Alifika stendi ya mabasi Musoma Mjini, pahala wanapokata tiketi na kulipa shilingi 85,000 /- mapema ya mwaka wa 2025 ikiwa ni nauli ya kutoka Musoma kwenda Dar es Salaam, kisha kuingia basini. Safari hii ilikuwa ya bahati tu, maana kiti alipata cha mwisho kabisa, siku hii kulikuwa na abiria wengi mabasi machache. Baada saa 26 Mwanakwetu aliingia Mbezi Dar es Salaam majira ya nane mchana, akaenda kituo cha Daladala Mbezi, watu walikuwa kibao, Daladala zilizokuwa tupu zilikuwa zile zinakwenda Chalinze na Msoga tu, mie wa Mbagala nakwenda Msoga kufanya nini?
Mwanakwetu anakwenda kwao, mtu kwao lakini usafiri hakuna. Dar es Salaam haibadiliki shida zile zile miaka nenda miaka rudi! Huku akitakiwa kufika Mbagala kabla ya saa 10 jioni. Hapo hapa akafanya mawasiliano na nduguye mmoja na kumshauri ili aweze kuwahi huku kwao apande bodaboda, akisubiri Daladala atafika Mbagala usiku wa manane.
Kweli Mwanakwetu akafanya hivyo na kumchagua bodaboda mmoja mwenye kofia mbili na kukubaliana naye kwenda Mbagala kwa nauli ya shilingi 40,000/- maana yake kwenda na kurudi ni 80,000. Lo salale mie mwana wa Makwega, mjukuu wa Binti Omari wa Mkongeni.
Hapa atatumia dakika 45 na kweli ilikuwa hivyo na alifika Mbagala kabla ya saa 10 jioni. Mwanakwetu akiwa amefika kwao Mbagala akasema moyoni maneno haya;
“Umbali kutoka Musoma hadi Dar es Salaam ni KM 1,287 kwa nauli ya Shilingi 85,000/-, wakati umbali kutoka Mbezi hadi Mbagala Sabasaba (Mbuyuni) nyumbani kwa akina Mwanakwetu ni KM 40 kwa nauli ya boda shilingi 40,000/- na jumla kwenda ana kurudi iwe 80,000/- wakati kwa nauli halali ya basi za umma/ treni Mbagala Mbezi haiwezi kuzidi shilingi 900/-Huu ukiwa sawa na umbali kutoka Bonn kwenda Jiji Cologne nchini Ujerumani.”
Huku wakazi wenyewe wa Dar es Salaam wakizungumza maneno mengi, lawama nyingi dhidi ya serikali kupitia kwa wale wanaokuwa nao jirani wakiwamo utingo, madereva na watumishi wa miradi hii ya umma ambayo imeonesha ugoigoi mkubwa na malalamiko yasiyokwisha tangu enzi ya UDA hadi leo hii ni DART ya Mwendokasi.
“Unaweza kusema nini? Wewe unaendesha basi lao tu, ili niwe salama na kuepuka kupigwa na abiria hawa, mie nikiwa ndani ya steringi nakuwa kimya wao watasema wee wakifika watakaa kimya, kisha watashuka, kikubwa Napata mshahara wangu hivyo ndivyo ninavyofanya. Nikiona kila kona kelele nitarudi znagu Mbezi niendeshe mabasi ya mikoani kama zamani.”
Haya ni maelezo ya dereva wa mradi wa Mwendokasi Jijini Dar es Salaam ambaye jina lake linabaki kibindoni. Swali ambalo Mwanakwetu anajiuliza ni hili, je hali hii ilivyo na changamoto zote hizi je wafanyamaamuzi wanapata taarifa sahihi ili kufanya maamuzi sahihi kwa manufaa ya jamii wa Watanzania?
Swali hili lilimfikirisha mno Mwanakwetu na ndiyo linaloyajenga makala haya siku ya leo kwa heshimu ya Wadaresalaamaiti wenzake.
