. Hili halina ubishi na ushahidi wa hili utabakia katika shajara za mahakama na hata shajara za mahabusu na magereza taifa hili lililotawaliwa na Mjerumani na Mwingereza baadaye.
Mara baada ya Kifo ya John Pombe Magufuli hali hii ilibadilika na hata hiki kilichoonekana wakati mgombea wa urais wa CCM mwaka wa 2025 akikusanya matajiri na kumchangia mabilioni ya fedha na hata baadhi ya matajiri hao kusimama hadharani mbele ya mashine za kurekodia na kamera kujinasibu kwa mambo mengi, huku kundi na masikini likioneka kulalamikia hali hii nakuwa Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimetekwa na matajiri na masikini hawana chao.
Hapa kukiwa na ulimwengu mbili; John Pombe Magufuli na Masikini huku Samia Suluhu Hassan na Matajiri, huku kwa ukweli wa Mungu Masikini na Matajiri ni sawa na Mbingu na Ardhi, japokuwa kila upande unamuhitaji mwingine.
Chama kile kile cha siasa kilichopambania ukombozi kikioneka kimewaadaa Watanzania ambao vizazi vyao vilishiriki kuunda ASP na TANU na hata kushiriki harakati za ukombozi kupambana na ukandamizaji hata Watanzania wengine kufariki wakipambania harakati hizo. Je iweje sasa harakati za ukombozi zimekufa kifo cha Mende?
Chama kile kile kilichotunga nyimbo, ngojera, mashairi na vitambu juu ya ukombozi sasa kumekuwa bubu,kimewatupa Watanzania masikini na sasa kimekuwa mufilisi kupinga ukandamizaji wa mtu mnyonge? Huku madai na shutuma kwa vyombo vya dola hasa POLISI yakidaiwa kufanywa kama yale yale ya MAKABURU.
“Hata hili zoezi la kupiga kura kama wananchi wameweza kugomea kupiga kura maana yake taarifa za vyama vya upinzani zinafika kwa wananchi, zamani hali haikuwa hivyo, hizi kura zilizotangazwa, tuache unafiki, hii ni dhambi, mimi ninaamini hizi ni kura za kuchanja, kura za usiku na kura za wataalamu. Hoja ni hii kama Watanzania kweli wangepiga kura ni kati ya milioni 5 hadi 10 tu siyo hizo zilizotangazwa.
Nusu ya Watanzania wapige kura kisha wakaandamane na wapigwe risasi? Hili siyo kweli, jamani tuwe wakweli, hapa duniani hatukai milele, tutaishi tu kwa kipindi kifupi, KWA KIPINDI KIFUPI sana. Kama Watanzania wamegomea uchaguzi na kama kiongozi wa juu kakataliwa, basi tume hii ya uchaguzi imekataliwa, Polisi pia wamekataliwa, nani wa kuliongoza jahazi ambaye anaaminika?
Je wakubwa wana busara? Kama busara inngetumia tusingalifika hapa,nina hakika hawahawa hata leo na kesho yao aina busara.
Angalia tu Mkuu wa Majeshi sasa ameitisha hali ya dharura lakini hakuna jipya.
Shida ipo kwa Rais na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Samia Suluhu Hassan yeye mwenyewe, yapo madai ameshindwa kujibu hoja za watu wake anaowaongoza.
Kwa hali hii bado vurugu zinaendelea na Watanzania sasa wanatoka kweli. Mimi nina njaa na familia yangu haina kitu, nitakaa ndani nife kwa njaa? Hata hayo matamko ya maana hayapo na hawasemi kitu…hata redio haziruhisiwi kusema chochote, nasikia wahariri kumbe waliitwa…hii ni changamoto. Mtu ambaye ndugu yake amevunjwa miguu, mtu ambaye ndugu yake ameuwawa unamwambia nini kwa sasa juu ya CCM leo hii…?
Jakaya Kikwete ameharibu chama. Yeye mwenyewe anaweza kuona madhara yake ni madogo kwa kutumia vyombo vya dola na hata wao Polisi watachoka, maana migogoro hii hauwezi kusema POLISI wako salama, POLISI na wao hawako salama.
Ndio maana CHADEMA walitaka reforms, huyu anayetangaza matokeo ameteuliwa na rais, huyu anayelinda uchaguzi ameteuliwa na rais, ukihoji mahakamani unakutana na akina Jaji Mwambegele ameteuliwa na rais, je haki utaipatia wapi?”
Haya ni maelezo ya kina ya mwanachama cha CHAMA CHA MAPINDUZI nchini Tanzania.
Kumekuwa na mshangao juu ya wakubwa ndani ya CCM kukataa kusikiliza,na wanachama wao wanasema nini katika hili?
“Wakubwa wangesikilizana tu, wangesikiliza tu, mathalani Humphrey Polepole si mwanachama mwenzao, tangu aliposema wangemsikiliza tu, mbona mambo yalikuwa ya kawaida. Wananchi wanataka kuandamana umewapiga risasi, umewauwa…hatari hii hapa CCM inachafuliwa.
Kwa sasa ofisi ya CCM hatujafungua, sisi ndiyo watuhumiwa, hatuwezi kufungua ofisi hizi. Wananchi mitaani na vijijini watakutazamaje? Watoto wao wamefariki, watoto wao wameumizwa , sisi ndiyo watuhumiwa lazima tukae mbali na hizi ofisi maana mabosi wetu ndiyo waliyoyafanya haya na japokuwa wameyafanya haya kwa maslahi yao wenyewe na maslahi ya watu wachache wakijitazama wenyewe.
