Adeladius Makwega-MBAGALA.
Mwanakwetu alikuwa pahala fulani gafla kukawa na majadala mzuri dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan na Oktoba 29 ya mwaka 2025. Mdau mmoja akasema,
“Unajua utawala wa Rais Samia ninautazama vizuri na nashanga mambo mengi sana, mojawapo ni malalamiko kwa utawala wake lakini na hali ilivyokuwa wakati wa Ali Hassan Mwinyi na hata wakati wa serikali ya awamu ya nne kukiwa na hali tofauti kabisa, mbona hali ya sasa inashangaza? Au shida ya Rais Samia ni kwa kuwa Hakuna Imamu Mke?”
Mjadala huu ulidakwa na mtu mwingine akisema shida siyo JINSIA yake shida ni namna ufanyaji wa kazi tu.
“Unajua UIMAMU sio nafasi rasmi iliyowekwa kikanuni katika Uislamu bali ni jukumu la kidini na kijamii. Hata mtoto anaweza kuwa Imam wa watoto wenzake ikiwa atawaongoza kusali. Hata hivyo, jinsia ina mchango katika kuamua nani anaweza kuongoza nani.
Wanaume wanaweza kuwaongoza wanaume na wanawake katika sala, ilhali wanawake huongoza wanawake wenzao pekee. Hivyo basi, Imam Kiongozi ni nani hutegemea muundo wa waumini wanaosali nyuma yake.”
Mjadala ulikuwa mzuri sana.
“Hili ni suala la kiutendaji na heshima ni mambo ya kufahamu sana: Sala ya Kiislamu inahusisha kuinama na kusujudu mara kwa mara. Hali hii inaweza kuwa nyeti kwa pande zote mbili wanaume na wanawake na hawatakuwa huru kufanya hivyo mbele ya kila mmoja, hasa ikizingatiwa Uislamu unasisitiza kuzuia mitazamo isiyo ya lazima kwa jinsia tofauti ili kulinda maadili na kudhibiti matamanio. Kwa sababu hii, misikiti hujitahidi kutenganisha sehemu za kusalia, lakini pale ambapo hilo haliwezekani, wanawake husali nyuma ya wanaume. Kusali nyuma ya wanaume si dalili ya kudharauliwa, kwani waumini wote ni sawa mbele ya Mungu.”
Jamaa huyu aliongeza na hili;
“Sababu ya wanawake kusali nyuma ya wanaume inapowezekana, inaonekana kuwa ni kulinda heshima na staha ya mwanamke zaidi katika hali hiyo. Pia huenda ni kwa kutambua kwamba mwanaume anaweza kuvurugika zaidi akiona mwanamke akisali mbele yake kuliko kinyume chake. Hakuna ushahidi wa kisayansi wa moja kwa moja kuhusu hili, lakini ukweli kwamba jamii nyingi zinahusisha zaidi sura ya mwanamke.”
Kuongoza sala si cheo cha juu wala heshima ya kipekee katika Uislamu. Hakumpi mtu mamlaka ya kidini juu ya wengine. Ni jukumu rahisi la kuongoza ibada ya pamoja, na kila sala kama hiyo ni sawa haijalishi nani aliyeongoza.
Wengine wanaweza kusema ohhh kwamba ikiwa wanaume na wanawake wametenganishwa katika maeneo tofauti, basi mwanamke anaweza kuongoza wote. Wapo wanaoamini kuwa kuwaruhusu wanaume kuongoza mikusanyiko mchanganyiko kunahakikisha uthabiti katika hali zote, bila hitaji la kufanya udugu au ubaguzi maalum na bila kumpunguzia yeyote hadhi au thawabu.
“Uislamu unawaruhusu wanaume pekee kuongoza sala zenye mchanganyiko wa jinsia. Kwa hiyo, kuwa na Imamu mwanamke(Imamu Mke) kungekuwa hakumaanishi sana, kwani kwa kawaida hangekuwa akiendesha sala hizo. Zaidi ya hayo, Uislamu unawaondolea wanawake wajibu wa kusali wanapokuwa katika hedhi jambo ambalo ni afuu na si kizuizi. Uislamu unatambua kuwa wanawake wengi hupata maumivu makali katika kipindi hicho, na baadhi hawawezi hata kuelekeza akili katika sala, sembuse kuongoza ibada?”
Haya maelezo mengine Mwanakwetu aliyapata kutoka maandishi ya Msikiti Mkuu wa Sheikh Zayed, Abu Dhabi katika mada yao juu ya Uongozi wa Kiroho na Uanawake. Sababu nyingine ni kwamba Uislamu unahimiza familia yenye mgawanyo wa majukumu. Nafasi ya umama imetukuzwa mno katika Uislamu. Jamaa hawa walisema na haya;
Mtume Muhammad alisema maneno haya;
“Pepo ipo chini ya nyayo za mama.”