Kichwa cha Mwanakwetu kikakumbuka kisa hiki alichosimuliwa miaka karibu 12 iliyopita;
“Hapa tuna maktaba mbili ya wazi na maktaba ya siri. Hii Maktaba ya wazi zipo kanda kadhaa za sauti zilizorekodiwa ambazo zinaweza kutumika muda wowote ule lakini zipo za kanda zingine katika maktaba ya siri ambazo zinaweza kutumika kama rejea lakini kwa utaratibu maalumu ambapo zamani vikao hata vya siri vilikuwa vinarekodiwa, zipo hapa ili wale wanaotaka kujifunza na wafanye hivyo.zipo za kanda z aviongozi kadhaa wakubwa tangu Julius Nyerere na wenzake, sina hakika kama sasa hivi vikao vyenu vya siri vinarekodiwa, siri inabaki katika faili na inakuwepo katika mkanda mzima wa sauti juu ya mjadala mzima, namna maamuzi fulani magumu yalivyofikiwa.”
Mwanakwetu akawa anamsikiliza kwa umakini mkubwa huyu mkutubi nah ii elimu ya maktaba.
“Mara baada ya Vita Kagera Tanzania ilipitia hali ngumu mno ya kiuchumi na hata ya kisiasa, wakati huo ndiyo utawala wa Julius Nyerere unakaribia kufika mwisho mwisho, kesi kadhaa za uhaini na wakati huu ndipo Edward Moringe Sokoine anafariki dunia akiwa Waziri Mkuu baadaye Mwalimu Nyerere akamteua Salim Ahmed Salim kuwa waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 24, 1984.
Unajua wakati huo mimi nilikuwa kijana mdogo, nakumbuka Mhe Salim Ahmed Salim alifanya ziara kwenye kambi zetu za JWTZ huku sisi tulikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ziara moja nilikuwepo, tukafika na vifaa vyetu katika mhe. Salim akaomba viongozi wa wapinaji watoke ukumbini ili akabaki na wapiganaji wa ngazi ya chini, akaoangea nao weee kwa kuwasikiliza mmoja baada ya mwingine kwa uhuru mkubwa, kisha akamaliza alafu wakaitwa wale wakubwa wao ukumbuni, Dkt. Salim Ahmed Salim akatoka maagizo yake, kisha sie tukaondoka zetu.
Salim Ahmed Salim alikuwa muungwana sana, nakumbuka aliifanya kazi hiyo hadi Novemba 5, 1985 alipoingia Ali Hassan Mwinyo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndipo akateuliwa mhe. Joseph Sinde Warioba kuwa Waziri Mkuu.”
Kumbuka Mwanakwetu anaongea na Mkutubi huyu, huyu mzee akaendelea kusema maneno haya
“Siku hivi viongozi wanaongea wenyewe kwa wenyewe, hawatoi fursa ya kuongea na watu wa kawaida, hawatoi fursa ya kuongea na walio chini yao, viongozi wetu wamekuwa wavivu, mathalani Bodi zote za Maashirika ya Umma wanaokaa vikoani ni viongozi wa taasisi husika, wajumbe wa bodi na mwenyekiti wa bodi, upo wapi ushiriki wa wafanyakazi moja kwa moja? Mkurugenzi wa Utawala hawezi kuwasilisha hoja za wafanykazi kwa toni ya wafanyakazi katika bodi, vyama vyote vya wafanyakazi vimekuwa vijiwe vya kula michango ya wafanyakazi tu hakuna kazi wanayofanya, wafanykazi hawaoni umuhimu wa vyama vya wafanyakazi. Kwa sasa mashirika ya umma na taasisi nyingi zitaingia katika matatizo makubwa maana wafanyakazi hawana pahala pa msaada zaidi kuungana na jamii inayolalamikia, wananchi wanalalamika, wafanyakazi wanalalamikia taasisi, hali hii mwisho wake ni vurugu lazima itokee na shida wanabebeshwa polisi wa kutuliza ghasia, hali hii itaendelea hadi lini?”