Walengwa ni CCM, Mwenyekiti wa chama taifa hatuwezi kumuhoji, hili ni kosa kubwa, kosa la mwenyekiti kwa sasa limezamisha CCM, kama Mwenyekiti wa CCM asingekuwa yeye, nina hakika angeitisha kikao cha chama cha dharura, hapo wajumbe wa Kamati Kuu kwa sasa ni mabubu hawana uwezo wa kumohoji Samia, hakuna hata mmoja mwenye uwezo kuhoji na wala kuitisha kikao huyo Katibu Mkuu kachaguliwa nayeye.
Sasa naona ni jambo sahihi kama wanavyofanya ANC ya Afrika ya Kusini Rais wa Afrika ya Kusini ni Mjumbe tu katika Kikao cha juu ya ANC,
Rais Samia angekuwa ni mjumbe wa Kamati Kuu tu na siyo mwenyekiti wa CCM angehojiwa kikaoni na kama hana majibu yanayoeleweka angefutwa uanachama, kisha tungeingia katika uchaguzi …suala hili lililotokea lingefuata mkondo wa sheria. Sasa mpaka sasa CCM imefanya hivyo? Nani anayeweza kufanya hivyo kwa sasa ndani ya hii CCM ?
Kwa sasa shida ni Rais na Mwenyekiti wa CCM,yeye mwenyewe ameshindwa kuweka usawa baina ya Polisi na wananchi, huku akitumia matumizi ya nguvu kwa raia wake ambao hawana silaha. Mwenyekiti wa CCM anachangamoto tele, sasa watu wanaandamna unasema mkiandamana mtaona cha moto , wewe ndiyo kimbilio, watu wamkimbilie nani? Sasa Tanzania hakuna kimbili.
Shida ya yote haya Rais ana mamlaka makubwa kwa kuwa hata kama rais hamtaki kiongozi mwingine anaweza kumuondoa anavyotaka ni heri Rais angekuwa ni Mjumbe tu Kamati Kuu.”
Mwanachama huyu wa CCM wa Dar es Salaam nchini Tanzania pia anaitazama hali ilivyo kwa sasa jijini humo.
“Unga sasa ni kilo ni shilingi 4000, mchicha kitita ni kati ya 2000-4000/-. Hali ni ngumu boda boda umbali mdogo ni shilingi 10,000/-.Kwa sasa Jeshi la Polisi Tanzania limepewa nguvu mno. Polisi ukikutana naye bila sababu anakurusha kichurachura bila sababu, unaweza kukutana na polisi na wewe upo katika boda badoboda anapiga risasi …ni heri JWTZ wangesambazwa maeneo yote.
Polisi akimuona mwananchi anahofia usalama wake kwa kile kilichotokea na kinachoendelea nayeye mwananchi hivyo hivyo akikutana na Polisi anahofia.
Kwa haya yote sasa CCM imekufa kabisa, ofisi za CCM hazifunguliwi na kila mmoja anazikwepa, hizi mali za CCM zirudishwe tu serikalini maana wananchi waliweka nguvu zao.
Mimi Balozi wa nyumba kumikumi namwambia nini mwananchi kwa hali kama hii?Wakubwa wameangalia nafsi zao tu wakubwa wameharibu chama chetu.”
Msomaji wangu, haya ni machcahe tu kati ya mengi yaliyokusanywa na Mwanakwetu tangu ile saa 1400 mchana hadi saa 0000 ya usiku ya Novemba 2, 2025.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu anatambua kuwa hata wewe msomaji wake unayo mengi yanayotokea hapo ulipo katika kipindi hiki kigumu ambacho Tanzania Bara inapitia.
Mwanakwetu anaona ni muhimu sana akatilia mkazo jambo moja ambalo limesemwa na huyu mwanaCCM hapa nalinukuu;
“…sasa Jeshi la Polisi Tanzania limepewa nguvu mno. Polisi ukikutana naye bila sababu anakurusha kichurachura, bila sababu, unaweza kukutana na polisi na wewe upo katika boda badoboda na akapiga risasi.
Polisi akimuona mwananchi anahofia usalama wake kwa kile kilichotokea na kinachoendelea kutokea nayeye mwananchi hivyo hivyo akikutana na Polisi anahofia…ni heri JWTZ wangesambazwa zaidi mitaani…”
Hili Mwanakwetu analilisitiza na ndiyo ukweli hata maeneo aliyopo Mwanakwetu hili analithibitishwa. Wananchi wakimuona askari wa JWTZ wanamsalimia na kisha wanazungumza naye kwa ZERO DISTANCE wanajieleza lakini pale akioneka polisi hawawasalimii wanawapita tu na tena kwa umbali mkubwa. Katika hali kama hii JWTZ waangalie cha kufanya na pia Wazee wenye kuheshimika wanatakiwa kusimama imara ili Tanzania ipone, viinginevyo ni misiba zaidi huku ikumbukwe kuwa wapo wananchi kadhaa waliokamatwa katika kadhia hii, walioumia katika kadhia hii je wanapata huduma stahiki ? Je hali yao ikoje? Kulinda usalama pande zote mbili yaani Raia na Polisi Mwanakwetu anaunga mkono asilimia mia moja ya kusambazwa zaidi JWTZ mitaani na Vijijini kote.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka:
“JWTZ LISAMBAZWE ZAIDI MITAANI.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257









Post a Comment