Adeladius Makwega-KIJIJINI CHAMWINO IKULU
Aprili 13, 2022 Mwanakwetu alikuwa katika Kijiji cha Butiama ambapo ilitimia miaka 100 ya tangu mwalimu Julius Nyerere kuzaliwa na hapa ilifanyika shughuli kubwa, huku mgeni rasmi akiwa mzee wetu Mizengo Kayanza Peter Pinda. Mzee Pinda, huyu ni mjamaa siyo Bepari akiwa ni miongoni mwa Watanzania wachache wanaoweza kuyasimulia maisha ya Mwalimu Nyerere kwa namna ya kipekee. Mwanakwetu siku hiyo aliamuona mubashara mzee huyu maana ni kipindi cha miaka mingi alikuwa hajaonana naye kwa hiyo kwa hisani ya kumbukumu ya Mwalimu Nyerere ya miaka 100 ilifanikisha Mwanakwetu kumuona kwa jirani mzee wetu Mizengo Pinda. Mwanakwetu alitarajia katika kumbukumbu hiyo Mizengo Pinda angepiga zile suti za Chu Lai lakini mhe. Pinda hakufanya hivyo, alivaa koti na suruali za rangi tafauti Mzee Pinda alituangusha sana siku hii. Shughuli hiyo ilifanyika vizuri na muda wa jioni kila mmoja alianza safari ya kuondoka kurudi alipotoka.
Kwa hakika eneo hili la Butiama namna lilivyokaa ni vigumu mtu kuweza kupata usafiri wa moja kwa moja kuelekea Dar es Salaam , Mwanza au Dodoma. Msafiri anawajibu kutoka huko hadi Kiabakari hapo ndiyo barabara kubwa za kwenda katika miji hiyo mikubwa zilipo. Kwa kuwa shughuli ziliisha saa za jioni, kwa hiyo Mwanakwetu alitafuta usafiri wa kumtoa hapo, akiwa anatangatanga alimuona nduguye Shabani Kissu ambaye alikuwa mwendeshaji wa shughuli hii siku hiyo, nakumuliza swali hili,
“Kaka unarudi Dodoma?”
Shabaan Kisu alijibu kwa kusema Kiongozi wangu leo umekosa lifti , mie nakwenda Musoma kuna kazi nakwenda kufanya, siku hii Shabaan Kissu alikuwa na gari ndongo kama taksii aliyetoka nayo Dodoma lakini jamaa zako TBC wamekuja na Costa ongea nao. Mwanakwetu akatoka hapo akaunga na wafanyakazi wawili wa Wizara ya Habari /Utamaduni na kusogea jirani na basi la TBC la rangi nyeupe, huyu dada kwa sasa ni kiongozi mkubwa katika Wizara hii na kufika hapo kuwaeleza nia yao, hapo maombi yetu yaligonga mwamba.
“Basi letu limejaa, mwingine akisema jamani huku nyuma kuna nafasi. Jamani kweli tunamuacha mwenyekiti wetu wa zamani wa RAAWU hapa Butiama? Makwega achana kuwa Kiongozi wetu wa Wafanyakazi TBC, lakini amekuwa kiongozi Serikali kiongozi nab ado ni mtumishi wa wizara hii , tumamuachaje hapa Butiama?”
Watumishi wawili wa TBC wakawa wanatupiana maneno, mmoja injinia na mmoja Mtangazaji.
“Huyu anatufahamu vizuri hatuwezi kumuacha hapa, achene mambo yenu,achene siasa zenu, huyu bado ni ndugu yetu anayafahamu vizuri madhaifu yetu.”
Mtumishi wa tatu wa TBC alimalizia maneno haya lakini kwa hakika na ukweli wa Mungu Chairman Makwega aliachwa Butiama na wapiga kura wake wa zamani.
“Hassani Msumari, Ramadhani Muhoza, Edo Sanga, Abdallah Hemba, Andrew Sekiona, Saad Ally, Hosseah Mgohachi, Rashidi Sumuni, Mjusi Shemboza, Mwinyijuma Muumini na Dalila Msafiri.”
