Lucas Masunzu- TABORA
"Siku hiyo maandishi makubwa yaliyoandikwa kwa nakshi za rangi angavu yaliteka macho yangu. Baadhi yalikuwa kwa Kiingereza, mengine kwa Kiebrania. Nilipoyasoma, yale ya Kiebrania yalinichanganya, lakini maandishi ya Kiingereza yalisomeka: University of Haifa. Hapohapo nilitambua kuwa tayari nilikuwa nimewasili salama salimini katika Chuo Kikuu cha Haifa kilichopo nchini Israeli, barani Asia. Nilijawa na furaha isiyoelezeka huku nikatafakari mwanzo wa maisha mapya nikiwa ughaibuni. Hata hivyo, siku za mwanzo hazikuwa rahisi. Nilianza kujiona mpweke, mbali na nyumbani, mbali na ndugu, mbali na marafiki na mazingira niliyoyazoea. Lakini taratibu nikaanza kuzoea ulimwengu mpya, watu wapya na utaratibu mpya wa maisha. Ni kweli usiombe kuishi mbali na nyumbani lakini pia usiogope, kwa sababu mbali na nyumbani kuna fursa tele".
Hayo ni maneno ya Jesca Elikana, mwanafunzi kutoka shule ya sekondari Urambo –Tabora, aliyepata nafasi adimu ya kusoma Chuo Kikuu cha Haifa nchini Israeli. Nafasi hiyo ilifungua ukurasa mpya katika safari yake ya kielimu na maisha kwa ujumla. Mbali na manufaa ya kielimu akiwa Israeli, Jesca alipata fursa ya kuzuru maeneo maarufu ambayo yamekuwa kitovu cha historia ya dunia kwa miaka. Katika mazungumzo Jesca anasimulia kwa hisia kuhusu mambo aliyofaidi akiwa katika taifa hilo: Jambo nililofaidi zaidi ni pale nilipofika mto Yordani ambao unateremsha maji yake mpaka Galilaya.
Hapo ndipo ubatizo wa Yesu Kristo ulifanyika. Niligusa maji ya mto huo kwa mikono yangu mwenyewe, nilihisi msisimko wa pekee sana. Jambo hili kwangu si la kusahaulika. Jesca anaendelea:
"Nikiwa Israeli nilitembelea mji wa Yerusalemu, mji ambao kwa muda mrefu nilikuwa nikipata simulizi zake kupitia mafundisho ya dini. Safari yangu katika mji huo haikuwa ya bahati kwa sababu sikufaidi sana, msimu huo kulikuwa na maelfu ya watu hapo Yerusalemu ambao walikuja kutalii na mahujaji wengi wakitoka mataifa mbalimbali. Hata hivyo, bado nilijiona ni mwenye bahati mno kuweka unyayo wangu katika ardhi ya Yerusalemu. Kweli tembea uone, nilibahatika pia kutua Goligota mahali ambapo Yesu alisulubiwa. Siku hiyo nilikuwa na rafiki yangu ambaye hakuwa Mtanzania. Nilipofika hapo, simulizi za Goligota zilinihuzunisha moyoni maana kilichosimuliwa hapo ni kumwaga damu, kugongwa misumari, mateso na maumivu aliyoyapitia Yesu huku mnofu wa lawama akirushiwa Pontio Pilato wa jimbo la Yudea. Hapo hapo Goligota, niliponyanyua macho yangu ukutani, niliona picha ya Yesu akiwa ameelemewa na uzito wa msalaba. Moyoni nikasema: Ee Yesu, utuhurumie na utusamehe sisi wakosefu. Siku nikiwa Gologota, kwangu ilikuwa ni siku ya tafakari ya kina kuhusu mateso na upendo wa kweli wa mtu kutoa uhai kwa ajili ya wengine. Kwa hakika nilijifunza mengi kila siku, si tu darasani tu, bali pia kutoka kwa wanafunzi wenzangu waliotoka mataifa mbalimbali. Nilihitimu vizuri masomo yangu. Siku ya mahafali yangu ilikuwa ya kipekee zaidi. Nilipokea zawadi kutoka kwa balozi wa Tanzania nchini Israeli, nilijawa na furaha kubwa. Zawadi hiyo ilikuwa kama sauti ikiniambia: ‘Endelea kupigania ndoto zako, Jesca.”
theheroluke23@gmail.com |
0762 665 595.









Post a Comment