MARUFUKU KILIMO CHA KUBAHATISHA

 

Adeladius Makwega-RS-MARA&

Debora Kitundu–Iringa Univesity College (IUCo).

 

“Sisi Halmashauri ya Rorya tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia vifaa hivyi vya kilimo kwa wakulima wetu, nina hakika vifaa hivi vinakwenda kutuongezea mara dufu uzalishaji wa mazao kadhaa katika kilimo cha umwagiliaji, vitatuongezea wananchi wanaolipa ushuru na kodi kadhaa za serikali, vitaboresha maisha ya mkulima mmoja mmoja na pia zana hizi zinakwenda kuwaonesha wakulima wanaolima kilimo cha kizamani umuhimu wa matumizi ya zana bora za kilimo.

Hii sasa itakuwa RORYA MPYA.”

Haya ni maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Rorya Wakili Msomi Mhe. Abdul Omari Mtaka wakati akipokea vifaa bora vya kilimo vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 400 za Kitanzania kwa halmashauri tatu yaani; Musoma DC, Musoma TC na Rorya ndani ya Mkoa wa Mara Novemba 11, 2025.

Wakati Mkurungezi Mtaka anatoa shukrani zake, hali ya hewa ya Mji wa Musoma ilikuwa ya nyuzi Joto 27 nalo jua liliwaka vizuri sana huku Mkurugenzi Mtaka alikuwa akisogelea kivuli cha Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara.

 

Kwa jua hili lilivyokuwa linawaka kama Mkulima wa Mpunga kutoka Ikangao Ulanga Morogoro angevuna mpunga wake asubuhi ya siku hii na kuuanika juani kwa saa nne hakika majira ya jioni angeweza kuukoboa katika kinu vizuri na jioni ya siku hii familia yake ingekuwa wali.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mara Mwalimu Gerald Musabila Kusaya wakati akigawa vifaa hivyo alisisitiza wakulima wanufahika wote vifaa hivyo wavitumie kwa kusudio lilopangwa, wavitunze na huku akisema bayana kuwa yeye na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi watahakikisha wanafuatilia matumizi ya nyenzo hizi za kilimo bora kwa kila atakayanufahika shabaha ni matumizi sahihi ya zana hizi;

“Milioni 468 ni pesa nyingi, zingeweza kupelekwa katika miradi kadhaa iwe ya afya na hata ya elimu na kadhalika lakini serikali yenu inatambua mchango wa mkulima wa Tanzania na ndiyo maana nyinyi WAKULIMA WA MARA mmepewa kipao mbele cha kupatiwa zana hizi bora ya kilimo naomba mzitumie vizuri.”

Katika zoezi hili Katibu Mkuu wa Wizara Kilimo aliwakilishwa na Afisa Habari Mkuu Bi Nyabanganda Taraba ambapo wakati wa zoezi la kukabidhi zana hizo za kilimo linafanyika Katibu Tawala Mkoa wa Mara Mwalimu Kusaya aliwatania wakulima wa Mkoa wa Mara kwa maneno haya;

“Mnamuona mwakilishi wa Katibu Mkuu, huyu mama ni mchanganyiko kutoka mikoa miwili ya Kanda ya Ziwa, hizi mashine ni nzito lakini ameweza kuzitoa huko Dodoma na zikafika hapa salama salimini na hata hapa anaponikadhi anaweza kuzinyanyua japokuwa ni nzito zina uzito wa KG 50-75 hawa ndiyo wanawake wa Mkoa wa Mara hawa ndiyo kina Mama wa Kanda Ziwa.

Sasa nyinyi ndugu zangu wakulima wa Mkoa wa Mara mnapewa hizi zana za kilimo mkiniangusha mimi tambueni mmemuangusha na ndugu yenu Bi Taraba. Kwa sasa hapa Mkoani Mara hatutaki Kilimo cha Kupiga Ramli.”

Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu Kilimo Bi Taraba alisisitiza kuwa wakulima wajitume maana sasa kama Serikali yao imewaona katika zana bora za kilimo watambue kuwa serikali yao inafuatilia kilimo chao tangua utayarishaji wa mashamba hadi uvunaji wa mazaoana hadi kutafuta soko ya mazao ya;

“Zana hizi zimenunuliwa kutokana pesa ya mlipa kodi wa Kitanzania, wewe unayepata fursa ya kutumia zana  nakuomba itunze , hii ni pesa yako.”

Hadi shughuli hii ya makabidhiano inakamilika jua kali liliendelea kuushambulia vilivyo mji wa Musoma ulio jirani na Ziwa Victoria ambapo ilibidi Mkurugenzi Rorya mpaka zoezi la makabidhiano linakamilika tai aliyoivaa.

 

Mwanakwetu upo?

Kumbuka

“MKOA WA MARA MARUFUKU KILIMO CHA KUBAHATISHA.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 











































































 

 

 

0/Post a Comment/Comments