MJOMBA UADILIFU NI ZAIDI YA KUHESHIMU SHERIA BINI KATIBA

 


Adeladius Makwega-MBAGALA

Mjadala huu ulikuwa mkali mno, huku ndugu mmoja akauliza swali hili etii kwani yule ni kabila gani ? Mwanakwetu akajibu kuwa yule ni Mgogo. Ndugu huyu akauliza swali lengine kwani Wagogo wana akili? Mwanakwetu akasema kwanini unauliza swali hilo? Mbona kila kabila lina watu wenye tabia zote.

 

Ndugu huyu akasema;

“Wagogo wana shida kama unakumbuka kipindi cha Rais Ali Hassan Mwinyi, Mwalimu Julius Nyerere akiwa amestaafu aliyatoa maneno makali dhidi ya John Samweli Malecela na hadi jina lake likaondolewa wakati wa mchakato anagombea Urais mwaka ule 1995 ndani ya CCM. Wamemjua yule ni Mgogo wakafanya wawanavyotaka wao, ona sasa huku tulipofika! Nakwambia kabila lingine lisingeweza kukubali hali hii.”

Mwanakwetu akacheka, kisha akamwambia huyu jamaa hata mimi nina damu Ugogo, mama yangu ni mdogo baba yangu ni Mpogolo. Ndugu huyu akacheka sana, kisha akasema kwa kushangaa wewe Mwanakwetu Wagogo Wana Akili! Ushukuru Mungu umechanganya damu wewe siyo puwaa Mgogo.

Mwanakwetu akawa anasikitikia moyoni tu inakuwaje mama zake, wajomba zake, bibi zake na babu zake wanabebeshwa mzigo huo kwa makosa ya wengine? Mbona anawafahamu Wagogo  wengi wenye akili Mathalani Askofu Mandinda, Askofu Mtetemela, Balozi Job Lusinde na wengine wengi? Mjadala huu ukahamia katika hoja ya kufuatwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mbona wao wakiona Katiba inawabana wanabadilisha? Sheria siyo kila kitu na ndiyo maana Sheria zinabadilishwa kulingana na matakwa ya jamii husika.

 

Mjadala ulikuwa mtamu sana kisha kukasimuliwa kisa hiki;

“Kuna taifa moja lilikuwa katika vita vya wenyewe bini wenyewe, mambo haya ya migogoro yakapamba moto na kukawa na matukio kadhaa ya aibu. Matukio haya yakapamba moto, wakavamia nyumba moja ya Watawa wa Kike na inadaiwa kuwa wakabakwa. Baada ya hali kutulia iligundulika kuwa baadhi ya watawa walipata ujauzito kutokana na tukio hili. Swali likawa je watawa hawa Kanisa linafanyaje? Sheria mtawa harusiwi kushiriki mapenzi na wala kuzaa hawa watawa wamebakwa na wamepata ujauzito, Kanisa linfanyaje? Je wanafungasha virango vyao kurudi majumbani kwao wakalee ujauzito na watoto wao? Hoja hii ikapelekwa kwa Baba Mtakatifu ambaye alitajwa hapa kuwa ni Mtakatifu Yohane Paulo wa II(zamani Kadinali Carol Woytila). Mezani sheria iko wazi dhidi yao, hawapaswi kuendelea na utawa maana mtawa katika Kanisa Katoliki lazima awe mseja. Kadinali Carol Woytila akiwa Baba Mtakatifu akaamua hawa watawa wajifungue, wakajifungua salama, wakaruhusiwa kuendelea na utawa huku watoto waliozaliwa wakawa wamepatikana Shambani mwa Bwana na wakawa mali ya Kanisa.”

Mazungumzo haya yaliendelea na kujadili mambo mengine ya kidunia, kisha kila mmoja kuendelea na mambo yake.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

“Kauli ya kwamba uadilifu ni zaidi ya sheria inaungwa mkono sana katika mijadala ya kisheria na kimaadili. Wakati sheria inapoweka viwango vya chini vya tabia. Hapa uadilifu ni dhana pana zaidi inayohusisha kushikamana na kanuni za juu za maadili na maadili mema, hata pale ambapo haitakiwi kisheria/Kikatiba au hakuna mtu anayeshuhudia. Hapa sheria huweka msingi wa tabia inayokubalika, mara nyingi ikitoa wajibu wa raia au wa jinai kwa vitendo visivyo vya uaminifu. Hata hivyo, uadilifu unahitaji kiwango cha juu zaidi cha mwenendo ambacho kinahitaji kushikamana na kanuni ya kimaadili na ya kibinafsi au ya kitaaluma inayozidi utii wa sheria pekee. Mtu mwenye uadilifu hufanya mambo kulingana na imani yake ya ndani na uadilifu wake wa kimaadili. Kwa upande mwingine, sheria ni mkusanyiko wa kanuni za nje zinazotekelezwa na taasisi, bila kujali imani binafsi za mtu. Uadilifu mara nyingi huelezwa kama fadhila au thamani ya msingi inayojumuisha uaminifu, uadilifu, na uwajibikaji. Sheria, hata hivyo, zinaweza kuwa matokeo ya maafikiano ya kisiasa/kivikundi na wakati mwingine zinaweza kukosa kufikia haki kamilifu.”

