TUNAZAA MBUMBUMBU MZUNGU WA RELI

 


 Adeladius Makwega-MBAGALA

Suala la usafiri Jijini Dar es Salaam lina historia ndefu sana ambayo mara nyingi haijaandikwa wala kusimuliwa na yoyote yule na siku ya leo Mwanakwetu anaiweka simulizi hii katika makala haya. Mara nyingi wakazi wa asili wa Mzizima yaani Dar es Salaam ya leo wenye uwezo kidogo walikuwa na makazi yao mjini au wengine kupanga nyumba za mjini lakini wengine wengi kubakia mashambani katika ardhi za koo zao. Wale wa kutoka mashambani hudamkia mjini katika kazi ndogo ndogo ziwe za ofisini, upagazi, ufukweni au katika majumba ya matajiri.

“Unajua watu wa asili wa huu mji walikuwa wanakaa mashambani huku wakifanya shughuli zao za kilimo, mjini waende kufanya nini? Mjini kulikuwa makazi ya wageni kutoka maeneo mengine na mataifa mengine JIRANI KAMA VILE KONGO, MALAWI, ZAMBIA nk ambapo wengi wao walikuwa na ujuzi kama vile uselemala uliosababisha kufika na kuishi katikati ya Mzizima.

Haya alisema Fidelis Makwega Kazimbaya (1927-2004) mkazi wa Mbagala Sabasaba Mbuyuni (House Number 7). 

 

Mzee huyu aliongeza na haya;

“Haya maendeleo ya Mzungu, Kusoma na Ajira ndipo yakafanya safari za kila siku kwenda mjini kupamba moto na Mzizima kupanuka, hivyo usafiri wa kila asubuhi kwenda mjini na kurudi haukuwa na budi.”

Haya ni ya wale wenye Mzizima yao na waliokuwepo na wewe ambaye haukuwepo wapaswa kukaa kimya tu.

“Mimi nilikuwa nasoma Pugu Sekondari na wakati wa likizo nilikuwa natoka Pugu nakuja Mbagala pale nyumbani nikiwa na watoto wa Mzee Kazingoma, wakati huu wa likizo mimi na wezangu tulikuwa tunafanya biashara ya VIUNGO (makuti ya kuezekea nyumba) ambayo tayari yamesukwa vizuri.

Likizo tunayakusanya makuti mengi yanaanikwa vizuri na kuyasuka kwa kuyafuma vizuri tukiyawekea na miti yake vizuri tunafunga na kamba na kuwa KIUNGO cha kuuzekea nyumba za makuti maana wakati huo makuti ndiyo bati la TANZANIA, tunafungasha mizigo kadhaa kisha asubuhi moja kabla ya Shule kufunguliwa tunaibeba mizigo yetu ya VIUNGO kila mmoja na wake kwenda nayo POSTA YA ZAMANI KUUZA.

Tunatoka hapa Mbagala Sabasaba kwa mguu, tunapita Mto Mtongani kwa mguu tunafika Mtoni Aziz Ali kwa mguu, tunaenda nayo hado Posta kando ya FORODHANI, muda mwingine Mungu BAHATI wateja walikuwa wanapatikana njiani iwe MIVINJENI lakini aliyeuza hata kama alipata pesa yake Mivinjeni aliambatana nasi hadi POSTA na hili lilikuwa msaada maana ndugu huyu alikuwa anatusaidia kutupokea mizigo yetu ya VIUNGO vyetu hadi POSTA. Kwa hiyo njiani kama mpo kumi wameuza watatu hapo nyie saba mnapata nafuu ya kupokezana mizigo yenu hadi POSTA kutokea nyumbani kwetu MBAGALA, tukifika Posta kuuza jioni tunarudi na pesa zetu tukiwa tumenunua vitu kadhaa vya shuleni.

Sasa wakati wa kurudi tuna pesa ulikuwa unaweza kupanda basi kutoka Posta hadi Mtoni Azizi Ali ambapo basi hilo lilikuwa linakwenda Temeke, tunashuka Azizi Ali na kisha kuanza safari ya Mguu hadi Mbagala Sabasaba nyumbani .

Mabasi ya safari za Mjini Mzizima yalikuwa hayafiki Mbagala. Isipokuwa mabasi yale yaliyokuwa yanafanya safari ndefu kutoka Katikati ya Mji kwenda Kusini mwa Tanzania.

Kweli baada ya kuuza VIUNGO (Makuti ya Kuezekea) siku iliyofuata nilifunga safari kwenda Shuleni Pugu.”

Haya ni maelezo ya Mwalimu Francis Fidelis Makwega Kazimbaya(1950) Baba wa Mwanakwetu.

“Baadaye kulikuwa na mabasi ya safari fupi fupi, kisha kuja mabasi ya Usafiri Dar es Salaam (UDA) zikaja Daladala hizi za leo zinazotumiwa, nakumbuka mwanzoni zilikuwa moja moja.”

Maisha ya yanaendelea nayo mwaka 1987 Adeladius Makwega(1974) akisoma darasa la tano D Shule ya Msingi Mnazi Mmoja na mdogo wake Modestus Makwega(1977) akiwa darasa la tatu, walidamka usiku mmoja wakijiandaa ili wawahi mabasi na wawahi shuleni, hapa wanatokea Mbagala Sabasaba huku wakisoma katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Msafiri alikuwa na wajibu wa kupanda Basi Mbagala hadi Temeke, kisha Temeke hadi Kariakoo na akibahatisha hadi Mnazi Mmoja yaani basi lilikuwa linasafanya kazi yake ndani ya wilaya husika Temeke lingine Temeke Ilala na lingine Ilala hadi Kinondoni. Kama basi lilikuwa safari hizo ndefu basi ilikuwa ni kwa wizi au kwa ujanja ujanja au mabasi ya UDA tu.

“Nilimuamsha mdogo wangu aitwaye jina la Ukoo MAKWEGA (MODE), MAKWEGA, MAKWEGA amka ujiandae, tuwahi shuleni.”

Tulijiandaa vizuri, wakati tunaomba nauli ya basi ambayo ilikuwa shilingi moja kwa mwanafunzi kutoka Mbagala hadi Temeke na shilingi tena kutoka Temeke hadi Mnazi Mmoja, mama yetu mzazi mwalimu Doroth Mlemeta (1956-2002) akasema

“Nyie wanangu, bado muda, hivi sasa ni saa nane kamili usiku, mtakabwa, msiwe mnaamka mapema namna hiii, hilo ni hatari.”

Tukarudi kulala na viatu na nguo zetu za shule na saa kumi kamili akatuamsha na kwenda kupanda basi .Tulipofika stendi ya Mbagala Sabasaba basi la Bandari Tanzania (THA) saa kumi na moja kamili likafika na likawa linabeba abiria wengi na sie kuingia huku likiwa basi refu sana na wakisema maneno haya,

“Moja kwa moja Kariakoo, hatupitia Temeke na hatushushi njiani kituo cha kwanza Mivinjeni…”

Kweli tulipanda basi hili la umma tukalipa nauli  dereva huyu wa basi la umma alifanya kazi hii na kujiingizia kipato na safari ilikuwa nzuri na ya haraka, watu wengi walishuka vituo vinne Mivinjeni, Bandari, Chai na Girls School na kisha sie kuwahi shuleni mapema na saa 11 na dakika 39 tulikuwa Shule ya Msingi Mnazi Mmoja , kweli wanafunzi wa mbali tulikuwa wakwanza kufika shuleni siku hii.


 

Mwanakwetu akiwa mwanafunzi wa Tambaza pia anakumbuka usafiri ulikuwa mgumu sana si watu wazima tu bali hata kwa wanafunzi, huku kugombana, kupigana na makondakta lilikuwa jambo la kawaida mno. Hali ya usafiri ikiwa tete, vizazi na vizazi katika jiji hili ambalo wakazi wake wakiongezeka  kila siku ,Miji ikijengwa kila isku lakini hutatuzi wa changamoto ya usafiri katika maandishi ikiwa na kurasa nyingi, maneno mengi lakini katika uhalisia hakuna matokeo chanya, hakuna kitu, nayo matusi, lawama, kubenua midomo ,misonyo kutoka kwa abiria kwenda kwa viongozi wao imekuwa jambo lililozoeleka mno, jambo la kawaida miaka nenda miaka rudi.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Hii ni historia ya usafiri Dar es Salaam kwa karibu vizazi vitatu tu kwa wakazi wa Jiji hili kutoka kwa Baba Fidelis, mtoto wake Francis na wajukuu ambao ni Adeladius na Modestus ambao wenyewe sasa wana watoto na wana wajukuu, huku shida ya usafiri ni ile na tena afadhali ya zamani ambapo watu wa Dar es Salaam walikuwa wachache.

“Mzizima Amefanya Kosa Gani?Mzizima kwa wingi wote ule wa watu? Kweli akinamama wa Mzizima wanazaa watoto Mbumbumbu Mzungu Wa Reli, Wajinga? Wanaoshindwa kutatua changamoto ya usafiri Mzizima?

Ingekuwa Mzizima ipo mbali na Bahari Hindi tungesema akina mama wa Mzizima kila wanapokwenda kiliniki wapewe sana mafuta ya samaki ili baadae watoto wao wanaowazaa wawe na akili nyingi ili baadae waje kutatua shida hii lakini lakini lakini hata kwetu Mbagala tupo Jjirani na Bahari ya Hindi pale Mtoni Kijichi, pale Kota za Benki tunakula sana samaki kama vile UFUDU, UDUVI na wengine wengi  wenye madini haya kwa wingi.

Je shida ni nini? Heri hali ya usafiri wa Mzizima wa zamani wa akina Francis Makwega wa kutembea kwa miguu na kwenda kuuza makuti (VIUNGO) Posta kuliko ya sasa?”

Hali bado ni tete na hili halikubaliki kabisa.

Mwanakwetu upo?Je makala haya yaitwaje? Mzizima Wapewe Mafuta ya Samaki au Wanazaa Mbumbumbu Mzungu Reli!? Mwanakwetu vichwa vyote viwili amevipenda Swali linalobaki je Tunazaa Mbumbumbu Mzungu wa Reli?


 

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257
















 

 




 

 

0/Post a Comment/Comments