UCHAGUZI DONDA NDUGU KWA MTANZANIA

 



Adeladius Makwega-MBAGALA

Katika kulifahamu taifa la Tanzania inahitaji akili na hekima kubwa sana, huku ukiomba Mwenyezi Mungu akusaidie maana uongozi ni wito ili baada ya kufa Mungu aweze kutuweka pahala pema. Watanzania wana hekima sana nia ya hekima hizo hawataki ugomvi na mtu yoyote ili siku zisonge na maisha yao ya duniani yawe salama.

Usijiulize maswali mengi ndugu msomaji wangu, tambua kuwa Mwanakwetu ni mwanachama wa CCM wa muda mrefu sana na pengine wengi ambao ni wanachama wa CCM wa sasa ngazi fulani hawana ukongwe huu wa Mwanakwetu, Mwanakwetu Mkongwe tangu kadi za nyuzinyuzi.

Nakuomba msomaji wangu siku ya leo nikusimulie visa kadhaa vilivyo katika mkululu wa matukio kadhaa ya kweli kama vilivyookotwa na MwAnAkWeTu kutoka kwa wanachama wa CCM katika eneo ambalo Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Oktoba 2025 alikuwa anafanya mikutano ya kampeni na katika visa hivi wanaosimulia ni wanachama wa CCM watatu; mmoja ni Mfanyakazi wa Serikali na wawili ni wafanyabiashara ngazi ya kati. 


 

Msimuliaji anasimua haya;

“Ndugu mmoja mfanyakzi alikuwa na dazeni kadhaa za fulana za kampeni za mgombea urais huku wakigawiwa wadau, wanachama na wakerekwetwa wa CCM hapo pahala. Nyuma ya fulani kukiwa na maneno Chama cha Mapinduzi na kwa mbele ya fulana(kifuani) kukiwa na maneno Kiongozi Imara Taifa–Taifa Imara fulana mpya huku zikinukia upya wanguo hizo za chama tawala nchini Tanzania.”

Mgawaji wa fulana akiwa an jina la Paulo kama lile la Paulo Mtume wa Mataifa, mtu muungwana sana akiwa ni kada wa CCM,nasema mtu muugwana aliyejitosa kura za maoni CCM ubunge huko kwao lakini jina lake likakatwa na Kamati Kuu ya CCM Taifa, leo hii Paulo Mtume wa Mataifa anagawa fulana za mgombea urais wa CCM bila kinyongo.

“Nyuma ya pazia Paul Mtume alipoenda kugombea Kura za Maoni CCM alinyimwa mshahara miezi kadhaa huku kadi yake ya NHIF ikidaiwa karibu lakini tano, akitakiwa kulipa pesa hiyo ili aendelee na huduma kisa kwenda kugombea ubunge kura za maoni CCM, michango yake ilikuwa haiende NHIF wakati katia nia.”

Kumbuka Paul Mtume mtu muungwana, anayeheshimika sana, anagawa fulana,na siku moja nyuma alimfuata muungwana mmoja na kumuuliza.

“Hivi kweli Humphrey Polepele wamemteka? Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM taifa?”

Paul Mtume alijibiwa hivyo ndivyo, hicho kilichotokea katika Tanzania ya mwaka wa 2025. Paulo Mtume aligeuza kwa unyonge na kwenda zake.

 




Kumbuka fulana za CCM zinagawiwa,

“Mimi naomba fulana mbili na nyingine ya shemeji yako.”

Paul anatoa fulana hizo kisha mwingine anaingia akisema maneno haya;

“Mie naomba mbili ; yangu mie na Baba Mchungaji, mnataka nigombane na muwe wangu? Kwani wachungaji hawana vyama? Nataka nitoke nae pamoja twende tukampokea Mgombea Urais wa CCM mwaka wa 2025.”

Jamaa wanachukua fulana vizuri ambao kazi hii inafanyika kwa siku mbili kugonja kwenda kumpokea mgombea urais wa chama hiki cha siasa mwaka wa 2025 nchini Tanzania.

“Wafanyakazi wanachukua fulana hizo kwa heshima ya Paulo Mtume, huku wakisema fulana tunachukua lakini kwenda katika mkutano au kutokwenda akili kichwani mwetu, jamaa wasiseme fulana hajachukua, hawa siyo wenzetu.”

Kumbuka msomaji wangu Mwanakwetu anakusimulia visa hivi;

“Kompyuta zangu mbili zilikuwa mbovu, nikatoka zangu pale hadi kwa fundi, mtaani huku nyimbo za CCM zikipamba mji huu. Nilipofika kwa fundi wa Kompyuta nikamkuta na jamaa mmoja. Nikaeleza shida ya kifaa changu, kisha akaanza kutengeneza. Nikiwa pale akaja mzee mmoja mrefu sana na yeye kifaa chake kimoja kilikuwa kibovu lakini alikileta hapa mapema. Mzee huyu akauliza vipi kimpona? Fundi akajibu hakijapona, Mzee huyu akaomba kukabidhiwa kifaa chake na kweli ilikuwa hivyo.