Safari hii ilikuwa nzuri sana lakini Mwanakwetu hawezi kusema kama zaidi angepanda basi la TBC maana ya huko hayajui kama kulikuwa na mazuri zaidi au la? Lakini yeye yaani Mwanakwetu leo hii anakusimulia ule uhondo wa ndani ya basi hili alilopanda na wanamuziki hawa. Japokuwa safari ilitumia saa zaidi ya 15 hadi Dodoma usiku mzima Mwanakwetu hakupata hata chembe ya usingizi.
Huku Dalila Msafiri akisema,
“Jamani huyu kaka yangu hapa kando yeye hasinzii kabisa yupo macho tangu Butiama hadi tunaingia Dodoma!”
Kwa kuwa mara zote Mwanakwetu amekuwa si mchoyo wa simulizi anaomba siku ya leo kwa heshima ya wanamuziki hawa na heshima ya Mgeni Rasmi wa miaka 100 ya kuzaliwa Mwalimu Julius Nyerere anaomba kwa hisani yako pia msomaji wake akusimulie simulizi moja kati ya simulizi 22 zilizosimuliwa basini huku Mwanakwetu akiwa amekaa kiti jirani na mlango wa kutoka ndani ya basi hili, mwanamuziki mmoja ambaye hakuwa Dalila Msafiri alisema kuwa jamani tunafanya kazi lakini mtu ukistaafu mmm huko vijiji kwetu kuna mambo. Hapo kila mmoja ndani ya basi masikito yalitegwa kama dishi la runinga.
Kumbuka Aprili 13 ilikuwa siku ya mfungo wa Ramadhani kwa mwaka 2022, huku waliofunga Ramadhani wote akiwamo mwanamuziki Mwinjuma Muumini walishafuturu, sasa wanapita Mbuga ya Serengeti.Msimuliaji sasa aliendelea kusimulia;
“Katika kijiji kimoja kulikuwa na jamaa akifanya kazi katika mbuga za wanyama, watu wengi walimtambua kuwa ndugu huyu alikuwa ni gemu wa mbuga hiyo, huku akitajwa na nduguze kijijini kama mjuzi wa kupambana na wawindaji haramu. Ndugu huyu alifanya kazi katika mbuga hiyo kwa miaka kadhaa na ulipofika wakati wa kustaafu alilipwa kilicho chake na kuamua kurudi kijijini kwao.”
Mwanakwetu msimuliaji huyu aliendelea kusimulia huku basi hili likipita kwa kasi mbuga hii ya Serengeti.
“Kutokana na mazoea ya kufanya kazi kila siku na kuamka kwenda kazini, ndugu huyu alitamani kuwa na kazi ambayo itamsaidia ili awe bize kama yupo kazini hapo kijijini baada ya kustaafu, kazi ya hadhi yake aliyotamani kuwa nayo ni Mwenyekiti wa Kijiji ili awe bize na utatuzi wa migogoro ya kijijini hicho alichozaliwa. Kwa hiyo alimfuata Mwenyekiti wa Kijiji aliye madarakani ili amuachie hiyo nafasi. Kweli mwenyekiti aliye madarakani alimwambia kuwa ombi lake amelisikia lakini hapo kijijini hakuna Uenyekiti wa Ubwete (bure).J amaa alimwambia, sasa mwenyekiti aliye madarakani ampe hekima zake katika jambo hilo. Mwenyekiti aliye madarakani kwa kuwa alikuwa anahitaji wasomi washike nafasi ya uenyekiti kijijini hapo hakuwa na hiana alimwambia arudi nyumbani kwake na aje baada ya majuma mawili hekima itakuwa imepatikana- HEKIMA ZA MWENYEKITI WA KIJIJI.
Jamaa alirudi nyumbani kwake huku ulevi wa kuamka asubuhi na kwenda kazini ukiwa umemuingia damuni mithili ya mvinyo isiyoonekana kutoka katika utumishi wa umma aliyoufanya kwa miaka karibu 27. Haya majuma mawili ya kuyangoja yalikuwa sawa na miezi sita kijijini hapo. Huku wanakijiji wenzake wakiendelea na maisha yao kama kawaida na jambo hilo likimstajabisha mno ndugu huyu. Mwishoni mwa juma la pili huku juma la tatu likikaribia kuanza, mgambo wa kijiji hicho alitumwa na mwenyekiti kumfuata mstaafu huyo. Mstaafu huyu alifika kwa mwenyekiti kuitikia wito, mwenyekiti akamjulisha ndugu huyu kuwa kuna jambo hapo kijijini kuna taarifa ya simba kuonekana katika mipaka ya kijiji chao. Kwa kuwa alikuwa akifanya kazi mbuga za wanyama basi anawajibu wakumsaka na akifanikiwa kumuua atakabidhiwa Uenyekiti wa Kijiji.”