Jamaa huyu aliendelea kusema kuwa hata wafanya maamuzi ya mwisho hawana taarifa sahihi lakini wafanyakazi wa chini na jamii inazo taarifa sahihi na ili upate taarifa sahihi lazima ufanya kama alivyofanya Salim Ahmed Salim mwaka 1984 alivyozungumza na wapiganaji wa JWTZ. Kisa hiki ni cha miaka 12 nyuma ya mwaka 2025. Mwanakwetu anasema nini siku ya leo? Kwa hakika msomaji wangu natambua sasa umeelewa vizuri umuhimu mkubwa wa kujua mawazo ya watu chini juu ya jambo fulani likoje? Hapa umetambua hata namna ya kupata taarifa hizo sahihi kama wewe ni kiongozi na unataka kushamiri katika uongozi wako.Usipofahamu hili unapoteza muda wako wa kufanya maamuzi yoyote yale na hata uongozi wako hapo kesho utasimuliwa vibaya angalia Salimu Ahmed Salimu anavyosimuliwa vizuri mwaka 2013 miaka karibu 30 baada ya tukio hilo. Salim Ahmed Salim leo hii hana uwezo hata kuita wana habari na kuzungumza nao lakini kisa hiki alichosimuliwa Mwanakwetu kipo akilini mwake na leo kinasimuliwa vizuri.
Jamani tujifunze katika haya, sasa kwa kuwa Mwanakwetu ni mkazi wa asili wa Dar es Salaam, mwana Dar es Salaam (Daresalaamite) huku katika ardhi ya Jiji hili yako makaburi ya ukoo wake tangu enzi na ya miaka mingi sana, sasa anaomba kwa hisani yako msomaji wake aseme jambo juu ya MWENDOKASI JIJINI DAR ES SALAAM.Kwanza ndugu msomaji umfahamu bdugu Athuman Mbuttuka;
“Huyu jamaa awali alikuwa Deputy Auditor General na Rais Magufuli alibaini utendaji mzuri wa ndugu Mbuttuku akiwa huku hasa alipojenga ushirikiano mkubwa ndani wakaguzi wa ndani Serikalini , ambapo baadhi ya watu wanaona kuwa tangu Mbuttuka aondoke hali sasa ni tete, huyu jamaa akachaguliwa Januari 6, 2018 kuwa Msajili wa Hazina ambapo kazi hii aliifanya vizuri hadi 2023 alipochagliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati ambapo baadaye uteuzi wake ulitenguliwa wakati wa sekeseke la mikatiko ya umeme.”
Katika hoja juu ya utenguzi wa Athumani Mbuttuka baadhi ya watu wanasema Mbuttuka ni mchapakazi sana na utenguzi wake alionewa tu yanayosemwa kwa Mbuttuka ndiyo yanayosemwa kwa jina la pili ambalo litatupleka kwenye mwendo kasi naye ni Dkt. Edwin Mhede , ndugu huyu tangu mwaka wa 2020 ni Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania tangu mwaka 2019 hadi alipondolewa, amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Viwanda kwa sasa Dkt Mhede ni Naibu Katibu Mkuu Mifugo na Uvuvi awali pia Dkt Mhede amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yanayokwenda Kasi Dar es Salaam ambapo sasa msomaji wangu tumefika nilipokuwa napataka.
“Dkt Edwin Mhede alipofika DART alikuta hali yetu ya maisha ni mbaya, pesa tulikuwa tunakusanya vizuri lakini aliyekuwa kiongozi awali alikuwa mwoga sana , analinda cheo chake, wafanyakazi walikuwa na hali ngumu, ofisi zilikuwa chafu, mijadala ya awali ilikuwa kila unapotaka kutumia pesa lazima uombe kibali kwa Katibu Mkuu wa Wizara, mjadala ukawa kwani Katibu Mkuu ndiye Afisa Masuluhi? Jibu likawa hapana, kweli Dkt Edwin Mtede alipoingia tu kwanza aliboresha mazingira ya kazi, ofisini palikuwa pachafu akawema mazingira vizuri, wafanyakazi wengi waliokuwa wanadai maslahi yao walilipwa pesa zao zote za madeni na kazi ikawa inafanyika vizuri, wengi wa wafanyakazii mashati na magauni yao yalipauka na kuchujuka kidogo nafuu ikawajia.”
