“Kwani Humphrey Polepole anagombea mwanamke na mtu yoyote yule? Ni mwanamke gani huyo? Kwani Polepole kachukua mbuzi wa mtu? Hao wenye ugomvi na Polepole wamuachie, sisi hatuna ugomvi nayeye iwe upinzani na hata sisi CCM.
Kama mwiba ni yaliyokuwa anayasema, sawa wachambue moja baada ya lingine na watoe majibu. Kwa sababu kumkamata Polepole siyo kwamba yale aliyoyasema yamejibiwa, la hasha! Aliyoyasema bado yapo akilini mwa Watanzania, yanazunguka na sasa inajulikana kuwa kutekwa kwake kisa ni yale aliyayatamka na yasipojibiwa na yasipojibiwa vizuri kwa weledi, madhara yake ni makubwa sana, Polepole awe hai na hata Polepole awe mfu.”
Mjadala huu unaendelea;
“Hawa jamaa, wanashangaza sana, kwa hali ilivyo sasa kama mwalimu Julius Nyerere angekuwa hai basi jamaa wangemteka, Mwalimu Julius Nyerere amekufa na somo la kuwaachia wananchi waseme waliyo nayo moyoni somo hili lipo wazi na mwanafunzi wake hodari ni Jaji Warioba, huu mwenendo wa kutekana ni mbaya.
Tanzania inao viongozi wengi wastaafu, kutoka vyama vyetu vya siasa na hata serikalini je wazibe midomo yao hata kama hali ni mbaya? Kwa hali hii wakae kimya? Wakishauri vinginevyo mambo yatakuwa kama yale yale ya Humphrey Polepole? Huu mwenendo ni hatari kwa umoja wa taifa hili, Watanzania tumegawanyika sana, wasidhani sisi ni wamoja kweli mpaka sasa, tumegawanyika sana, tumegawanyika sana ; kwa makabila yetu , kwa ukanda wetu.
Ebu tazama kwa baadhi ya makabila ya mipakani, yana udugu na nasaba kwa ujirani mkubwa na mataifa jirani yao, kuliko makabila ya upande wa kati ya Tanzania na hata upande mwingine wa taifa hili, pia hata madhehebu yetu ya dini.
Tazama pale anapotekwa mtu, jamii inajiuliza huyu jamaa ni wa wapi? Huyu jamaa kabila gani? Huyu jamaa amewahi kukaa wapi? Huyu jamaa anasali wapi? Huyu jamaa amaesoma wapi?
Maswali haya yameulizwa sana hata pale alipotekwa komredi Polepole . “
Mjadala uliendelea huku Mwanakwetu akinukuu kila kitu.
“Kwa sasa jamii ya Watanzania inaonesha kupoteza matumaini kutoka kwa wanasiasa, imepoteza matumaini kutoka kwa vyama vya siasa.
Kwa sasa wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wamekuwa matumaini yao, wakipita njiani watu wanashangilia, wanapiga makofu, wanapiga miluzi wanapiga vigegele. Hali hii haijawahi kutoka kwa miaka karibu 40 sasa, siyo kwamba haijawahi kutokea kabisa ilitoka wakati wa Vita vya Kagera kupambana na Nduli Idd Amin Dada wanajeshi walipokuwa wakienda uwanja vita ndani ya mabasi na malori walishangiliwa mno na hata mara baada ya kurudi vitani walishangilia pia.
Swali ni je kwanini Watanzania sasa wanashangilia JWTZ ? Mbona vikosi vingine vya Majeshi yetu havishangiliwi?JWTZ wamefanya jambo gani jipya kwa sasa?Je Watanzania wana nini kwa sasa?”
Hawa jamaa wapo mbele, naye Mwanakwetu yu nyuma yao, jamaa wakitembea taratibu, umri wao ni watu wazima, naye Mwanakwetu akitembea taratibu sana ,huku akijifanya anaongea na simu ya mkononi. Mwanakwetu yu nyuma yao hawa ndugu mbele.
Safari hii ya miguu inaendelea wakafika eneo la makaburi huku kundi la vijana wakichimba kaburi.
Mkono wa shoto kaburi linachimbwa na mkono wa kulia bodaboda kadhaa zimepaki. Mzee mmoja mbele ya Mwanakwetu akawasemesha wale vijana wanaochimba kaburi kwa maneno haya;
“Mbuya Mwaraye…. ! Poreni Nurukuu…! Ndohe Moreveka…!”
Mwanakwetu akawa usawa sawa sawa na hawa ndugu kisha akawasalimu …
“Jamani Tumsifu Yesu Kristo…!”
Ndugu hawa wakajibu milele amina, Mwanakwetu akawa anawavuka huku akijiuliza akilini mwake, niwasaidie kuchimba kaburi hawa jamaa? Niwachangie hata 2000/ ya maji ya kunywa?
Mwanakwetu alifanya maamuzi haraka haraka akilini kuwa nikasali kwanza kanisa maana hiyo ni saa mbili na dakika 53 kisha nitakapo rudi nitashiriki kuchimba kaburi hilo, haya ndiyo yalikuwa maamuzi ya Mwanakwetu akaenda zake kusali.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kikubwa mpaka sasa ndugu yetu Humphrey Polepole yu mikononi mwa watekaji. Mwanakwetu kwa makala anawaomba watekaji wote wafahamu kuwa haya mambo hayana tija, yanaivunjavunja Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vipande vipande. Tanzania mnayoiona leo hii haikuwapo, kila mmoja alikuwa anaishi katika msitu wake, akilala pangoni pake na yeye na jamaa zake, msidhani kipo kitu kinaitwa Tanzania; kina miguu , kina mikono, kina tumbo na kina kichwa. Tanzania kama taifa ni dhana tu iliyojengwa na Mwalimu Julius Nyerere na wenzake dhana hii itadumu kama kutakuwa na kusikilizana, kuvumilia, kujibu hoja kwa hoja na siyo tabia ya kuyapiga rungu mawazo ya wengine.Humprey Polepole alikuwa kiongozi mkubwa ndani ya CCM na ndani ya taifa hili kama watu kama kuna mtu amekwazika na maneno ya Polepole ameshindwa kuongea naye vipi kama kwa mtu ambaye hana nafasi.
Mwisho msomaji wangu kumbuka katika makala haya kuna lugha imetumika ambayo ni Kikurya ;
“Mbuya Mwaraye…. ! Habari zenu…! Poreni Nurukuu…!-Poleni na msiba…! Ndohe Moreveka…! –Mnazika Lini…:!”
Makala haya ni maalumu kwa ndugu yetu Humphrey Polepole huku yakiandikwa wakati bado ndugu Humphrey Polepole yu mikononi mwa watekaji.
Mwanakwetu upo?Je makala haya yaitwaje? Jamaa wangeweza kumteka hata Julius Nyerere kama angekuwa hai au mnazika lini? Manakwetu anachagua;
“NDOHE MOREVEKA-MNAZIKA LINI”
Nakutakia siku njema.
0717649257
NB Katika makala haya pale nilipotumia Lugha ya Kikulya Inawezekana kukawa na makosa kidogo ya sarufi na kimaantiki ya lugha hii ya Kikurya, lakini mie ndugu yenu Adeladius Makwega nimejitahidi kukariri maneno ya hawa ndugu na baadaye kuwauliza niliyokuwa nao jirani maana ya maneno haya, nawashukuru wote walionisaidia kutafsiri asanteni sana.
Post a Comment