Adeladius Makwega
Awali mchana wa siku hii, Mwanakwetu alibeba vitu vyake na kuzunguka Mji wa Musoma…
“Kwa hakika sehemu kubwa ya maduka ya Mji huu yalifungwa, huku vituo vya wapiga kura vikiwa tupu.”
Mwanakwetu akiwa njiani alikutana na mgambo mmoja akauliza?
“Hapo hawa jamaa wanapopiga kura wapo?”
Yule mgambo wala hakumsalimu Mwanakwetu, yeye alimtwanga swali hilo tu Mwanakwetu akamjibu na akapishana na naye kisha kuelekea kituo cha kupiga kura ambapo muelekeo huo Mwanakwetu ndiyo alikuwa anatokea.
Saa 10. 47 Mvua kubwa inaanza kunyesha badala ya saa saba mchana, Mwanakwetu akajificha nje ya choo cha nyumba moja ambapo choo hiki kipo barabarani na kilikuwa na bati kidogo linaloweza kumsaidia anayejificha lakini manukato ya choo hiki ilihitaji uvumilivu.
“Kazi ni kwako wewe unayejificha mvua… kwanini unatembea bila mwavuli? na Kwanini unatembea bila viatu vya mvua?
Hakuna kulalamikia manukato ya choo hiki.”
Mwanakwetu akiwa hapo alimkumbuka bwana mmoja ambaye walisoma naye Tambaza mwaka 1993 alikuwa mtoro sana shuleni na mara nyingi ukimtafuta utamkuta chooni, wahuni wa Tambaza Wakamuita jina la FATHER OF TOILET kwa wale waliosoma TAMBAZA naomba nikumbusheni jina halisi ya huyu ndugu.
Kando ya choo hiki kulikuwa na nyumba ya bati lakini bati zake haziruhusu mtu kujificha mvua, Mwanakwetu akabakia katika kipanda hicho cha choo huku mvua ikipiga kama nusu saa.
“Mwanakwetu kaloani ndambandamba, vilivyo mvua inazidi .”
Upande wa pili na choo hiki kuna barabara ya vumbi, kisha kuna Kanisa la Menonite of Tanzania (KMT), mkono wa kulia wa kanisa hili kuna vituo viwili vya kupiga kura vya turubai jeupe laini, kituo kimoja kina vijana watatu wakiwa na bodaboda.
Kituo kingine cha kupiga kura hakina watu na nadhani matokeo yamebandikiwa huku yakipigwa mvua vilivyo, matokeo yamebandikwa katika mringoti wa umem/simu. Mwanakwetu akavuka na kwenda kujificha kituo hiki cha vijana wenye boda boda.
Mvua kubwa inanyesha lakini haina radi wala katarina. Mwanakwetu akawauliza hawa vijana nadhani walikuwa mgambo na mawakala wa chama kimoja cha siasa.
Mmemaliza kazi? Wakajibu ndiyo. Watu wamejitokeza? Hapa kwetu kidogo nafuu!Walijibu.
Mvua ikapungua, Mwanakwetu akaaga na kutoka akawa anaelekea mkono wa kushoto KMT. Akaenda kama mita mia tatu hivi, akakutana vituo viiwili vya uchaguzi na askari mmoja wa kike kaloana mno, binti mmoja ana mwili uliojengeka, huku akiwa amejificha mvua na wenzake kadhaa, nadhana wasimamizi wa Uchaguzi Wasaidizi wa vituo vyote jirani. Mwanakwetu akapita zake kuelekea barabarani huku akitafuta wakala ili aweze kutoa fedha katika simu yake.
Mwanakwetu alitembelea karibu KM tatu kila wakala wa fedha kafunga, maduka yamefungwa, mtandao wa internet haupatikani.
Mwanakwetu akafika kwa jamaa wanaouza chips akawauliza jamaa wakala gani hapo yupo wazi? Kijana wa Chips akasema mzee hali siyo nzuri lakini nenda hapo njia ya vumbi, achana kabisa na lami yupo jamaa yeye peke yake yupo wazi. Kijana wa Chips akamtazama Mwanakwetu kaloana mno akamuonea huruma kisha kijana akasema
“Hii simu yako itaharibika na mvua, Oya dogo…! Leta Nailoni Moja ya Viepe…”
Mwanakwetu akapewa nailoni na kuhifadhi simu yake, akamshukuru kisha kuanza safari kwa wakala wa kutoka fedha. Hapo msikilizaji wangu inakwenda 11.45 ya jioni ya Oktoba 29, 2025 Musoma Mjini, Mkoani Mara. Mwanakwetu akafika kwa wakala akamuuliza kaka una MPESA ? Jamaa akajibu ndiyo, Mwanakwetu akatoa fedha yake ya ngama kwa wakala anayefahamika kama KAIZA FRORIANI JEREMIA. Mwanakwetu alipotoa fedha akamshukuru wakala huyu na kusema, daa! Nimetembea umbali mrefu ili nitoe pesa hii, umenisaidia mno, wakala huyu akajibu ;
“Mzee ! Hali mbaya…
Huko NYAKATO hali ni tete… hali ni mbaya, nani afungue biashara yake ? Wote wamefunga, hata mimi nafunga sasa hivi…”
Mbele ya duka la wakala huyu ambaye alionekana anauza na vilezi kulikuwa vijana wengi, huku Mwanakwetu akisema moyoni kuwa vijana hawa pengine watamsaidia ndugu huyu kwa ulinzi kama akipata shida. Mwanakwetu alirudi kwa kijana muuza viepe na kununua , kumshukuru muuza viepe kwa msaafa wake wote kisha kurudi zake kwake. Hiyo sasa inakwenda majira ya saa moja usiku wa Oktoba 29, 2025.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Msomaji wangu kwanza haya ni makala ya rejea tu kwa hali aliyoiona Mwanakwetu Oktoba 29, 2025 katika eneo alipokuwapo siku hii. Jambo la pili kwa Jaji Mwambegele Hawezi Kubaki Salama ndani ya makala haya kwa haya yaliyosimuliwa;
“Jaji Mwambegele, katika maeneo yenye msimu wa mvua Tume Huru ya Uchaguzi Isitumie vituo vya maturubai ya jua kali, maturubai laini hayafahi hii hali inawatesa wanaofanya shughuli hizi mathalani vituo vyote vinne kando ya KMT kuelekea Mtakuja.Mengine kwa Jaji Mwambegele yatasimuliwa siku nyingine”
Mwanakwetu Upo? Je makala haya niyaitaje? Leta Nailo ya Viepe?Au Lakini Jaji Mwambegele Hawezi Kubaki Salama? Mwanakwetu anachagua… Hawezi Kubaki Salama.
Nakutakia Siku Njema.
0717649257

Post a Comment