Lucas Masunzu - TABORA
Ni majira ya asubuhi, saa nne siku ya Ijumaa ya Oktoba 10, 2025. Afisa Elimu Divisheni ya Elimu ya Sekondari –Urambo, Bi Sarah Nalogwa, anashuka kwenye gari na kukanyaga viunga vya Shule ya Sekondari Urambo kwa ziara maalumu ya pongezi huku akipokelewa kwa heshima na bashasha na Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Haji Salumu Simba.
Katika uso wake, Bi Nalogwa alionesha tabasamu laini, ishara ya furaha na kuridhishwa na mafanikio ambayo shule hiyo imeendelea kunyakua mwaka hadi mwaka kwenye matokeo ya mitihani ya taifa ya kidato cha sita. Takwimu zinadokeza kuwa mwaka 2025 shule hiyo ilipata divisheni I- 96, divisheni II -133, na divisheni III-28. Matokeo haya ndiyo kusema yakaibua ziara maalumu ya kiongozi huyo. Katika ziara hiyo, Bi Nalogwa aliambatana na viongozi wengine kutoka ofisi yake, akiwamo Neema Mpembela, Saimon P. Makaranga, Hamis H. Omary na Severine Kapongo. Mara baada ya mapokezi, Bi Nalogwa aliongozana na Mkuu wa shule kwenye ukumbi wa shule, ambako alikutana na makumi ya walimu wa shule hiyo kwa ajili ya kikao kifupi cha pongezi na mazungumzo ya kujenga.
"Niliahidi kufika kwa ajili ya kuwapongeza, nilitingwa na msururu wa majukumu, hata hivyo namshukuru Mungu leo nimetimiza ahadi yangu".
Alisema Bi Narogwa mbele ya walimu waliohudhuria kikao hicho ukumbini. Katika mazungumzo ya wazi, Bi Nalogwa alitumia fursa hiyo kuwataka walimu kuwasilisha taarifa za madai yao mbalimbali, yakiwa ni nauli za likizo, gharama za matibabu, na stahiki za uhamisho ili ziweze kufanyiwa ufuatiliaji na kushughulikiwa kwa wakati.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa tukio la furaha la kukata kwa keki ya pongezi na zawadi kedekede kutolewa kwa walimu- tukio lililozua furaha na hamasa kubwa, na kuwaacha walimu wakiwa na ari mpya ya kazi. Katika kutambua juhudi binafsi, Afisa Elimu Maalumu, Severine Kapongo, alitoa pongezi kwa mwalimu wa somo la Fizikia kwa mchango wake mkubwa umewezesha mwanafunzi wa shule hiyo kuingia kwenye orodha ya wanafunzi kumi bora katika mtihani wa Pre-Necta kidato cha nne ngazi ya wilaya.
Pongezi hizo hazikuwa za mkono mtupu bali ziliambatana na kitita cha pesa alichopewa hadharani mwalimu huyo. Hata hivyo, pamoja na mafanikio ya kitaaluma, Kwa sasa Shule ya Sekondari Urambo inashuhudiwa kuwa na maendeleo makubwa ya miundombinu yakiwamo madarasa na mabweni ya kisasa ambayo yameota kwa kasi shuleni hapo, ikiwa ni miongoni mwa miradi tele inayotekezwa wilayani humo na serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kufuatia ziara hiyo walimu wa shule hiyo walitoa pongezi kwa uongozi wa Divisheni ya Elimu ya Sekondari –Urambo, kwa kutambua juhudi za walimu katika upatikanaji wa matokeo hayo na kuahidi kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na matokeo mazuri mwaka hadi mwaka. Nakutakia siku njema, Karibu Shule ya Sekondari Urambo.
0762665595
Post a Comment