Hapa tunaweza kusema kuwa mtazamo wa UADILIFU ni zaidi ya SHERIA/, hata hii KATIBA nayo ni SHERIA pia. Katika makala haya msomaji wangu kumbuka kimetajwa kisa cha Wagogo na lile swali aliloulizwa Mwanakwetu kuhusu wajomba zake;

“…wana shida kama unakumbuka kipindi cha Rais Ali Hassan Mwinyi, Mwalimu Julius Nyerere akiwa amestaafu aliyatoa maneno makali dhidi ya John Samweli Malecela na hadi jina lake likaondolewa wakati anagombea Urais mwaka ule 1995 mchakato ndani ya CCM… ni Mgogo wakafanya wawanavyotaka wao, ona sasa huku tulipofika!”

Msomaji wangu kumbuka pia kisa kile kilichotajwa juu ya watawa wale wa kike;

“…Kadinali Carol Woytila akiwa Baba Mtakatifu akaamua hawa watawa wajifungue, wakajifungua salama, wakaruhusiwa kuendelea na utawa huku watoto waliozaliwa wakawa wamepatikana Shambani mwa Bwana…”

Katika visa hivi tangu ule uvamizi wa makazi ya watawa wale na kuwabaki ule haukuwa uvamizi kwa watawa tu bali pia ulikuwa uvamizi wa shetani dhidi ya Kanisa na ndiyo maana Kadinali Carol Woytila akiwa Baba Mtakatfu  Mwanakwetu anaamini kuwa kama kisa hiki cha kweli alifanya maamuzi mazuri kwa manufaa ya Kanisa la Mungu na hata hili la kuwashambulia kwa risasi raia wasio na silaha wawe wanaandamana au wawe katika makazi yao, siyo uvamizi wa raia tu huo ni uvamizi wa nchi hivyo kiongozi Mkuu wa Vyombo vya ulinzi na Usalama umetimiza vipi wajibu wako katika hili? Jiulize kama haukutimiza wajibu wako maana yake unadhani ni haki kuendelea kulipwa mshahara na hiyo jamii husika inayolia misiba kila kona? Ni kweli SHERIA na ni Kweli KATIBA lakini kuwadungua raia wasio na silaha kwa bunduki hilo ni SHERIA na KATIBA, kumbuka kitendo hicho siyo UADILIFU. Ukumbuke kuwa Mwanakwetu anaamini kuwa UADILIFU ni zaidi ya SHERIA BINI KATIBA.

“…hapa uadilifu ni dhana pana zaidi inayohusisha kushikamana na kanuni za juu za maadili na maadili mema, hata pale ambapo haitakiwi kisheria au hakuna mtu anayeshuhudia…”

Ndiyo maana mama huyu anauliza swali hili la Je Wajomba wa Mwanakwetu wana Akili? Mwanakwetu anaamini kuwa wapo wajomba zake wenye tabia mbalimbali nzuri kwa mbaya na huo ndiyo ubinadamu maana Mjomba UADILIFU ZAIDI YA KUHESHIMU SHERIA BINI KATIBA.


 

Mwanakwetu Upo? Kumbuka

“MJOMBA UADILIFU ZAIDI YA KUHESHIMU SHERIA BINI KATIBA”

Nakutakia Siku Njema.

………………………………………………………………………………………………………

NB Msomaji wangu kisa hiki cha WATAWA nilichojaribu kukinukuu katika makala haya kama nilivyosimuliwa, naomba kwa wale wanaofahamu Sheria za Kanisa CONON LAW na hata maisha ya Kadinali Carl Woytila akiwa Baba Mtakatifu naomba mtanisaidia ukweli wa kisa hiki na kama kuna nyaraka inayosimulia tukio hli naomba mnitumie kisa hiki kama kilivyo na taifa kilipotokea ili niweze kukisimulia barabara, shabaha ni moja tu kutoa somo kuwa UADILIFU ZAIDI YA SHERIA/KATIBA.

makwadeladius@gmail.com

 


 
























0/Post a Comment/Comments