Jioni ya Mei 5, 2018 nikiwa mtumishi wa Halmashauri ya Lushoto mkoani Tanga, Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW KISWAHILI lilitayarisha Kipindi cha Mahojiano kilichopewa jina KINAGAUBAGA ambapo kulikuwa na mazungumzo na Kiongozi wa Baraza la Habari la Burundi ambalo liliamua kwa kauli moja kuvifungia vyombo viwili vya habari vya kimataifa yaani Voice of America (VOA) na British Broadcasting Cooperation (BBC) nchini humo, wakati taifa hili la Afrika Mashariki lilikuwa linajiandaa na kura za maoni za mabadiliko ya Katiba yake ili kumpa nafasi zaidi Rais wa Burundi wakati huo marehemu Pierre Nkurunzinza.
Kama kumbukumbu zangu kama zipo vizuri mahojiano haya yalifanywa na Daniel Gakuba ambaye kwa mwaka wa 2025 ndiye Mkuu wa Idhaa ya KISWAHILI ya DW yenye makao yake pale Bonn Ujerumani ambaye ni mwanahabari ninayemfahamu.
Mtangazaji Daniel Gakuba ambaye anaasili ya Rwanda alimuhoji mwanahabari mkongwe Al Ustadh Ramadhani Karenga ambaye alikuwa ni kiongozi aliyeongoza kikao cha kuzifungia BBC na VOA akiwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Habari na Utangazaji nchini Burundi wakitoa waraka wa maamuzi yao kwa vyombo vya habari.
“Kazi tuliyokuwa nayo ilikuwa ni kuangalia vyombo vya habari vilivyosajiliwa vinafanya kazi kama sheria na kanuni zake za Habari na Utangazaji kisha tukaamua kuvifungia VOA, BBC na pamoja gazeri la serikali linaloandikwa kwa lugha ya Kifaransa kwa kuwa wamevunja sheria.
VOA walikuwa wanatumia moja ya mtandao uliyopigwa marufuku wa redio washirika, VOA pia ilimpa kazi mtangazaji ambaye alikuwa anafuatiliwa na mahakama ya Burundi na kandoni akiwa na Waranti ya Kimataifa ya Kukamatwa na Mahakama za Kiharifu nao BBC walikuwa na mtangazaji ambaye aliripoti kwa kupotisha, tukaomba habari zao ziwe na mlingano hapo hapo kulitolewa kashfa, hayo ndiyo makosa ya msingi.”
Katika kisa hiki waliokuwa wakipiga kelele kupinga kufungiwa vyombo hivi wakiwamo wanasiasa wa upinzani nchini Burundi walisema kuwa kuvifungia vyombo hiivyo ilikuwa ni mkakati wa Serikali ya Burundi wa kumtengenezea njia Rais Nkurunzinza ili abaki madarakani hadi 2034 huku VOA na BBC walikuwa wakimuharibia mpango huo kwa kuchochoa kuni zenye moshi katika mkakati huu kabambe. Al-Ustadh Ramadhani Karenga katika mahojiano haya alijinasibu kuwa anajua BBC na VOA wataendelea kurusha matangazo yao nchini Burundi kwa kutumia vyanzo vingine na walichofanya wao ni kuzipoka frekwinsi tu walizowapa kwa muda wa miezi sita ikiisha watarudishiwa haki hii;
“Hiyo watarudishiwa baadaye ili waendelee na kazi, mimi ni mahiri katika taaluma hii ya Habari na Utangazaji kwa miaka zaidi ya 30 kwa kufanya kazi na Redio kadhaa za Kimataifa ikiwa Redio Kairo, Redio Japani DW na hata BBC wenyewe, hapa Burundi ninautumia vizuri uzoefu wangu wote katika kuifanya kazi hii hapa nyumbani.”
Katika makala haya Daniel Gakuba alimuuliza swali nzuri sana Al- Ustadh Ramadhani Karenga ;
“Wewe unasema ni gwiji , mahiri na uzoefu tele katika habari pia unasema unafuata misingi ya habari sasa kwanini hamkuomba haki ya kujibu hoja na badala yake BBC na VOA mmepiga rungu katika taarifa yenu la kuwafungia?”
Majibu ya Al -Ustadh Ramadhani Karenga yalikuwa haya;
“Mimi sina muda wa kufundishwa chochote kwa sasa, mtu kaleta malalamiko, tumewapa muda wakujibu, hawakufanya hivyo ndiyo maana tumeamua hivyo.”
