Adeladius Makwega-MBAGALA
“Kindumbwedumbwe chalia, Kindumbwe dumbwe Chali. Kikojozi Kakojoa na Nguo Kazia Moto Hiiii….Hilooo…
Kindumbedumbe Chalia, Kindumbwedumbwe Chalia. Kikojozi kakojoa na Nguo Kazitia Moto Hiloooo…”
Haya ni maneno ya ngoma maalumu ya mitaani/vijijini nchini Tanzania miaka ya 1960-1990 ambayo ilikuwa ikiimbwa na kuchezwa na watoto na hata watu wazima katika jukumu la kumfedhehesha/kumuadhibu mtoto/binti/kijana kikojozi katika eneo husika, ikiambatana na kupigwa masingi, kung’onga, kumramba kisogo kabora na adhabu nyingine kazaa.Mara nyingi ngoma hii kwa mtaa wa Mbagala Sabasaba ilichezwa kuanzia saa 12.30 hadi saa 3.00 ya asubuhi baada ya kikojozi kuamka akiwa ameshafanya vitu vyake. Mara nyingi kabla ya kuchezwa ngoma hii familia husika yenye kikojozi kwanza huanza na kumkanya kikojozi huyu;
“Acha kukojo ndugu yetu, unatufanya tushindwa kulala kwa amani, mimi nimechoka kuanika mikeka yako, mikeka yangu inaharibika kisa mikojo yako, vitanda vyangu vya chuma hata springi zake zinapata kutu, ndugu yetu unatutia aiabu…baba zima/ binti unakaribia kuwa mwali kumbe KIKOJOZI?”
Hali hii inapoendelea ndipo siku ya siku jamii mtaani/kijiji ikishirikiana na familia anapotoka KIKOJOZI inaibuka tu na kukusanya matandiko/mikeka, shuka, mito na kumfunika KIKOJOZI na kuanzisha ngoma ya KINDUMBWEDUMBWE.
Msomaji wangu Mwanakwetu akiwa pale Mbagala Sabasaba na hata Mbagala Mangaya jijini Dar es Salaam yeye alikuwa bingwa wa kuziongoza nyimbo za kidumbwedumbwe.
Ifahamike wazi kuwa mara nyingi muimbishaji wa KIDUMBWEDUMBWE huwa siyo mwanafamilia anatoka katika koo jirani na mtaa/kijiji hicho au jirani. Manju wa Kidumbedumbe huibukia nyumba kwa KIKOJOZI na kutoa matandiko yake kisha kuanza ngoma ya KIDUMBWEDUMBWE, hapa lazima familia ya KIKOJOZI lazima itoe ushirikiano maana Harufu wa Mkojo, Kuharibu Vitanda na Matandiko Kuoza inakuwa kero.
Jamii lazima iseme mengi;
“Hali hii ikiendelea huyu atakuwa KIKOJOZI hadi kwa mumewe, atakuwa kikojozi hata kwa mkewe…”
Hizi ni simulizi za Mwanakwetu kutoka nyumbani kwao MBAGALA na wewe msomaji wangu nipe simulizi za kwenu.
Kwanini Mwanakwetu ameikumbuka Ngoma ya KINDUMBWENDUMBWE siku ya Leo?
Hivi karibuni katika Ulimwengu wa Kihabari na Siasa tumeona Shirika la Kimataifa ya Habari Kutoka Marekani CNN limerushwa katika runinga yake makala juu ya hali ya Tanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mwanakwetu amefuatuatilia kwa karibu hali hii huku akitambua kuwa Tanzania kwa muda mrefu inafanya kazi kwa karibu na mashirika kadhaa ya habari ya kimataifa ikiwamo VOA, BBC, DW, RFI na mengine mengi ambayo yanarusha matangazo yake hadi kwa KISWAHILI.
Kwa kuyatazama mashiriki haya yanafanya kazi huku yakitakiwa kuheshimu Sheria na Kanun za Habari na Utangazaji za Tanzania kinyume chake kanuni hizo huziangukia taasisi hizo za kimataifa hadi kufungiwa au wakati mwingine kupokwa frekwensi na hata madhara kwa mwanahabari binafsi.
Swali la kujiuliza ilikuwaje kazi hii ya uchunguzi ilifanya na CNN badala ya vyombo hivi vilivyopo jirani na Tanzania muda mrefu vinavyotangazwa kwa KISWAHILI?
Jibu lake ni moja tu Larry Madowo mzaliwa wa Siaya nchini Kenya shirika lake halibanwa sana na kanuni na sheria la Tanzania, hivyo hivyo vyombo vya kimataifa vingine sasa vinaripoti tu kilichotokea kwa kiasi na kile kinachotokea .
Mwanakwetu anaiona nafuu kwa DW KISWAHILI kuliko kwa BBC ambapo awali Larry Madowo aliwahi kufanya nao kazi,huku nyuma ya pazia kwa sasa kumekuwa na tabia ya Serikali kadhaa za Afrika na hata Tanzania kutoa vyeo kwa wale waliowahi kufanya nao kazi na jambo hili linaonesha udhaifu mkubwa kwa BBC kuweza kufanya vizuri kihabari katika mataifa haya tena yenye changamoto tele.
Hapa waweza kurejea nafasi walizopewa akina Al –Ustadha Karenga Ramadhani, Tido Mhando na hata marehemu Hafsa Mosi majina haya na kukiwa na ushahidi. Huku ikiaminika kuwa kwa wanahabari wa BBC, DW, VOA na hata RFI ni rahisi mno kuwafikia lakini ni kazi ngumu kuwafikia CNN ya Larry Mabowo.
Nakuomba msomaji wangu ukumbuke na hili Viongozi wa Afrika wanatakiwa kuwa makini mno kwa sasa kwa kila wanachokifanya dhidi ya raia wao maana Afrika iligawanya kupitia Mkutano ule wa Berlini mwaka 1884-1885 huku makabila kama Maasai,Wamakonde, Jaluo, Wakulya, Waha, Wamanyema, Wakamba, Wadigo na mengine mengi yakiwa katika mataifa yanayopakana na Watanzania.
Hawa ni ndugu kabisa wadamu, hivyo ukiweka kando Larry Madowo kama mwanahabari , yeye pia anaripoti kwa hisia zote maana yeye ni miongoni mwa jamii ya Wajaluo wa Kenya yenye udugu na jamii ya Wajaluo wa Tanzania, isitoshe pia akiwa ni mzungumzaji wa Kiswahili ambapo hali hii ni vigumu kuiona kwa makabila ya katikati ya Tanzania ambayo hayapo mipakani.
Ndiyo kusema Larry Madowo ule UJALUO wake, kuzaliwa kwake Siaya, kuwa Mkenya, kule kuzungumza kwake KISWAHILI kunafanya kuwa jirani na jamii ya Watanzania akiwa sawa na yule anayeiongoza NGOMA ya KINDUMBWENDUMBWE akijua kuimbisha nyimbo hizo vizuri, na kilichomualika katika ngoma hii ni kile kile kinachotokea katika Kijiji./Mtaa wake kwa nduguze wala si kingine.
Mwanakwetu anaamini kuwa Larry Madowo hapaswi kulaumiwa bali wa kujilaumu ni sisi wenyewe kwani magodoro yetu yanaharibiwa, kwanini kitanda chetu cha chuma kinapata kutu? Kwa nini mikeka yenu inaoza? Kwanini Magodoro yetu yanavunda? Huyu aanayefanya uhalifu ndiye wa kupambana naye na siyo vinginevyo.
Mwanakwetu Upo?
Kumbuka.
“Manju wa Kindumbwendumbe Hapaswi Kuguswa.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257










Post a Comment