

Adeladius Makwega
“Salaam! Kutokana na Tangazo lililotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi kupitia vyombo vya habari kuhusu Watumishi wa Umma kufanya kazi nyumbani siku ya kesho, nashauri kila mmoja awajulishe watumishi walio chini yake kuzingatia tangazo hili na kuchukua tahadhari wakati wote, niwatakie kila la kheri.”
Oktoba 30, 2025 ilifika, huku Mwanakwetu akiwa amepokea ujumbe huu; Tangazo hili lilitoa ishara kuwa hali ni tete.Huku Mwanakwetu akiwasiliana na ndugu zake kadhaa maeneo mbalimbali ya Tanzania.
“Hapa pana vurugu za hapa na pale, ninawaonea huruma sana Jeshi la Polisi, vijana hawa waliingia jeshi hili kutafuta ajira tu sema sasa hali siyo nzuri.
Hii hali inashangaza maana vijana wanaonekana kuongoza hali hii ni wadogo sana na utaona kama hawana kiongozi na vigumu kujua nani yu nyuma yao.
Utakutana na vijana mbele, kisha mita mia vijana wengine watatu, huku wakiongezeka kidogo kidogo mwisho kundi linakuwa kubwa vijana kama 200 vurugu zinatokea. Unajua zamani maandamano kupambana nayo yalikuwa mepesi sana unajua aliyeitisha ni Lipumba mnaweza kukaa naye meza moja, mnazungumza naye , sasa leo hii hawa vijana unazungumza na nani?”
Mwanakwetu akaongea na mdau mwingine;
“Tanzania kweli media hamna kabisa yaaani hapa natazama … eti wanaonesha ufugaji wa nyuki, ngoma za asili… jamani muda huu ni wakati wa kuwachukua wachambuzi wa hali tuliyo nayo, kisha wafanye uchambuzi ili jamii ijue tunaelekea wapi? Yaani watu hawajajitokeza kupiga kura vyombo vya habari vinasema watu wengi wamejitokeza, Jamani Tanzania hakuna media…”
Mwanakwetu anaongea na nduguze juu ya hali ilivyo maeneo mbalimbali ya Tanzania.
Katika makala haya awali nimegusia suala la maandamano yenyewe namna yalivyo na utata wake pia nimezungunzia juu lawama ambazo vyombo vya habari vya Tanzania inavibeba. Jambo la mwisho ambalo nadhani lina umuhimu mkubwa kama yalivyo haya mambo mawili juu ni hali ilivyo katika hospitali zetu wakati hali hii inavyondelea na kikubwa watumishi afya namna wanavyofanya kazi.
“Hapa Kwetu alifika Mkurugenzi wetu Dkt. Delila Kimambo ameagizi mambo kadhaa ikiwamo tuletewe chakula na kweli hili linafanyika. Dkt. Kimambo ametutia moyo sana akasema tusirudi nyuma tuchape kazi.
Kwa hakika hali siyo nzuri maana watumishi wengi tuliopo kazini tuliingia asubuhi ya Oktoba 29, 2025 mpaka sasa hatujarudi nyumbani. Shinda wafanyakzai waliopo majumbani hawawezi kutoka makwao kuja kazini.”
Ndugu huyu alisema kuwa hospitali yao huwa ina zamu tatu kwa sik ; saa 0730 hadi 1400, 1400-1800 nakisha 1800 hadi 0730 katika zamu hizo tatu zamu moja iliondolewa kwa sababu ya idadi ya watumishi na hizo zamu zipo mbili tu 0730 hadi 1800 na 1800 hadi 0730 kila siku inayokwenda kwa Mungu na zamu hiyo kuwafanyisha kazi watumishi zamu tatu kwa mbili wanalipwa posho kiasi kidogo . Kwa uchunguzi wa Mwanakwetu mpaka jioni ya Oktoba 30, 2025 hakuna dalili za watumishi hawa kurudi nyumbani kwao inaaminiwa labda wataweza kurudi nyumbani Jumatatu ya juma lijalo. Hali hii inaweza kuwa sampuli ya hospitali zote za umma nchini wakato hili fukuto linaendelea. Jambo la kusikitisha watumishi wanawake hawakubeba nguo za ziada na vifaa vya kujisitiri hasa akinamama wakiwa katika siku zao ikiwamo SODO.
“…maduka nje yamefungwa hapa tunatumia GAUZE na bandaji zile laini…”
Msomaji wangu haya yanaelezewa si kuwadhalilishwa mama zetu bali kuelezea hali ilivyo. Kwa kifupi msomaji wangu haya yote ni Oktoba 30, 2025 tanhu saa 0000 usiku hadi saa 2100 ya usiku ambapo makala haya yalikamilika kutayarishwa na Mwanakwetu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mwanakwetu kwa heshima zote anawapongeza sana wahudumu wa afya hosiptali zote nchini kwa kazi nzuri wanayofanya katika fukuto hili, huku viongozi wa hospitali zetu nawaomba watimize wajibu wao kama alivyoonekana Dkt. Delila Kimambo Mkurugenzi wa Muhimbili. Kwa vyombo vyetu vya habari vya Tanzania lazima tujitafakari kwa kina katika haya tunayolaumiwa, vyombo hivi viwe binafsi au vya umma katika hali kama hii tunawajibu kwa kuitendea haki jamii ya Watanzania tutake tusitake maana sisi wenyewe ndiyo tuliamua kusomea uanahabari.
Mwanakwetu upo? Kumbuka;
“Kweli Media Tanzania Hamna Kabisa.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257












Post a Comment