Kwa hakika kilichotokea nchini Burundi wengi wanajua na haukupita miaka miwili yaani Juni 8, 2020 Rais Pierre Nkurunzinza alifariki dunia na kisha taifa hili kupata rais mwingine, huku hoja ile ya 2034 ilikufa kifo cha mende.
Kwa nini Mwanakwetu amekumbuka kisa hiki?
Kwa hakika mwishoni mwa mwaka wa 2025 nchini Tanzania kumekuwa na hoja juu ya makala ya CNN iliyotayarishwa na mwanahabari wa Larry Madowo wa CNNjuu hali ilivyokuwa Okoba 29, 2025 na siku zilizofuata nchini Tanzania.
Kumekuwa na hoja kuwa ati ile kazi nzuri haikufuata mizani ya ulinganifu huku tuhuma tele zikitoka kwa Msemaji wa Serikali ya Tanzania ambaye awali alikuwa mwakilishi wa SHIUTA mkoani Ruvuma.
Mwanakwetu ameitazama filamu hii vizuri sana yenye dakika zisizozidi sita na kwa hakika CNN wamefanya kazi nzuri ikiwa ni makala inayotia chachu ya kutaka walioumizwa , ndugu wa waliofariki waibuke waseme zaidi maana dakika tano ni sehemu ndogo sana kwa yote yaliyotokea wakati wa balaa hili. Pia makala hii fupi ya CNN kwa lugha iliyotumiwa ya Kiingereza inalenga pia kueleza ulimwengu kwa muhtasari kile kilichotokea nchini Tanzania
Serikali ya Tanzania hakupaswa kusema kitu maana kinyume chake ukiitazama vizuri na inavyoonekana CNN wana ushahidi zaidi wa kile kilichotokea wameuweka kibindoni, kwa mtu makini unaweza kuliona hili.
“Angalau tungetayarisha makala ya dakika tano na tungeweka ilani ya kusema kuwa Tanzania ni nchi kubwa, yenye watu karibu milioni 70, watu wenye tabia tafauti tunakubali mengi yametokea lakini sasa tunayafanyia kazi.”
Kwa kuwakumbusha CNN mizani linganifu hii si hoja , hii ina hitilafu ya utetezi wetu maana kazi za habari ziko za aina nyingi.
Ninaomba kushauri hivi;
“Mwanzako ametoa makala fupi ya dakika 5 na ushehe na wewe jibu kwa makala kwa lugha aliyotumia, kama KISWAHILI tumia hicho hicho na kama Kiingereza tumia KIINGEREZA siyo kwa mkutano na vyombo vya habari.
Unapojibu kwa Mkutano wa Vyombo vya habari inaonesha kuwa una mashaka na majibu yako, tulipaswa kujibu kwa makala kuonesha kuwa kama siyo kweli yale yote yaliyosemwa na CNN na ukweli ulikuwa upi?
Kwa sasa na hata baada ya miaka 100 Watanzania watakaokuja kuona makala ya CNN na wakatazama Mkutano wa Vyombo vya Habari ule wa Mwakilishi wa zamani wa SHIUTA mkoani Ruvuma hapo, hapa hapa makala ya VOA bini CNN, hawa ndugu Wamerekani kazi yao itabaki kuwa mshindi.
Makala ya CNN itaendelea kuleta simanzi kwa umma wa watazamaji. Wewe unayejibu utaoneka milele kuwa ni sehemu ya matatizo haya.”
Msomaji wangu kumbuka ndiyo maana katika makala haya awali Mkuu wa Idhaa ya DW KISWAHILI Daniel Gakuba wakati anamuhoji Al –Ustadh Ramadhani Karenga kuhusu VOA na BBC kufungiwa alimuuliza swali hili;
“Wewe unasema ni gwiji, mahiri na una uzoefu tele habari pia unasema unafuata misingi ya habari kwanini hamkuomba haki ya kujibu hoja na badala yake BBC na VOA mmewapiga rungu la kuwafungia na mkitoa taarifa kwa vyombo vya habari?
Al-Ustadh Ramadhani Karenga alijibu kwa hasira.
Mwanakwetu upo? Kumbuka
“Awali Makala Hujibiwa Kwa Makala.”
Nakutakia siku Njema.
0717649257
NB Katika makala ya sauti mwishoni kabisa wakati inapohitimishwa pale ilipotajwa VOA ni CNN haya ni mashirika ndugu kutoka nchini Marekani, huku VOA likifahamika zaidi maana lina mahusiano mazuri na Redio washirika huku pia likirusha matangazo yake kwa KISWAHILI.






















Post a Comment