Ndugu huyu anaendelea kusimulia kuwa wakiwa kazini kulikuwa na hoja kuwa kuna kampuni inakuja kuwekeza mabasi yake ili yafanye kazi, lakini kampuni iliomba ipewa njia mbili zaidi na nauli katika njia hiyo walisema kama watapewa njia mbili basi nauli itakuwa nusu na ile iliyokuwa inatozwa kama ni shlingi 900/- iwe 450/- huku kampuni za matangazo zikawa zinalipa vizuri na wafanyakazi wakawa na amani vizuri sana kazini chini ya Uongozi wa Dkt. Edwin Mhede.
Mwanakwetu ni mwandishi tu yeye ananukuu neno kwa neno na Wala hamfahamu Athumani Mbuttuka wala hana Ujirani na Dkt. Edwin Mhede nah hata Benki anayoiongoza ya NMB Mwanakwetu haipendi. Lakini Wafanyakazi hawa wanahoja moja ya msingi ilikuwaje Dkt Edwin Mhede aliondolewa MWENDOKASI? Aliyefanya hivyo, aliyeshauri hilo ndiye chanzo cha yote haya ya mwaka wa 2025. Nani wa kulaumiwa kama siyo viongozi? Kwanini hawafanyi tathmini ya haki kwa viongozi wanavyokuwa katika shughuli zao za kiutendaji kwa kupata maoni ya wafanyakazi wa chini? Swali ambalo Mwanakwetu anajiuliza leo hii au Dkt Edwin Mhede na Athuman Mbuttuka ni kuku weupe wenye madoa meusi mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan? Wanaoitazama hali hii wanakwenda mbali sana hata wanatilia mashaka hata uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri DART David Kafulila, wanaipiga mbiu ya mgambo kuwa Kafulila hana uwezo wa kuifanya kazi hiyo, huku ikipitiwa kwa kina namna alivyokuwa Katibu Tawala na Mkuu wa Mkoa ameonexha umahiri gani?Huo umahiri utajwe hadharani.Nani kamdanganya Rais Samia kwamba Davidi Kafulila ana uwezo wa kuishauri juu ya mwendokasi?Hapa angetafutwa mwana Dar es salaam anayelijua jiji hili aifanye KAZI hii siyo Kafulula. Binafsi nimefanya KAZI na huyu ndugu anatabia ya kuwatisha watumishi na kukimbiia kushitaki ngazi za juu.Nakumbuka visa viwili vya madaktari wa binadamu nasema uteuzi wa Kafulila tunekosea na kutukosea watu wa DSM.Mradi wetu wa mabasi hauwezi kufanya vizuri chini ya ushauri wa mwenyekiti Kafulula KAZI hii imemzidi kimo..Kwa hakika Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuyafikia malengo ya utawala wake inaonekana wazi mlango wake mmoja umefungwa, hasa wenye jicho la watu walio chini.
“Huu mlango ufungulie mapema… rejea kisa hiki cha SalimuAhmed Salim, tena huyu ni ndugu yako kabisa.”
Kwa hakika siyo haki nauli ya kutoka Mbezi hadi Mbagala na kurudi iwe shilingi 80,000/- ilingana na nauli ya basi kutoka Musoma hadi Dar es Salaam … mama yangu weee hilo halikubalika. Ndugu zetu Mbuttuka na Mhede walionesha umahiri katika nafasi zao simulizi za utendaji wao kazini zinasimuliwa hadharaniili…Ili maamuzi sahihi yafanyike.
Mwanakwetu upo? Kumbuka
“MBUTTUKA MHEDE NI JOGOO WEUPEEEE WENYE MADOA MAWILI SHINGONI MEUS?’
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment