TUNATAKA KWENDA KUTAMBUA MIILI USAFIRI HAKUNA

 

 

Adeladius Makwega

Oktoba 31, 2025 ilitimia huku hali ya mtandao ulikuwa haupatikani, nyuma ya pazia ya giza hili totoro la taarifa Mwanakwetu aliyapata mengi juu ya hali ilivyo katika maeneo mbalimbali .

“Kituo kimoja cha kupiga kura walijitokeza wananchi wengi kupiga kura, shida ikawa, jamaa hawataki kuchukua karatasi za kupiga kura za Mbunge wala za Rais, jamaa wanaosimamia uchaguzi wakawa wamechanganyikiwa lakini hali ilikuwa hiyo. Wapiga kura wanasema sisi tunampiga kura diwani tu, ‘Msimamizi wa uchaguzi hauna mamlaka ya kunilazimisha kupiga kura tatu , mimi napiga kura moja tu ya DIWANI.’

Katika kituo hiki wapiga kura walikuwa na mahaba na Mgombea UDIWANI WA ACT WAZALENDO.

Kazi ilikuwa Kubwa, Wapiga kura wanasema, ‘Sisi hatuoni maana ya kumpigia kura Mbunge wala Rais.’ Kilichotokea baada ya kutangazwa matokeo ni vurugu kubwa mpaka muda huu wananchi wapo majumbani mwao hakuna kutoka nje…”

Mwanakwetu pia siku hii ya Oktoba 31, 2025 liliibuka na jambo hili;

“Mimi nipo Mbeya, usafiri hamna, wapo watu ndugu zao hawafahamu walipo sasa wanataka kwenda META na RUFAA Kutambua miili, tumeambiwa miili ipo mingi huko. Je babab! tutafikaje huko kutambua miili bila ya usafiri? Magari hayapiti na bodaboda za kuvizia...”

Safari ya Mwanakwetu kwa siku hii aliyapata na haya;

“Nimeiona miili kadhaa iliyookotwa na kupelekwa vyumba vya kuhifadhi maiti, jambo la kushangaza ni moja tu hali ya namna maiti hizi zinavyofikishwa mara nyingi hawatakia watumishi wengine tuone, kwa nini wanakataa watumishi wengine tusionee?”

Haya ni machache tu msomaji wangu ya Oktoba 31, 2025 ambayo Mwanakwetu ameyapokea tangu ile saa 0001  usiku hadi saa 1400 ya mchana kwa saa za Afrika ya Mashariki.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika matumaini makubwa ya Watanzania yapo kwa Jeshi la Wananchi la Tanzania JWTZ. Watanzania wamebeba sahani yenye moyo ya Matumaini kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania lilooundwa mara baada ya kuvunjwa KING AFRICAN RIFLE jeshi la Mwingereza.

Mwanakwetu katika hili anashauri hata vikosi vya JWTZ vilinde hadi Hospitali zetu ambazo zinapokea miili ya waliyofariki katika kadhia hii maana kumekuwa na mashaka katika hali hii katika baadhi ya maeneo.

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka,

“Tunataka Kwenda Kutambua Miili Lakini Usafiri Hakuna.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 











 

 

 

0/Post a Comment/Comments