MAFANIKIO NI MUENDELEZO WA KUAMINI MAMBO MADOGO

 

Samson kalekwa

Mwanakwetu Blog

Baada ya kutafakari sana Ninaweza kusema kwamba Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo vijana wengi wamekua wakilalamikia tatizo la ukosefu wa Ajira kwani wengi wamehitimu elimu za juu lakini wanakosa chakufanya kulingana na kile walichosoma na kuwafanya kuingia katika harakati za kutafuta mkate wa kila siku kwa kufanya kazi mbalimbali tofauti na elimu zao.

Inafahamika kwamba Kila mwanadamu anapenda mafanikio lakini si kila mtu yuko tayari kwa safari yake.

Najua utakua unajiuliza sana kwanini Mwanakwetu anasema hivyo yamkini ukweli ni kwamba, Ndoto ni rahisi sana kuota, lakini ni nidhamu, heshima, na sala zinazoifanya ndoto hiyo iwe hai.

Katika dunia ya leo yenye haraka, watu wengi wanatafuta njia fupi ya kufanikiwa, lakini ukweli unabaki pale pale: hakuna mafanikio ya kweli bila maadili na bidii.

Mwanakwetu anaamini kuna vitu sita vya muhimu ambayo kila mtaftaji au mpambanaji anapaswa kuvipa kipaumbele zaidi katika harakati zake za kuyatafuta mafanikio, japo wemgine watakuwa wanajiuliza kwani mwanakwetu ni mtu aliyefanikiwa sana mpaka aanze kutuandikia vitu vya kuzingatia! Lahasha mwanakwetu nayeye pia ni mpambanaji na mtaftaji kama wengine tu.

1. Sala (Ibada): Kusali (kufanya sala au dua) inaaminika kuwa ni chanzo cha nguvu isiyoonekana kwa macho ya nyama bali kiroho. Kila mafanikio ya kudumu huanza na imani.

Sala siyo tu ombi kwa Mungu, bali ni mazungumzo ya ndani yanayojenga ujasiri, utulivu na maamuzi sahihi.

Anayesali kwa moyo safi hujua lini achukue hatua na lini asubiri.

Maombi ni dira, yanapounga mkono juhudi zako, kila hatua inakuwa na maana.

“Mtu anayesali hujua amesimama wapi, hata dunia inapoyumba.”

2. Nidhamu: Nidhamu ndiyo daraja kati ya ndoto na matokeo. Ni kufanya jambo sahihi hata lisipokuwa rahisi, kwa sababu unajua thamani yake.

Watu waliofanikiwa si wale wenye vipaji zaidi, bali wale wenye nidhamu ya kudumu.

Nidhamu ndiyo inakufundisha kuamka mapema, kuendelea kujifunza, na kuamini kuwa kila hatua ndogo ni sehemu ya safari kubwa.

3. Heshima: Heshima ni tunda la moyo wenye hekima.

Ni kujua kwamba kila mtu, awe mkubwa au mdogo, ana thamani mbele ya Mungu.

Wale wanaoheshimu wengine hupokea heshima bila kulazimisha.

Heshima inajenga daraja kati ya watu na Mungu, kati ya wazo na fursa.

Watu wanaoheshimu wanajua kushirikiana, na ushirikiano ndiyo moyo wa mafanikio.

4.Jitihada: Hakuna njia ya mkato kwenye mafanikio.

Maombi yatakuonyesha njia, lakini jitihada ndizo zitakufikisha.

Kila kazi unayofanya kwa moyo ni mbegu ya kesho.

Kuna siku utachoka, lakini usikate tamaa, jasho lako leo litakuwa ushuhuda wako kesho.

“Mungu hubariki mikono inayofanya kazi, si midomo inayolalamika.”

5. Uthubutu na Uaminifu: Mafanikio bila uaminifu ni kivuli cha heshima.

Kuwa na uthubutu wa kusimamia ukweli, hata kama ni vigumu.

Kuwa mwaminifu kwa Mungu, kwa watu, na kwa nafsi yako.

Uaminifu ni utajiri ambao hauibiwi, hauzeeki, wala haupotei.

Mtu mwaminifu hukosa kwa muda, lakini hushinda kwa kudumu.

6. Uvumilivu: Wakati mwingine mafanikio huchelewa si kwa sababu hujafanya vya kutosha, bali kwa sababu Mungu bado anaandaa mazingira.

Uvumilivu ni kipimo cha imani yako.

Usikate tamaa unapochelewa kufika kila kuchelewa kwa haki ni maandalizi ya ushindi mkubwa zaidi.

“Mafanikio si haraka, ni mwendelezo wa uaminifu katika mambo madogo.”

Baada ya Tafakari ya muda mrefu ya mwanakwetu ndipo akaona awashirikishe na vijana wenzake wa Kitanzania ambapo wapo katika hali ya kupambana kwa kesho yao iliyo bora.

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika Maisha yenye mafanikio ni yale yenye utulivu wa ndani, si kelele za nje.

Sali kwa imani, fanya kazi kwa bidii, heshimu kwa moyo, thubutu kwa uaminifu, na subiri kwa uvumilivu.

Mwanakwetu anakusihi haya kwasababu anaamini kwamba watu wengi wanapenda mkato hivyo Wakati wengine wakitafuta njia fupi, wewe jenga msingi imara Kwa sababu mafanikio yanayojengwa juu ya maadili hayatikiswi na upepo wa dunia.

“Omba kwa imani, fanya kwa nidhamu, heshimu kwa moyo, jitume kwa bidii, na shikilia uaminifu wako hapo ndipo Mungu huinua bila kelele.”

THINK BIG, AIM FAR

Kumbuka tu, Mafanikio ni mwendelezo wa Kuamini Mambo Madogo.

Nakutakia Siku Njema



Samsonrichard511@gmail.com

0654653936


0/Post a Comment/Comments