Pale kando yupo jamaa mwingine akamuuliza, mzee huyu vipi ulipata kazi ya muziki katika ugeni huu wa mgombea wetu? Mzee mrefu akajibu kwa maneno ya kukata tamaa, ‘Yaani Hata Hamu Nao Ninayo, Sina Hamu Nao.’ Aliyeuliza akasema nilidhani wewe wamekupa kazi kumbe kama mimi tu ! Pole mzee wangu. Kisha huyu mzee mrefu akaondoka zake.”

Kumbuka msomaji wangu kuwa msimuliaji yupo kwa fundi na sasa amebaki fundi, msimuliaji wa Mwanakwetu na yule aliyekuwa anamuuliza maswali yule mzee aliyeondoka. Msimuliaji akasema tukiwa pale yule jamaa aliyemuuliza maswali yule mzee akasema maneno haya,

“Mwaka huu nimetoa milioni 38 kuboresha vifaa vyangu za muziki ili niweze kupata pesa wakati wa kampeni na nilijua pesa zangu zingerudi, mpaka sasa sielewi kinachoendelea kabisa. Hapa mgombea Ubunge wa CCM nilifanya nae mazungumzo, wakati tunafanya makubaliano ya kazi akawapigia jamaa zake wakamwambia usikodi huo muziki tutakununulia vifaa vyako na kweli wamefanya hivyo wamemnunulia vifaa vya muziki wa milioni 28 na mimi nimekosa kazi hii.

Kama uchaguzi huu akina Tundu Lissu na CHADEMA yao wangeshiriki fedha zangu zingerudi, baba nina muziku mkubwa spika za bezi zipo 40. Bali CCM yenyewe imeharibu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 nilifanya biashara vizuri sana tangu kwa madiwani, wabunge na hata Wagombea Urais wa CHADEMA na CCM, mimi nipo CCM lakini siwezi kuikataa pesa ya CHADEMA na CCM Taifa ilipaswa kulijua hilo katika siasa tunahitajiana.

Angalia hata hapa Halmashauri kama madiwani wote ni 60 CCM wakiwa 35 na CHADEMA 25 hii inatosha, inapunguza malalamiko na kupunguza uchungu wa maisha pande zote, haiwezekani CCM wawe na madiwani wote 60.

Hapa ndipo CCM inatunyima fursa wanachama wake , sasa nani anaweza kukubali kitu kama hiki? Hapa ndipo malalamiko yanakuja, kazi hizi za wagombea wawe wa Ubunge na hata wagombea Urais ni vizuri fursa hizo wapate maeneo wagombea wanapofika, sasa hivi kampeni zinaacha vidonda…

Hata kama majukwaa yetu, miziki yetu siyo ya kisasa, CCM ifanye kampeni katika mazingira anayoyakutana na siyo mambo ya Dar es Salaam kuletwa huku, viongozi hawa si sehemu ya jamii ya Watanzania?

Pesa tunazopata sisi katika biashara hazina nembo ya CCM wala CHADEMA, chama hiki kiache Watanzania waachwe waishi maisha yao waliyoyazoea.

Angalia sasa suala la Humphrey Polepole limepamba moto, mama yake analalamika, nduguze wanalia, CHADEMA wanalia na hata CCM wanalia, jamani haya mambo ni mabaya…

Kwa Mgombea Urais wa CCM hata kama angekuwa anashindana na Tundu Lissu CCM ingeshinda kwa asilimia hata 50.00009 kuna shida gani? ushindi ni ushindi tu, mathalani CHADEMA iwe na wambunge 170 na CCM iwe wabunge 200 kuna ubaya gani? 

Kikubwa tugawane kilichomo ili kuondoa maneno.”

Kumbuka Mwanakwetu anasimulia haya mambo baada ya kusimuliwa, huyu msimuliaji akasema kompyuta yake ilipona vizuri na yeye kisha kuondoka zake.

 


Mwanakwetu anasema nini siku leo?

Kwa hakika simulizi hii ya ndugu huyu imemgusa sana na Mwanakwetu ameamua kuiweka katika makala yake kama kipo cha kujifunza basi wale wanaopaswa kujifunza wafanye hivyo.

Tazama wanachama hawa watatu wa CCM; yule mfanyakazi anavyopitia kipindi kigumu kisa kutoa nia ubunge kupitia CCM hadi kakosa mshahara na kadi yake ya NHIF haifanyi kazi, kwanini Serikali ya CCM inawawekea mazingira magumu wafanyakazi serikalini wanpofanya siasa ? 

Je CCM inataka wafanya siasa wawe wafanyabiashara tu? 

Kumbuka hata changamoto za fursa za wafanyabiasha hawa wa muziki na maturubai waliyokosa kazi ya vifaa vyao hivyo na kilio chao juu. Kama ni kidogo tunapaswa kugawana sote na kazi hizo asipewe mtu mmoja kutoka mijini tu kisha kitu kiwe na ubora Rais wa  CCM mtu wa jamii yote wenye vitu na vitu visivyo bora, yeye ni mali ya jamii nzima, vinginevy tunaigawa jamii ya Watanzania katika uchaguzi huu, uchaguzi unakuwa  donda na tena donda ndugu.


 

Mwanakwetu upo? 

Kumbuka;

“UCHAGUZI DONDA NDUGU KWA WATANZANIA.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257






 

0/Post a Comment/Comments