Adeladius Makwega-Musoma TANZANIA
Oktoba 12, 2025, siku ya dominika, kila mmoja anajongea Kanisa kwake kusali na hapa Musoma Mjini nchini Tanzania hali ndiyo hiyo , wewe ndugu yangu Frank Kidani na wewe Rose Mary Kidani. umesali?
Huku kwetu hali ya hewa Mji huu kwa juma zima ni ya utulivu sana tunakula samaki, nayo Jumapili hii jua kali likiwaka , joto ni la Sentigredi 27, ujirani na mvua ni kwa asilimia 5, unyevuyenyevu ni wa asilimia 48 na upepo ukivuma kwa KM 11 kwa saa.
Mwanakwetu nayeye anafika Kanisa kusali, misa ya pili ya saa 3.00 ya Asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Agustino-Parokia ya Mwisenge, Jimbo Katoliki la Musoma.
Siku hii misa ikiongozwa na Padri Julius Ogolla.
Wakati wa mahubiri unafika na Padri huyu anasema maneno haya;
“Katika Jumapili hii tunakutana na mambo makubwa mawili yenye maana sana kwetu ; Kwanza neno la shukrani na Pili ni juu ya wagonjwa ambao walikuwa wanatengwa na jamii zao wakati wa Uyahudi. Nyakati hizo kulikuwa na magonjwa kama vile leo hii leo mathalani haya ya UKIMWI, MALARIA , UVIKO na hata mengine mengi.
Magonjwa haya hayakujali wadhifa wa mtu. Wagonjwa hawa walitengwa na jamii zao. Jamii hii ilikuwa na matabaka kadhaa lakini haya matabaka ya kutengwa yaliwaweka jamaa pamoja hapa ndiyo maana wakoma wakiwa pamoja kigulu na njia hadi wanafunga safari kwa Bwana Yesu.
Yesu hakuwatenga hawa ndugu, Yesu aliwaponya. Katika jamii zetu wapo watu kama hawa wakoma wapo watu wanaokubalika na wapo wengine hawakubaliki, hawa jamaa ule ukoma wao uliwafanya wawe pamoja, watembee pamoja hadi jirani na Yesu na kweli yeye aliwaponya.
Je mimi na wewe wenye UKOMA wa leo hii unatufanya tuwe pamoja? Je unamkimbilia nani? Jibu lake lazima kimbilio letu awe Bwana Yesu.”
Haya ni ya Parokia ya Mwisenge Jimbo Katoliki la Musoma nchini Tanznaia ambapo Mwanakwetu amesali.
Swali lengine ni Je hawa ndugu zetu huko Vatikani wanasema nini juu ya Dominika hii?
Huyu hapa Kadinali Luis Antonie Tagle Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojihusisha na Uinjilishaji wa Watu Ulimwennguni.
“Leo ni Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa, Injili ya leo inasimulia uponyaji wa wakoma kumi. Yesu alipokuwa akielekea Yerusalemu, aliingia katika kijiji kimoja. Wakoma wale walimwita, ‘Yesu, Mwalimu, utuhurumie.’ Yesu aliwajibu, akiwaambia, ‘Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.’
Mtakatifu Luka anatueleza kwamba walipokuwa njiani, walitakaswa. Hii ina maana kwamba waliponywa kwa rehema za Yesu aliyewaona. Alipowaona wakiteseka na kuwaambia waende wakajionyeshe kwa makuhani, Yesu pale pale aliwatamkia kuwa wameponywa. Kazi ya makuhani katika tamaduni zao wakati huo ilikuwa ni kuthibitisha kwamba wakoma wamepona na wametakaswa kweli.
Kinachogusa mioyo yetu katika tukio hili, ndugu zangu, ni kwamba yule Mkoma Msamaria, alipotambua kuwa ameponywa njiani, alirudi kwa Yesu na kumtukuza Mungu. Shukrani yake zilimsukuma kujionyesha kwa Yesu, kuhani pekee anayeweza kuthibitisha kuwa amesafishwa na kuokolewa.‘Simame uende zako; imani yako imekuokoa,’ Bwana akamwambia.
Leo mimi
na wewe tunamshukuru Mungu kwa nini?
Je, tunaona miujiza na baraka za Mungu katika maisha yetu?
Je, tunamrudia kumpa shukrani?”
Haya msomaji wangu ni Vatikani juu ya Dominika hii lakini usiyasahau yale ya Padri Julius Ogolla wa Parokia ya Mwisenge Jimbo Katoliki la Musoma.
Nadhani msomaji wangu nikupe na hili la ghadhabu za Mwanakwetu Kanisani. Katika misa hii ya Jumapili ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa hapa Katika Kanisa la Mtakatifu Agustino Parokia ya Mwisenga Ibada ya Misa ya Pilii, Mwanakwetu alighadhabishwa na aliyepanga nyimbo za misa hii, maana katika misa nzima haukuimbwa wimbo hata mmoja wa Mama Bikira Maria.
Mwanakwetu akasama kimoyo moyo;
“Shabashi(Haikubaliki) kwa aliyepanga nyimbo hizo za dominika yetu, inawezekanaje misa nzima ya dominika ya Mwezi Oktoba hakuna hata wimbo mmoja wa Mama Bikira Maria?
Wewe mwalimu wetu wa Kwaya, wewe Mwalimu wa Kwaya wa Parokia ya Mwisenge?
Tunakukumbusha kuwa Kwaya iliyoimba Misa ya pili ya Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa Oktoba 12, 2025 tunadai wimbo wa Mama Bikira Maria, Wewe Mwalimu wa Kwaya Wewe!”
Kwa ghadhabu hiyi Mwanakwetu aliamua kuuimba wimbo huu wa Mama Bikira Maria siku nzima.
“Tunahitaji Msaada Wako, Mama Maria, Mama Maria , Tuoneshe Njia…
Giza limeyafunika macho, Mama Maria Mama Maria Mama Maria Twapotea…”
Mwanakwetu upo? Kumbuka
“Mwalimu wa Kwaya Anadaiwa Wimbo wa Mama Bikira Maria.”
Nakutakia Jumapili Njema.
0717649257
NB Makala haya yametayarishwa kwa Heshima zote ya Mama Bikira Maria.
Post a Comment