... YALIYOKATIKA GAFLA BINI VUU

 

 

Adeladius Makwega –Musoma MARA

Katika hali isiyo ya kawaida, Kitabu cha Wageni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara Septemba 15, 2025 kimeweza kusainiwa na wageni wengi kuliko siku yoyote ile ambapo Mkoa wa Mara ulipokea ugeni mkubwa kutoka nchini Kenya, wakiwamo Mawaziri kadhaa, wabunge na viongozi wengine kutoka serikali ya nchi hiyo walipomtembelea Kanali Evans Alfred Mtambi Ofisini kwake iliyopo 13 Barabara ya Boma, Mukendo Musoma Mjini. 

Katika ugeni huu Mwanakwetu alivutiwa na mama mmoja aliyeonekana kama Mmaasai, alipovutiwa na mama huyu Mwanakwetu aliongea neno, kisha kuomba ampige picha, mama huyu, mama huyu alikubali kupigwa picha na Mwanakwetu bila hiana.

Kando ya eneo hili alikuwepo Katibu Tawala Mkoa wa Mara Mwalimu Gerald Musabila Kusaya, ujirani huo ukasababisha Mwanakwetu ashindwe kusema neno la pili, baadaye Katibu Tawala aliingia ndani kisha Mwanakwetu uwanja ukawa huru, hapo hapo hakupoteza muda akaomba namba ya simu ya mama huyu wa Kimaasai alitoa kadi iliyoandikwa mheshimiwa David Ole Sankok mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.


 

Baadaye akaja baba mmoja aliyevalia nguo zinazofanana na huyu mama za rangi ya njano, Mwanakwetu akawapiga picha hapo hapo, lakini picha hii  Mwanakwetu hakuitilia maanani sana, akili yake ilikuwa kwa yule mama wa Kimaasai aliyempiga picha awali na kumuomba kadi yake ya mawasiliano. 

Kadi hiiMwanakwetu akaisoma kisha ikamshitua mno mbona aliyetoa kadi ni mwanamke wakati jina kadini ni la mwanaume? 

Hilo halikumpa tabu sana yapo majina ya namna hiyo mathalani Andrea ambapo mataifa kama Ujerumani majina haya yanatumika kwa wanawake.

Hapa hakuna shida na shaka lakini hakupata jibu, viongozi hawa walipoingia ndani wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara yule baba sikumuona lakini alikuwepo baba mmoja alikuwa anaongea sana na akisaini kitabu cha wageni akiwa na nguo za kijani. 

Katika ugeni huu viongozi kadha walisalimiana na Kanali Mtambi kisha kuingia ofisini kwake na kusaini vitabu viwili vya wageni vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Ndani ya kikao hiki yakazungumzwa mambo mengi; yawe ya kijamii na ya kiserikali, kidogo akili ya Mwanakwetu imevutiwa na mama yule wa Kimaasai aliyependeza sana, Mwanakwetu akisema yule mama nitamtafuta tu baadaye niongee naye natamani nimepeleke kwetu Mbagala Sabasaba akaogele Bahari ya Hindi na kupiga mbizi Mto Mzinga.

 Ugeni huo ukaondoka zake, Mwanakwetu akabaki ofisini kisha akaamua kuomba vitabu vya wageni viwili kimoja cha Katibu Tawala na kingine cha Mkuu wa Mkoa wa Mara ili ajue akina nani ndiyo walifika hapa mkoani? 

Wakati Mwanakwetu anafanya hivyo akabaini kuwa mawaziri ,wabunge na viongozi kadhaa wa Serikali ya Kenya na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamesaini vitabu vyetu viwili.

Katika pekua pekua akakutana na jina la David Ole Sankok ambaye ni mbunge wa Afrika ya Mashariki kutoka nchini Kenya, Mwanakwetu akashituka mbona yule mama sikumuona ndani ya ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara? Hapa amesaini kimiujiza?Hapo hapa kengele ya hatari ikalia  akilini mwa Mwanakwetu. 



 

“Lo salale ! Kumbe aliyenipa kadi ni labda mke wa mbunge huyo na siyo Mbunge mwenyewe na yule aliyepiga naye picha mara ya pili ndiye mbunge wa Afrika Mashariki mhe David Ole Sankok? Wamefanana labda mdogo wake.”

Mwanakwetu anataka kufedheheka leo hii! Mheshimiwa Davis Ole Sankok katika kitabu hiki cha wageni ni yule mhe aliyekuwa anaongea sana aliyevaa nguo za kijani na aliandika ujumbe huu.

“Nawashukuru kwa mapokezi mazuri kwanza kwa mchapalo wa jana ulikuwa mzuri sana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hoyeee…”

Mwanakwetu alifanya utafiti kidogo juu ya mhesimiwa David Ole Sankok, hapo hapo alibaini kuwa ni mbunge anayeheshimu sana mazingira na mara nyingi huvaa nguo za rangi ya kijani na  likimaanisha kuwa ni mtu anayethamini mno mazingira.

 

 

Huku mama ni mke wa mbunge ambaye awali anipa kadi na anaitwa Hellen Sankok wakiwa katika ndoa yao kwa miaka zaidi ya ishirini.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

“Kwa hakika nilivutiwa mno na muonekano wa Bi Hellen Sankok na huku nikitamani mama huyu wa kimaasai kutoka Kenya angebaki Tanzania na ahamie kwetu Mbagala Sabasaba Mbuyuni ,kumbe mama huyu ni mke wa mtu, itabidi nimtafute Bi Hellen Sankok siku nyingine kama anaye mdogo wake basi anifanyie mipango ili mdogo wake wa Kimaasai aje kuishi kwetu Tanzania akaogelee Mtoni Kijichi Mbagala Dar es Salaam. Mahaba na Helena Sankok Yalikatishwa Gafla Bini Vuu.”

Wakati haya yakiendelea katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, hali ya hewa ya Mji wa Musoma uliokumbatiwa na Ziwa Victoria mithili ya mtoto aliye  katika tumbo la mama mjamzito joto ni sentigredi 24 kunatarajiwa kunyesha mvua na unyenyevu ni wa asilimia 20 huku ujirani na mvua ni asilimia 75 na upepo ukivuma kwa KM11 kwa saa.


 

Mwanakwetu upo? Kumbuka

“Haya Mahaba Yaliyokatika Gafla Bini Vuu.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

NB Makala haya ya maandishi na Sauti yametayarishwa na Adeladius Makwega kwa heshima ya rafiki yake BRUCE AMANI mtangazaji wa Shirika la Utangazaji ya Ujerumani DW KISWAHILI ambapo ndugu Bruce Amani ana asili ya Kenya.

Bruce BinI Amani

 Bruce Amani.

 

 

 

 

 

 

 





















































 

0/Post a Comment/Comments