Adeladius Makwega-MBAGALA
Ilikuwa ni majira ya asubuhi ya Septemba 20, 2025 ujumbe unaingia katika simu yangu.
“MwAnAkWeTu una taarifa kuwa Baba Askofu Stephern Munga amefariki dunia?”
Nilijibu hapana, hapo hapo nilitaka kuipiga simu ya Baba Askofu Munga lakini nikaona haina maana na hili lilikuwa wazo la mtu aliyetoka usingizini-Wazo la Kitomaso, sekunde chache pale nilipotazama Mitandao ya Kijamii taarifa hizo zilishatapakaa.
Nikasema Moyoni;
“Kweli, Baba Askofu Stephern Munga Hatunaye!”
Kwa hakika MwAnAkWeTu nimesikitishwa na msiba huu, kichwa changu kikiwa na mengi ya kuyaeleza juu ya maisha ya ndugu yetu Stephern Munga lakini nashinda nianzie na kumalizia wapi?
Jambo kubwa na la msingi ambalo nikiwa na majonzi huku nikiwa na furaha kubwa , kubwa moyoni mwangu binafsi, binafsi kwa kuona ya sehemu ya maisha yako ambapo ninaweza kusimama kifua mbele ya kuyasimuli mambo mengi kwa kipindi cha karibu miaka 20.
Kwa hakika siku nzima ya Septemba 20, 2025 niliitumia kuyakumbuka yote hayo na kukata shauri kuwa lazima niyaseme machache hadharani, kwa kuwa binadamu tumejawa na Utomasi kama vile mimi binafsi nilivyokumbwa na Utomaso wa kuamini kuwa Baba Askofu Stephern Munga umefariki dunia baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa rafiki yangu Simon Ikoja.
Kwa hakika akili yangu imeyakumbuka mengi baada ya taarifa hii ya tanzia.Kwa kuogopa kuwachosha wasomaji naomba niyaseme matatu tu;
Kwanza nimekukumbuka ulivyoniita pale Ofisi ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya DKMs juu ya changamoto za kisiasa Wilayani Lushoto mwaka 2017/2018. Nakumbuka nilikwambia maneno haya
“… tatizo la CCM, wanasiasa wake wengi ni wafanyabiashara, wapo siasani huku wakiwa na mambo haya makubwa mawili biashara na siasa. Baba hilo ndilo changamoto kubwa… ufanyaji wa siasa siasa safi unapwaya na hapo ndipo Wakurugenzi wengi Watendaji wanakuwa kafara au kuchagua kukukubaliana kila analolitaka mwanasaisa kwenye eneo husika liwe… usipofanya hivyo wanakwambia huyu hana mahusiano mazuri na wenzake. Mahusiano mazuri yafuate misingi ya haki na kuondoa upendeleo kwa baadhi ya watu.”
Tulizungumza mengi Baba Askofu Munga huku maelezo yako yalikuwa yakunitia moyo sana;
“… fanya kazi tu , usirudi nyuma, haya mambo yapo, si katika siasa tu bali hata katika maeneo mengine, wewe kumbuka kufanya kazi, usirudi nyuma, usikate tamaa, iko siku wao wenyewe watakumbuka…”
Nakumbuka nilikuwa natoka ofisini kwako nikala chakula cha mchana katika mkahawa wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki -Lushoto Mjini na nilipotaka kulipa chakula changu ukasema unalipa wewe na kweli ulifanya hivyo.
Je hilo tu? la hasha, Februari 2024 nilikamatwa na Polisi Dodoma kwa tuhuma za makala zangu juu ya Kadhia kadhaa wanavyotendewa watoto wetu wanaosoma Chuo Kikuu cha Dodoma.
Vifaa vyangu vyote vya kihabari walichukua, pamoja na simu zangu. Nilipokuwa chini ya Ulinzi nilimuomba ndugu yangu Mtweve Kayanda, mwanafunzi wangu niliyefundisha sekondari na mtumishi mwenzagu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo wakati huo awasiliane na wewe (Baba Askofu Stephern Munga)
“Mteve Kayanda wasiliana na Baba Askofu Stephern Munga mueleze kilichotokea kama kilivyo na mtumie makala zote 32, mwambie Adeladius Makwega amenituma nikujulishe hilo.”
Kwa hakika ulifanya kazi kubwa ukishirikiana na Maaskofu Wengine wa Makanisa ya Tanzania (Mungu Awabariki).
Huku nilipotoka nilikuuliza Kanisa Katoliki lilifanya chochote? Ulinijibu hatua zote za mchango wa Kanisa Katoliki ambapo awali hilo sikulifahamu. Huku Kiongozi mkubwa wa Parokia yangu ya zamani Chamwino Ikulu alinitafuta na kufuatilia kilichotokea na kilichokuwa kinaendelea hatua kwa hatua.
Tatu na mwisho Baba Askofu Munga ulikuwa na desturi moja nzuri ambapo binafsi sikuhifahamu mapema sana lakini baada ya miaka mitatu nikagundua hilo;
“Kila siku ya IJumaa Kuu ya kila Mwaka ulikuwa unanitumie ujumbe wako wa Ijumaa Kuu katika simu yangu ya mkononi, baadaye nilipobaini hilo nikawa nahifadhi ujumbe wako vizuri sana ili siku nije kuandikia makala lakini lakini nina masikitiko simu hiyo kwa leo siko nayo bado wanayo vijana waleeee… waliyoichukua wakati uleee lakini ningekuwa nayo leo hii ningeupachika ujumbe mmojawpao wa Ijumaa Kuu uliyonitumia wakati wa uhai wako.”
Kwa leo sitaki kusema maneno mengi, naomba wale niliyowataja katika makala haya ambao wapo hai wanisamehe lakini kubwa ni huzuni bini masikitiko kutoka na msiba wa mtu niliyemfahamu miaka mingi ambapo sehemu ya maisha yake imenigusa.
Pole kwa Dkt. Aneth Munga, pole kwa watoto na wajukuu wote waliotawanyika ulimwenguni, msamilie Baba Askofu Sebastian Kolowa , Msamilie rafiki yako na ndugu yetu Benjamin Mkapa na msalimie Baba Askofu Joseph Jali.
“Ntambo Ntana Askofu Munga.”
0717649257
Post a Comment