Adeladius Makwega-MBAGALA
Majira ya Jioni ya Novemba 21, 2025 Mwanakwetu anarudi nyumbani anapoishi hapo Mkoani Mara, akiwa katika yadi ya makazi ya ofisi anayohudumu mara akasikia sauti ya juu inaita ;
“Mwalimu Makwegaaa!, Mwalimu Makwegaaa!, Mr Makwegaaaa!”
Mwanakwetu akiwa amevalia jaketi la njano, suruali ya khaki, begi mgongoni na mkono wa kuume kabeba samaki wawili katika mfuko wa nailoni…muito huo akageuka na kumuuliza nani mwazangu? Aliyeita akamkimbilia kwa furaha mpaka alipo Mwanakwetu na kumsalimu kwa neno SHIKAMOO MWALIMU ! Kisha kijana huyu kusema maneno haya,
“Mimi ni mwanafunzi wako wa Isimani Sekondari…”
Mwanakwetu akamkumbuka mwanafunzi wake huyu ambaye alimfundisha akiwa kidato cha kwanza A mwaka 2005 Isimani Sekondari Iringa Vijijini Tanzania na Mwanakwetu akiwa Mwalimu wa darasa hili.
Mwanakwetu akamuuliza huyu kijana;
“Wewe ni Bakari au wewe Mohammed?”
Kijana huyu akajibu kuwa yeye ni Mohammed Hamza Lalika alisoma Isimani Sekondari mwaka wa 2005-2008. Mwanakwetu akamuuliza Mohammed mbona upo katika yadi ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara?
Mohammed alijibu haya,
“Hivi sasa nafanyakazi na Mahakama ya Tanzania kama Afisa Usafirishaji hapa Mara na ofisi yangu ndiyo lile basi kubwa, nimekuja kulilaza hapa…hapa Mkoa wa Mara mimi ni mgeni maana nimehamia hivi punde kutoka Mkoa wa Geita…”
Mwanakwetu alizungumza mengi na mwanafunzi wake huku akisema;
“Kumbe Hiki Chuma Kinaendeshwa na Mwanafunzi wa Mwanakwetu !”
Hapa akimaanisha lile basi la Mahakama ya Tanzania. Mwanakwetu akamwambia Mohammed Hamza Bini Lalika kuwa;
“Jitahidi ukae vizuri na watumishi wote wa Mahakama ya Tanzania tangu walinzi getini, madereva, wafagiaji, makarani, mawakili, mahakimu na majaji na wao nitawaambia jamani eee mkae vizuri na Mohammed Hamza Bini Lalika maana nia mwanafunzi wangu huyu ni mwanafunzi wa Mwanakwetu.”
Mohammed Lalika akawa anacheka akidhani huo ni utani, kumbe Mwanakwetu alikuwa ana maanisha. kisha kupiga naye picha na kuagana naye.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu aliajiliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka wa 2004 kama Afisa Elimu Msaidizi Daraja la tatu baada ya kuhitumu Chuo cha Ualimu Kasulu Stashahada ya UALIMU mwaka wa 2003. Kwa hiyo mwaka wa 2003, 2004 na hata 2005 ni miaka ya mwanzoni kabisa Mwanakwetu akiwa mwalimu na ndiyo kusema Mohammed Lalika ni miongoni mwa wanafunzi wake wa kwanza kwanza kwanza.
Mwanakwetu akiwa anafundisha Isimani Sekondari anaomba ifahamike hili, hii ilikuwa ni shule kubwa kati ya Mtera na Iringa Mjini na Mohammed Bini Lalika ni miongoni mwa vijana wa Kiisilamu kutoka dhehebu la Ahamadiya ambapo wakati huo ndiyo dhehebu lililokuwa na Misikiti mingi njia ya Dodoma Iringa.
Kwa heshima ya Mahakama ya Tanzania naomba mfahamu hili, Mohammed Bini Lalika ni ile jamii ya vitukuu ya Ndolela, Kisinga, Mkungugu, Chamundindi na Isimani Tarafani ambapo ni hodari mno wa kilimo cha mahindi. Eneo hili lina mchwa sana , tena mno ambapo hata mashamba yao wanaweza kulima bila mbolea maana mchwa wanafanya kazi vizuri na mahindi wakilima wanapata sana.Pia Bini Lalika ni jamii ya Waisilamu kwa ile kesi ya mwaka 1971, 1972, 1973 hadi 1974 ile iliyohusisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Kleluu na Said Abdallah Mwamwindi-Mkulima wa Mahindi alipokwa mashamba yake.
Kwa kuwa Mwanakwetu nimemfundisha Mohammed Lalika akiwa kijana mdogo sana nayakumbuka haya;
“Kijana mpole, mtulivu, hana maneno mengi anapenda kucheza mpira kijana mkarimu , nilikuwa nawape pesa waninulie kuku wa kienyeji na walikuwa wananiletea huku kuku mmoja alikuwa kati ya shilingi 3000-4000 ya Kitanzania maana Mwanakwetu alikuwa Mwalimu Mfugaji”
Mwanakwetu upo? Je Makala haya yaitwaje? Mwalimu Mfugaji? Chuma Kinachoendesha na Mwanafunzi Wangu? Mahakama Tanzania Kaeni Vizuri na Mwanafunzi Wangu? Mwanakwetu anachagua Mahakama Tanzania Kaeni Vizuri na Mwanafunzi Wangu.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
NB Makala haya yameandikwa na Mwanakwetu kwa Heshima ya Mahakama ya Tanzania na watumishi wake akiwamo mwanafunzi wa Mwanakwetu Mohammed Hamza Lalika.







Post a Comment