Kauli hii inaonyesha si tu kwamba watoto wanapaswa kuwatumikia mama zao, bali pia jamii yenye ucha Mungu inajengwa kupitia malezi ya karibu na makini ya mama kwa watoto wake. Hii haimaanishi kwamba wanaume hawapaswi kushiriki katika malezi, au kwamba wanawake wanapaswa kukaa nyumbani maisha yao yote. Bali, familia yoyote ina majukumu mawili makuu: Kupata kipato cha kuihudumia familia, na kuwalea watoto ipasavyo. Msikiti Mkuu wa Sheikh Zayed maandishi yao yanadokeza kuwa katika miaka ya awali ya maisha ya mtoto mchanga, mama ana jukumu lisiloweza kubadilishwa.
Mwanamke pekee ndiye anayeweza kunyonyesha, jambo ambalo lina faida nyingi kiafya na linahimizwa na mashirika kama WHO na NHS.
“Kwa uhusiano huu wa karibu wa kimwili, mama huwa kiambatanisho cha msingi cha mtoto wake. Baba ana wajibu mkubwa pia, lakini hawezi kunyonyesha, na kiambatanisho kikuu cha kihisia huwa kimoja tu. Wakati mama anashughulika na jukumu hili, mtu mwingine lazima bado atafute riziki na kwa kawaida ni baba. Kwa hivyo, jamii inaelewa mgawanyo huu wa kazi katika miezi ya mwanzo ya uzazi. Ndiyo maana kukosa likizo ya uzazi kwa mama huonekana kama jambo la kutisha, ilhali kukosa likizo ya baba ni tatizo, lakini si kashfa ya kijamii.”
Iwapo familia ina watoto zaidi ya mmoja, mama kwa kawaida hutumia miezi au miaka kadhaa akiendelea na jukumu la malezi. Kwa wakati huu, baba huchukua jukumu la msingi la kipato. Hili halimaanishi kwamba wanawake hawaruhusiwi kufanya kazi wanaweza, mradi tu wanaweza kutimiza wajibu wao wa msingi wa malezi ya awali. Sasa, tuchukulie kwamba mwanamke ndiye Imam wa msikiti. Je, angeweza kuongoza sala mara tano kwa siku huku akimlea mtoto mchanga anayehitaji kunyonyeshwa au anatapika usiku? Je, aende msikitini na kumuacha mtoto, au abaki nyumbani na jamaa wanaosubiri sala? Makala ya Msikiti Mkuu wa Sheikh Zayed yanauliza;
“Ni wazi, hali kama hiyo haingefanya kazi. Hivyo, Uislamu, badala ya kujaribu kulazimisha mitindo ya kisasa isiyozingatia maumbile, umeweka majukumu haya mikononi mwa wanaume. Ulinganifu wa Kiroho Hata hivyo, hii haimaanishi kwamba Uislamu unawadunisha wanawake kiroho.”
Makala ya Msikiti Mkuu wa Sheikh Zayed inasema;
“Na anayefanya matendo mema, awe mwanamume au mwanamke, nayeye ni mwamini, basi hao wataingia Peponi.”
Sura ya 4, aya ya 125.
“Hakika wanaume na wanawake Waislamu, waumini, watii, wakweli, wenye subira, wanyenyekevu, watoaji sadaka, wafungaji, wanaojilinda na wanaomkumbuka sana Mwenyezi Mungu wote hao Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na thawabu kubwa.”
Haya ni ya Korani Sura ya 33, aya ya 36.
Jamaa yule aliyekuwa na Mwanakwetu akasema Aidha, katika Sura ya 66, waumini wote wanaume na wanawake wamefananishwa na wanawake wawili wema: Asiya mke wa Firauni, na Maryam mama wa Yesu. Hii inaonyesha kuwa Uislamu hauwaoni wanawake kuwa duni kiroho. Kwa hiyo, Uislamu unakubali tofauti za kijinsia, lakini hauzichukulii kama ubaguzi. Unazielekeza, unazidhibiti, na kuziweka katika mfumo unaowezesha kila mtu mwanaume au mwanamke kustawi kwa uwezo wake bora zaidi.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo? Katika Makala haya kuna maneno haya;
“Uislamu unakubali tofauti za kijinsia, lakini hauzichukulii kama ubaguzi. Unazielekeza, unazidhibiti, na kuziweka katika mfumo unaowezesha kila mtu — mwanaume au mwanamke kustawi kwa uwezo wake bora zaidi.”
Kwa maelezo haya Mwanakwetu anaamini kuwa Rais Samia Sukuhu Hassan pale tunapompima kwa jinsia yake ni kosa kubwa sana, jambo la msingi ni kumpima ana uwezo gani wa kutatua changamoto zozote za Watanzania kwa sasa? Mathalani namna anavyopambana na watekaji? Kwa namna gani analinda uhai wa Watanzania?
Kwa hakika yako majukumu ya Mwanamke ambayo anaweza kuyafanya kwa umahiri mkubwa mathalani kunyonyesha mtoto, kubeba ujauzito ambayo mwanamme hawezi kuyafanya hata kidogo. Kikubwa kila mmoja wetu atapimwa kwa namna anavyotekeleza majumu aliyogatuliwa na jamii yake.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya yaitwaje? Shida Imamu Mke? au Shida Uwezo wa Kuifanya Kazi Hiyo? Mwanakwetu siku ya leo anachagua Shida Imamu Mke.
Nakutakia Siku Njema.
makwadeladius @gmail.com
0717649257
Post a Comment