Lucas Masunzu- TABORA
Majira ya saa tano na ushehe, Jumatano ya Septemba 24, 2025, Shule ya Sekondari Urambo ilipata heshima ya kipekee yYakupokea ugeni kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA). Ugeni huo uliongozwa na Bi Neema Mpembela, Afisa Elimu Taaluma Sekondari wa Wilaya ya Urambo. Kumbukumbu zinadokeza kuwa kabla ya ugeni huh uje sekondari Urambo ilipokea ugeni kutoka TMDA mwa 2018/2019 hivyo kufanya ziara ya mwaka huu kuwa ya pili kwa taasisi hiyo katika kipindi cha miaka saba. Wageni waliowasili, akiwemo Bi Evelyne Makoye, Richard Mnzava, na Rogers walipokelewa kwa heshima na ukarimu mkubwa na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Urambo.
Baada ya kupokelewa rasmi, wageni walipata fursa ya kujihudhurisha kwenye kitabu cha wageni, hatua iliyoashiria mwanzo rasmi wa ugeni huo huku wakidokeza kuwa lengo la ziara hiyo ni kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa. Mmoja wa maafisa wa TMDA aliyepewa nafasi ya kuongoza mjadala, alijipambanua kwa umahiri mkubwa wa kujieleza, kiasi cha kuwavutia wanafunzi waliokuwa wamejawa na shauku ya kusikiliza na kujifunza.
Uwezo wake wa kuwasiliana kwa ufasaha uliwachangamsha wanafunzi, ambao walimshabihisha na Ali Kamwe, Afisa habari wa moja ya klabu maarufu za soka nchini Tanzania. Kwa pamoja, wanafunzi wakampachika jina la "Ali Kamwe wa TMDA", jambo lililozua vicheko na kufungua milango ya uhuru wa kushiriki kikamilifu katika mjadala. "Tumekuja hapa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya dawa. Tunaamini vijana kama ninyi ni nguzo muhimu ya mabadiliko katika jamii.
Mkielimika kuhusu matumizi sahihi ya dawa, mtakuwa mabalozi wazuri kwa familia zenu na kwa taifa kwa ujumla," alisisitiza mmoja wa maafisa kutoka TMDA. Katika maelezo yake, Afisa huyo alieleza baadhi ya changamoto zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa, madhara ya kiafya yatokanayo na matumizi ya dawa zilizoisha muda wake, pamoja na hatari ya kutumia dawa bila vipimo sahihi. Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Urambo walionyesha ari, hamasa na utayari mkubwa wa kujifunza, huku wakishiriki kikamilifu kwa kuuliza msururu wa maswali. Jumla ya maswali ishirini (20) yaliulizwa na kujibiwa kwa kina na maafisa wa TMDA huku ndugu Rogers alionekana kuwa kinara wa kujibu maswali hayo ambayo urambo sekondari waliitwanga moja kwa moja TMDA.
Uongozi wa shule ulitoa shukrani za dhati kwa wageni hao kwa kufika shuleni hapo na kuwapa wanafunzi elimu muhimu. Aidha, walisisitiza kuwa elimu hiyo si tu ya msaada kwa wanafunzi, bali ina mchango mkubwa katika kutokomeza matumizi holela ya dawa katika jamii nzima. Tunaamini kuwa elimu hii mliyoitoa itakuwa mbegu njema itakayoota katika mioyo ya vijana hawa na kuwa na matokeo chanya kwa jamii. Nakutakia siku njema.
0762665595

Post a Comment