MWENDO NYIMBO ZA KUPUNGA MASHETANI

 



Adeladius Makwega-MBAGALA.

“Nyinyi Wakristo hamna maana kabisa, yaani mnashindwa kumtunza mchungaji wenu, hadi anajinyonga! Kisa ugumu wa maisha? Mbona nyinyi mambo yenu mazuri! Wengine mnaendesha magari! Wako Wakristo wangapi hapa Mbagala wenye uwezo? Msio marofa mnamiliki maekari na maekari ya ardhi ? Isitoshe mbona kuna watumishi wengi wa umma hapa Mbagala ni Wakristo ? Kwanini hamkumtunza mchungaji wenu hadi anaaamua kujionyonga? Kisa ugumu wa maisha?”

Wakristo tunasimangwa msibani baada ya mchungaji wa Kanisa la Anglikana Mbagala mwanzoni mwa miaka 1990 kujinyonga nyumbani kwake Mbagala kwa Mangaya , hoja ikiwa ugumu wa maisha, hilo lilijulikana baada ya mchungaji husika kuacha ujumbe katika meza yake chumbani kwake.


 

Mjadala msibani unaendelea,

“Hapa yupo Jaji Kimicha ni mtu mwenye ardhi kubwa kuliko mtu yoyote wa Mbagala, yeye tu kama angeamua kumuhudumia mchungaji wake asingali jinyonga, hapa bado Wakristo Wadogo akina Makwega akina Mpelumbe, akina Linje ile ni familia kubwa ya askari mstaafu na wengine kibao.”

Msomaji wangu masimango yanaendelea msibani, Wakristo kimya, watani wa Wagogo wanatamba Mbagala kwa Mangaya jirani na Masjidi Sinina, nyumba kama ya saba hivi ukivuka Barabara ambapo hapa ndipo mchungaji huyu alikuwa amepanga, yeye mkewe na wanawe kadhaa.


 

Msomaji wanangu tambua kuwa Mwanakwetu (Adeladius Makwega) yu msibani na rafiki yake mpembwa Godwin Mpelumbe sasa Mkurugenzi wa Takwimu nchini ambapo tumekwenda kuzika mchungaji aliyejinyoga kutokana ugumu wa maisha.

Mchungaji huyu alikuwa mtu mtulivu sana . mpole, mkimya huku siku za huduma za kiroho anakwenda kusalisha Waanglikana katika mojawapo ya darasa pale Shule ya Msingi Mbagala, siku zingine mchungaji huyu alikuwa akienda machinjio ya ng’ombe Mbagala kwa Mpili ambapo alikuwa akifanya shughuli zake.

Mchungaji huyu wa Kanisa la Anglikana alikuwa Mgogo wa Dodoma, huku akihudumia Wakristo wa Mbagala nzima ambapo walikuwa hawana kanisa bali wanasali Shule ya Msingi Mbagala tu. Huyu mchungaji alikuwa na watoto wake vijana wakubwa kwa Mwanakwetu na Mpelumbe ambao walimaliza Shule ya Msingi Mbagala mwaka 1987 na 1988 na mmojawapo alikuwa anaitwa BOAZ.


 

Mjadala wa masimango ulikuwa mzuri sana Mwanakwetu akijitetea kuwa yeye anasali katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Antony wa Padua Mbagala,Godwin Mpelumbe ambaye alikuwa mwanakwaya wa kanisa hilo kimya, huku jamaa hawa wanarusha maneno wanasema,

“Hakuna nyinyi wote siyo ni Wakristo? Nyinyi nyote ni mnamtaje Yesu Bini Mariamu? Mchungaji wenu huyu hapa kalala sasa nendeni mkamle nyama.”

Msomaji wangu nikuongezee na jambo lingine, wakati huo Kanisa Katoliki lilikuwepo Mbagala Misheni, ukitoka hapo kuelekea Kibiti Kanisa lingine la kujengwa imara utalikuta Kilimahewa mbele ya Kimanzichana, huu ni umbali kama wa KM 100. Watumishi wa umma Wakristo ikifika jumapili wanakusanya darasani wanasali.

Ninachokumbuka Mkristo ukisikia wenzako wanaimba nyimbo za kumtaja Yesu, wewe unaingia huko kumuabudu Bwana Yesu bila kujali ni dhehebu lako au laa.

Wakati huo eneo lote la Mbagala majira ya usiku ni milio ya ngoma za kupunga mashetani, ngoma kama Mbugi Mthimini na kadhalika, huku usiku kucha tangu saa 4 usiku hadi 11 ni kelele za manyanga na watu wakipandisha mashetani.

Msomaji wangu kumbuka tuko msibani, kweli mchungaji yule alizikwa kimya kimya kisha na sisi kuendelea maisha yetu wa Mbagala.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika hali hii ya madhehebu ya Kikristo kwa sasa unaweza kuiona kama mazingira ya dhehebu lako yamewekwa vizuri, kanisa limejengwa na waamini mnakwenda kuabudu unaweza kuona kama utani vile. Mtu ambaye siyo Mkristo anapowatazama Wakristo hayaoni yale madhehebu yetu, yeye anauona Ukristo ambalo hilo ni jambo sahihi sana lakini cha kustaajabu Wakristo wenyewe tunajiona katika ile migawanyiko yetu ya kimadhehebu na ndiyo maana katika kisa hiki Wakristo wote wa Mbagala tulilalamikiwa kwa nini hatukumtunza mchungaji wetu, hadi anajinyonga kwa ugumu wa maisha?

Kwa sasa hali ya Ukristo ni nzuri, yamejengwa makanisa tele, hatua mbili unasikia Yesu anatajwa, huku utaisikia kengele, kule utaisikia mapambio, hapa kwaya inafanya mazoezi na pale watoto wa Sunday School wanacheza.

Huku na kule Makanisa yakimiliki taasisi kama vile shule , zahanati na kadhalika, haya ni maendeleo.


 

Habari za zamani, zile za kelele za Mbagala Mwendo wa Nyimbo za Kupunga Mashetani zimepungua. Kwa wale Wakristo wenye nafasi Serikalini mjitahidi sana kutimiza wajibu wenu kwa kanisa bila kujali dhehebu lako,tujiulize Tanzania ina mawaziri wangapi Wakristo? Tanzania ina wabunge Wangapi Wakristo? Kweli hili jambo la Kanisa la Dkt. Gwajima limewashinda?

Au Shabaha yenu kutaka kuwarejesha Watanzania wakapunge Mashetani? Jamani eee msifungie makanisa yetu, muache mara moja , tulikotoka ni mbali.

Simulizi hii inatayarishwa na Mwanakwetu kwa heshima zote kwa Kanisa la Tanzania, hii ni mojawapo ya hatua Kanisa la Tanzania limepitia, najua kwa Mbagala wale Waangikana wengi ni wageni lakini mkiuliza Ukoo wa Mpelumbe, Ukoo wa Jaji Kimicha na hata Ukoo wa Linje wataeleza kwa kina tukio hili.

 Huku madhehebu mengine ya Kikristo lipo la kujifunza katika kisa hiki cha kweli.


 

Mwanakwetu Upo?

Kumbuka

“Mwendo Nyimbo za Kupunga Mashetani.”

Nakutakia siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

NB picha zote ni za maktaba isipokuwa Picha ya Askofu Dkt J Gwajima.




 

0/Post a Comment/Comments