

Adeladius Makwega-MBAGALA
“Sikiliza ndugu yangu, askari mwenye akili timamu hawezi kukataa amri (oda). Kwanza unaipokea hiyo amri kama ilivyo, unapiga salute kisha unakwenda kuitekeleza hiyo amri ukiwa na akili timamu.”
Ndugu huyu anaongea na hapa hapa Mwanakwetu akakumbuka kuwa askari waliowauwa wafanyabiashara wa madini wa Mahenge wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne walikuwa hawatekelezi amri? Jibu walikuwa wanatekeleza amri kutoka kwa wakubwa wao;
“Amri kutoka wa afande Christopher Bageni na pengine wakubwa wengine ZAIDI japokuwa wao walipona katika katika kesi hii, huku Christopher Bageni akifungwa maisha baada ya kutiwa hatiani.
Kijana Pasifiki katika kesi ya mauwaji ya marehemu Daudi Mwangosi alikuwa hatekelezi amri kutoka kwa wakubwa wake?
Afande Pasifiki alikuwa anatekeleza amri kutoka kwa wakubwa wake lakini baadaye kijana huyu peke yake yeye mwenyewe alitiwa hatiani kwa mauwaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi.”
Haya yalikuwa mazungumzo ya wadau juu ya askari makini na utimamu wake akilini wakati anatekeleza amri na yeye Mwanakwetu kuiongeza nyama tafakari hii kisha kuiweka katika Makala haya.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
“Jambo la msingi kwa askari yoyote yule ni umakini wake wakati anapokuwa akitekeleza hiyo amri. Hoja ni moja tu aliyeagiza mara nyingi hayupo wakati ukiwa unatekeleza hiyo amri, inawezekana kufika wakati huyo aliyetoa oda akakana kuwa hakuagiza hicho ulichofanya, ili yeye abaki salama, rejea kesi ya mauwaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge. Jambo la msingi ni kwa kila askari ni kuwa makini unapotelekeleza hiyo amri unayeweza kuingia hatarini ni wewe mwenyewe na siyo mwingine.
Kamati zitaundwa, uchunguzi utafanywa aliyetoa amri mara nyingi ni mtu wa mwisho kukamatwa wakati wewe wa ngazi ya chini utaingia mashakani wakwanza, awali nafsini mwako umeuwa na baada ya hapa kufanya tukio pili baada ya kukamatwa na mwisho baada ya kuingizwa hatiani.”
Kwa hakika Mwanakwetu alihudhulia mafunzo maalumu kwa viongozi wa umma ambayo yalihudhuliwa na viongozi kadhaa na hata kutoka Jeshi la Piolisi Tanzania mapema mwaka wa 2025 yalisemwa haya;
“Kwenye huu uhalali, kwanza zingatia sheria, lakini Katika Utumishi wa UMMA tambua UADILIFU ni zaidi ya kuzingatia sheria. Hapa ndipo wakati mwingine yanatolewa maelekezo. Maelekezo unatakiwa kuyapima kama ni halali au siyo halali, usikurupuke, ukiyapima utabaini ni halali, hapa hapa tekeleleza, usipotekeleza hilo ni kosa na lina adhabu yake ambayo ni kufukuzwa kazi.
Kama maelekezo uliyopewa umebaini siyo halali, utartaaibu utayapima kama siyo halali, yana madhara kwa taifa hili na ndani yake yamejaa hila na maslahi binafsi ya muelekezaji, mkono wako ndiyo unatekeleza mwishoni mtoa maelezo haonekani, sauti yake haitosikia maana yake Mkono Ulio na Damu Ndiyo wa Yule Aliyekula Nyama.
Hakikisha umemshauri kiongozi wako kwa maandish , mara moja na kama ukipata fursa shauri hata zaidi ya mara mbili. Tunza kumbukumbu za ushauri wako, mwishoni kama madhara yake siyo makubwa nenda katekeleze kwa sababu sheria ya insubordination itatumika kukuumiza kama madhara yake makubwa acha kutekeleza usitekeleze kabisa…”
Haya siyo maelezo ya Mwanakwetu bali ya maafisa waandamizi wa Utumishi wa Umma wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Mwanakwetu katika kikao hiki alishiriki kama mwanahabari na kunukuu neon kwa neon.
Kwa hiyo askari wetu wanatakiwa kufahamu kuwa hata Afande PASIFIKI katika Mauwaji ya Daudi Mwangosi na hata Afande Chrisopher Bageni katika mauwaji ya wafanyabiashara wa madini wa Mahenge hali ilikuwa kama ilivyo kwa matukio ya Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania. Dunia tunayoiona leo siyo dunia ya mwaka 1950 kuna maendeleo makubwa ya sana ya tekinolojia. Kwa maendeleo haya tekinolojia yule aliyetoa amri atajitahidi kujiondoa ili yeye awe salama, usalama wa mtu mwenye cheo cha chini ni mdogo kama ulivyo usalama hafifu wa nduguze waliopata shida(wananchi waliuwawa na kuumizwa) siku ya Oktoba 29, 2025 na siku ziliozofuata nchini Tanzania, sasa wewe uliyekuwepo katika tukio utakuwa salama?
“Askari wa Jeshi la Polisi Tanzania ni ndugu zetu, mnatoka katika jamii hii ya Watanzania wanaolia misiba na walipata majeraha wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.”
Mwanakwetu nina hakika zipo koo zenye askari ambao ndugu zao wameuwawa, wapo ndugu zao wamuumia na wapo ndugu zao wanauguza vidonda vya matukio ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
“Tukumbuke wewe umebeba bunduki yenye silaha eneo A ambapo pengine siyo nyumbani kwako lakini ni nyumbani kwa askari mwingine ambapo nayeye amebeba bunduki eneo C nyumbani kwa askari mwingine. Madhara ya risasi uliyofyatua iwe eneo A au C yakitokea yatawakumba askari wote wawili bila ya kujua tukio la eneo A linashabiana na tukio la eneo C na madhara kwa aliyetoa oda.”
Mwanakwetu ninayasema haya kwa moyo mweupe kabisa maana wapo wadogo zangu kadhaa ni askari waJjeshi la Polisi Tanzania, wapo vijana kadhaa nimewalipia karo wakiwa sekondari na sasa wanafanya kazi na Jeshi la Polisi Tanzania.
Mkumbuke kweli mnatekeleza amri lakini kuweni makini maana baada ya kutekeleza sasa tambua na wewe unakuwa miongoni mwa waliopoteza ndugu zao katika matukio haya, ni jambo la kushangaza.
Haya ni ya tafakari ya Mwanakwetu ambapo sasa Jamii inaona UASKARI NI MZIGO wakati watu wengi kabla ya Oktoba 29, 2025 waliona Uaskari ni ZAWADI. Binafsi ninajiuliza wale askari niliowalipia ada wakiwa wanasoma shule ya sekondari naona kama nilifanya kosa ili waje kuwadungua ndugu zao wenyewe?
”KATIKA UTUMISHI WA UMMA UADILIFU NI ZAIDI YA KUZINGATIA SHERIA.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257.



















Post a Comment