UONGOZI HAUANZII UKUBWANI ATII

 



Lucas Masunzu- TABORA

SIKU ya ijumaa 17 Oktoba 2025, Shule ya Sekondari Urambo iliyopo mkoani Tabora imegeuka kuwa jukwaa la demokrasia hai, wakati wanafunzi wa shule hiyo walipojitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali ya wanafunzi kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026. Kwa amani, nidhamu na ushindani wa kistaarabu, wanafunzi walionesha ukomavu na kiu yao ya kuwa viongozi. Mchakato ulianza kwa hatua ya uchukujia na urejeshaji wa fomu, ambapo wanafunzi walionyesha mwitikio mkubwa.

Makumi ya wanafunzi walijitosa ulingoni kuwania nafasi mbalimbali. Nafasi zilizowaniwa ni Kiranja Mkuu, Kiranja wa Taaluma, Kiranja wa chakula, Kiranja wa Michezo, pamoja na nyadhifa nyingine muhimu katika safu ya uongozi wa serikali ya wanafunzi.Katika siku zilizotangulia uchaguzi, shule iligeuka kuwa jukwaa la hoja na sera, huku wagombea wakitumia fursa hiyo kujinadi kwa wenzao kupitia mijadala ya wazi na hotuba fupi za kunangana kistarabu ambazo kwa muda zilizopamba viunga vya shule hiyo.Katika kilele cha uchaguzi, wanafunzi walijitokeza kwa wingi katika madarasa ya kupigia kura yaliyoandaliwa na kamati ya uchaguzi ya shule, chini ya usimamizi wa mwalimu makini Melzedeki Kwabila kwa kushirikiana na walimu wengine pamoja na viongozi wa shule. Kila mwanafunzi alipata fursa ya kutumia haki yake ya kupiga kura kwa njia ya siri, hali iliyoongeza imani katika mchakato mzima.

 

“Baada ya kura kuhesabiwa kwa uwazi mkubwa huku matokeo yakitangazwa mbele ya umati wa wanafunzi, Omari Salumu, mwanafunzi wa Kidato cha Tatu, alitangazwa mshindi wa nafasi ya Kiranja Mkuu, kwa kishindo kikubwa, akiibuka na asilimia 68.5 ya kura zote zilizopigwa.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Habiba Juma, mwanafunzi wa Kidato cha Tano (HKL), ambaye alionesha ushindani wa kweli licha ya kutofua dafu mbele ya Omari ambaye ushindi wake ulipokelewa kwa shangwe, huku wengi wakimtaja Omari Salumu kuwa ni mwanafunzi mwenye nidhamu ya hali ya juu, na ana uwezo mkubwa wa kushirikiana na wengine.”

Katika hotuba yake ya shukrani, Kiranja Mkuu huyo, alitoa ujumbe mzito kwa wanafunzi wenzake, akiahidi kuwa serikali yake itakuwa ya haki, uwazi na itahudumia wanafunzi wote bila upendeleo. Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Haji Salumu Simba, aliipongeza kamati ya uchaguzi kwa kuandaa na kusimamia mchakato huo kwa mafanikio makubwa. Akizungumza baada ya kutangazwa kwa matokeo, Mwalimu Simba alisema:

"Zoezi lililofanyika ni la kidemokrasia. Tunajifunza darasani na nje ya darasa. Viongozi waliopatikana watakula kiapo, baadaye makabidhiano yatafanyika, na wataanza kutekeleza majukumu yao kama kawaida."

Msomaji wangu siku ya leo ninasema nini?

Ukiyatazama matokeo ya uchaguzi huo utabaini kuwa Omari Bin Salum aliyeshinda Ukaka Mkuu wa Urambo Sekondari ni wa kidato cha tatu, huku aliyeshindwa ni binti mwenye jina la Habiba Binti Juma wa kidato cha tano.

Jambo la pili ukitazama katika hili ipo taswira nzuri ya matokeo haya hasa ushindi wa asilimia 68-69 hii inatoa taswira ya matokeo halali maana yake Kamati ya Uchaguzi ya Urambo Sekondari ilitimiza wajibu wake tangu wagombea kuchukua fomu na hadi kuwachuja wagombea hao na ndiyo maana mkuu wa shule ameipongeza kamati husika.


 

Huu ni uchaguzi wa Serikali ya wanafunzi katika ngazi ya msingi, hapa taasisi zingine za uchaguzi zijifunze katika hili.

Jambo la mwisho katika makala haya ni kuwa uongozi haunzii ukubwani, kiongozi mzuri utaweza kumuona tangu ngazi za msingi, akiwa kiongozi wa wenzake na wenzake wakimuona, wakimuheshimu hata baada ya masomo watamuheshimu kuwa Omari Bin Salumu alikuwa kaka Mkuu tulipokuwa sekondari.

Karibu Shule ya Sekondari Urambo.

theheroluke23@gmail.com

0762665595























 

0/Post a Comment/Comments