Mwanakwetu msimuliaji anasimulia huku basi linakata mbuga nao Waisilamu waliokuwa wanafunga saa zikisonga ili wale daku, daku la safarini. Kumbuka safari hiyo ya usiku kwa usiku.
“Baada ya makubaliano hayo mwenyekiti aliitisha mkutano wa kijiji na kuwaeleza tukio hilo la simba huku wanakijiji kukaa kwa tahadhari huku ndugu zao wakiingia msituni kumsaka simba huyo. Huyu ndugu yetu amestaafu ugemu serikalini, kwa hiyo ni hodari mno wa kupambana na wanyama wakali katika mbuga sebuse huyu simba mmoja wa ualani? Katika kazi hii anaambatana na wanamgambo watano wa kijiji kumsaidia.”
Mwenyekiti aliwahakikishia wanakijiji wake kuwa kazi hiyo itafanyika vizuri maana kijini kina gemu mzoefu.
“Kweli safari ilianza na kuelekea kumsaka simba huyo kabla ya kuleta madhara kijijini. Kwa hiyo kikosi cha watu sita kilianza safari hadi msituni wakimsaka simba huyo. Walizunguka zunguka wapi, siku ya kwanza, ya pili hivyo hivyo hadi siku ya sita jioni waliamua kupanda juu ya miti kupumzika maana simba hakuonekana, kandoni kukiwa na mto unaopitisha maji ambapo wanyama kadhaa hunywa maji ya mto huu.
Kabla ya kupanda juu ya miti hiyo walikula posho zao za mabumunda na asali wakanywa maji na kupanda juu ya miti mikubwa sita. Wakiwa wamelala juu kila mmoja na gobore lake kwapani walipatwa na uzingizi mzito kutokana na miti hiyo kuwa na upepo mwanana lakini kijana mmoja wapo alikuwa macho. Simba alifika pale walipolala na kujilaza chini ya mti wa yule ndugu ambaye alikuwa akifanya kazi mbuga za wanyama. Kijana aliyekuwa macho alidhani anaota, aliyafungua macho yake vizuri akamuona simba dume amejilaza kwenye kisiki cha mti mmoja, akawasitua wenzake kwa lugha ya ishara. “
Yupo(simba) chini ya mti. Kijana huyu alitoa ishara hiyo kwa wenzake; simulizi iliendelea kusimuliwa ndani ya basi hilo.Yule ndugu ambaye alikuwa mstaafu kutoka mbugani kwa woga wa kumuona simba alichanganyikiwa huku kila kitu kikimtoka hapo hapo juu na kumuangukia simba yule, naye simba kutimka mbio mgongoni akiwa mstaafu huyu.
“Mstaafu alikamata masikio na nywele za simba dume huku akitambua kuwa akimuachia basi ataliwa hapo hapo, naye simba akifuata maelekezo ya jamaa mstaafu juu ya mgongo wa simba.
Wenzake walishuka juu ya mti na magobore yao wakachukua na gobore la mstaafu huku wakimkimbiza simba ambaye walidhani kuwa mwenzao analiwa. Kwa mbali huku wakikimbia walibaini kuwa walimuona simba akiwa amembeba mwenzao huku wakitaka kutupa risasi wakiogopa kuwa inaweza kuleta madhara kwa mwenzao. Wakidhani kuwa mwenzao alisomea namna ya kumpanda simba huku mbugani akiwa hai.
Simba na abiria wake mstaafu huyo walikuwa mithili wa dereva wa pikipiki aliyokuwa akikata mbuga porini. Simba huyo aliongozwa na ndugu huyu hadi kwa mwenyekiti wa kijiji.”
Mwenyekiti, mwenyekiti, mwenyekiti nimemleta mzima mzima! Mwenyekiti, mwenyekiti nimeleta mzima mzima, mstaafu alisema kwa sauti ya juu. Mweyekiti akasema ebo, unasemaje ? Majibu yalikuwa yale,
“Mwenyekiti mwenyekiti nimemleta mzima mzima!”
Mwenyekiti wa kijiji akasema kwa sauti kubwa,
“Ebo acha mambo yako bwana, mimi nilisema mlete akiwa amekufa na kwanza uenyekiti umeshaupata, rudi nae huko huko porini.”
Kweli jamaa alimuelekeza simba huyo vizuri katika mwembe ambao mikutano ya kijiji inafanyika simba huyu alijigonga katika kisiki hicho na kufa hapo hapo. Wenzake walioambatana naye walipofika hapo wakashangaza walichokiona kikitokea, mstaafu nayeye haamini kilichotokea. Baada ya siku kufa watu wamejaa mwembeni , jamaa aliyempanda simba akasema;
“Jamani mie mwenzenu katika mbuga za wanyama sikuwa gemu bali nilikuwa mpishi tu…”
Maneno kadhaa yakimtoka.
Mstaafu alisema maneno hayo. Jamaa wenzake wakisema kama mpishi tu wa mbuga za wanyama mambo yako hivyo, vipi kwa gemu wenyewe? Wenzake wakiongeza kuwa mstaafu alikuwa kiongozi wa magemu maana mambo ya kuwapanda simba wakiwa hai ni hatari mno na huo ni ujuzi wa hali ya juu. Mbiu ya mgambo ilipigwa na wanakjiji waliwapongeza kwa kufanikisha kumuuwa simba yule na ndugu huyu kukabidhiwa Uenyekiti wa Kijiji huku mwenyekiti wa zamani wa kijiji akigoma hata kutokea kikaoni akisema kuwa kama uenyekiti wenyewe wa sasa wa mambo ya kuwapanda simba wakiwa hai hataki hata ujirani na mwenyeekiti mpya maana yeye ameshatamka kumkabidhi pale pale simba alipofikishwa nyumbani kwake akiwa hai nani anataka ujirani na mwenyekiti wa mazingaombwe?
Ama kweli hakuna Uenyekiti wa Ubwete,
Mwanakwetu lumbuka safari ya kutoka Butiama kwenda Dodoma ilifika mwisho wake baada ya kushuka Njia Panda ya Chamiwno Ikulu (Buigiri) na wanamuziki hawa kuendelea na safari yao kwenda Dar es Salaam, huku akisema moyoni hivi Vijiji vya Ujamaa vya Mwalimu Nyerere vina simulizi nyingi sana.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika binadamu kwa namna alivyo anapenda kupata baadhi ya vitu kwa wepesi sana, kuhangaikia kuvipata vitu hivyo hawataki huo ndiyo ubinadamu ikumbukwe kuwa hakuna kitu cha ubwete katika ulimwengu huu, ukikipata kitu kwa ubwete na kitakuponyoka kwa ubwete tu.Shida ya uongozi siyo kuupata unaweza kwa ngekewa lakini hakuna kuutumikia uongozi kwa ngekewa lazima uchape kazi, hapo ndipo balaa linakuja.Haiwezi kutoke tana ukamuangkia simba na kumpanda mgongoni na kumshika nywele na masikio tena ukifanya hivyo tena unakwenda na maji .
Mwanakwetu upo?
Je Makala haya yaitwaje? Uongozi wa Ubwete?Wafanyakazi Walimuacha Mbugani Mwenyekiti Wao wa Wafanyakazi? Wanamuziki Walimpa Lifti Mwanakwetu au Hekima za Mwenyekiti? Mwanakwetu anachagua Hakuna Uongozi wa Ubwete.
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
NB SIMULIZI HII IMEANDIKWA NA MWANAKWETU KWA HESHIMA ZOTE KWA MIAKA 100 YA MWALIMU NYERERE LAKINI KWA HESHIMA YA WAZEE WETU WASTAAFU AKIWAMO MIZENGO PINDA ALIYEKUWAPO SIKU HIYO. NAWAOMBA WAISOME SIMULIZI HII ALAFU WAWASIMULIE WAJUKUU ZAO SIKU WAKIWATEMBELEA ..
Post a Comment