Adeladius Makwega-Sirari Tarime MARA.
Wafanyabiashara ndogo ndogo Wilayani Tarime, Septemba 23, 2025 wameilalamikia Mahakama ya Mwanzo Sirari kwa kuwalipisha fedha bila ya kuwapa control number na jambo hili kusababisha kushindwa kukamilisha taratibu za kupata mikopo inayotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa taratibu mbalimbali..
“Jambo hili ni kero, linatunyima amani, hapo yupo mtumishi wa mahakama ya mwanzo na kila tunapomwambia, anasema nendeni popote pale tunalipishwa kiasi kati ya shilingi 30,000/- hadi 35,000/- kulipia fomu moja tu basi iwe pesa ya serikali sawa lakini ni pesa ya mfukoni mwake tu.”
Kwa utafiti wa mwandishi wa makala haya mjasiriamali anapotaka kupata mkopo hupitia katika taasisi za kibenki na hupewa fomu maalumu ya kuupata mkopo huo, fomu hii inahitaji hakimu ama wakili kuthibitisha kuwa mwombaji huyo ndiye yeye. hapa ndipo ugomvi wa wafanyabisahara wa Sirari na Mahakama unaanza.
“Tunakwenada mahakama siyo kwa kupenda, hoja ni moja tu mahakama ilipaswa kuwa sehemu salama kuliko kwa mawakili binafsi, hivyo ndivyo tulivyozoea. Mahakama ya Mwanzao ziko angalau kila baada ya umbali fulanim, siyo mawakili. Je Mawakili Binafsi Mbadala wa Mahakama?”
Katika kikao hiki kilichohudhuliwa na wafanyabiashara karibu 700 katika ukumbi wa Kanisa Katoliki la Malaika Gabrieli, Parokia ya Sirari Jimbo Katoliki la Musoma, malalamiko haya yalilindima bila woga, Mkuu wa Wilaya ya Tarime akiongoza kikao hiki kwa haki, akijibu hoja hii Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Gowele alisema;
“Ni kweli Mahakama ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mihimili miwili tofauti lakini nitaongea na Hakimu Mfawidhi juu ya jambo hili la mahakama ya Mwanzo Sirari na suala hili litafanyiwa kazi haraka.”
Akizungumza katika kikao hiki, Afisa Vijana Mkoa wa Mara Fidel Balagaye alaisema kuwa anawashukuru wananchi wa Tarime kujitokeza katika kikao hiki alisema serikali imefanya kazi kubwa kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata mikopo yenye masharti nafuu.
Katika kikao hiki Mwanakwetu alibaini mambo kadhaa;
“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeipatia Benki ya NMB karibu Bilioni 20 ili wakopeshwe wajasiriamali mbalimbali nchini kwa riba ya asilimia saba, huku asilimia tano zikibaki kwa taasisi inayowakopesha wafanyabiashara hao, yaani NMB nayo asilimia mbili ya riba inarudi Serikali Kuu.
Hadi Septemba 2025 kwa Mkoa wa Mara wafanyabiashara ndogo ndogo 217 wamesanufahika na fedha hizo ambapo shilingi milioni 380 na ushehe zimetolewa.
Takwimu zinagonga kengele yake kwa sauti ya juu kuwa wafanyabiashara 5037 wamejisali na huku wafanyabishara 1665 tu ndiyo wenye vitambulisho na sifa ya kukopeshwa. Kwa Wilaya ya Tarime hadi Septemba 2025 imewakopeshwa shilingi milioni 124 ikiwa ndiyo halmashauri iliyonufahika zaidi na pesa hizi.”
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa Halmashauri zenye mapato makubwa nchini ambapo tangu mwaka wa 2021 hadi 2025 mapato yake yamepanda kutoka Bilioni tano na ushehe hadi bilioni 19 na ushehe huku maoteo kwa mwaka wa fedha wa 2025/ 2026 kuwa ni karibu bilioni 18 na kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025 Halmashauari ya Wilaya ya Tarime ilitenga milioni 754 kama mapato ya mikopo ya asilimia kumi ya mapato yake ya ndani ya akina yakhe.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Kwa hakika kikao cha wafanyabishara ndogondngo wilaya ya Tarime kimefana sana, huku Mkuu wa Wilaya ya Tarime akikiongoza vizuri sana.
Mwanakwetu binafsi anaona kuwa Mahakama ya Tanzania inapaswa kutambua wajibu wake kwa Watanzania wa kutoa huduma, suala la kusainiwa fomu wananchi ni haki yao na haki yao na lnapaswa kufanya na mahakama zetu kwa gharama nafuu isiyozidi shilingi 5,000/ kwa fomu moja, maana Mahakama ya Tanzania inaendesha kwa kodi za Watanznia, Jaji Mkuu wa Tanzania wa sasa atambue hili.
Mwanakwetu kwa makala haya anasema wazi kuwa mahakama hawezi kukwepa jukumu hili, japokuwa mawakili binafsi wanatusainiwa na kutugongea mihuri mara nyingi sana na tunaheshimu mchango wao lakini mawakili hawawezi kuwa mbadala wa Mahakama ya Tanzania na hili pia Jaji Mkuu wa sasa atambue pia.
Mwanakwetu anaamini kuwa hata Watanzania wanapolalamikia kulipishwa gharama katika mahakama kitendo hiki kinaonesha Watanzania wanatambua wajabu wa Mahakama ya Tanzania kwao, Jaji Mkuu anaweza kuamua hata fomu hizi za mikopo kugongewa mihuri bure, hili litaleta heshima ya Mahakama Ya Tanzania kwa wananchi wao.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Mawakili Mbadala wa Mahakama ya Tanzania.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment