Adeladius Makwega-MBAGALA.
Mwanakwetu siku hii alifanya kazi zake vizuri, kisha kile kiongeza sauti masikioni mwake kikaharibika, lo salale, hivyo basi akashindwa kuendelea na kazi, akatoka zake kuelekea manunuzini ya kifaa hiki, akiwa anatoka tu gafla mlangoni akakutana na ndugu yake mmoja, akiuliza MwAnAkWeTu unakwenda wapi?
“Nakwenda kununua earphone zangu maana zimeharibika na siwezi kuendelea na kazi.”
Jamaa akasema, kaka subiri kaka! Tuongee kitu, ndugu huyu akaweka mizigo yake na kutoka kuambatana na MwAnAkWeTu, wakiwa wanatoka wakaongea jambo fulani kisha jamaa wakawa wanaagana, huyu ndugu akasema maneno haya,
“Kaka mimi nakwenda kula chakula cha mchana, kwani wewe unakula (ga) wapi?”
MwAnAkWeTu akajibu , jamaa huyu muungwana sana akasema kaka leo tupite njia hii, katika maisha yako usipende kupitia njia moja, badilishabadisha njia.
Wakatembea kwa miguu na jamaa huyu akafika mkahawani kula, nayeye MwAnAkWeTu aliyeshiba kande na supu ya asubuhi ya siku hii akaenda kununua kifaa kile kichoharibika, akafika dukani akakutana na bei ya shilingi 3000/= na vingine vya shilingi 20,000/= . MwAnAkWeTU akanunua vya shilingi 3,000/= akalipa 10,000/- kisha kurejeshewa shilingi 7,000/= maana MwAnAkWeTu siyo BWENYENYE, hapa hapa akaanza kurudi kupitia mkahawani akutane na yule ndugu yake ili warudi walipotoka pamoja.
Kweli MwAnAkWeTu akafika mkahawani na kukutana na huyu ndugu yake anamalizia mfupa wa mwisho wa nyama katika sahani yake bilauri ya mtindi kando. MwAnAkWeTu akatoa salaam kwa huyu ndugu kando yaani siyo yule jamaa yake maana mezani walikuwa wawili.
“Kaka kweli umewahi, maana nimeshamaliza kula, tunaondoka sasa hivi.”
Jamaa kando ya huyu ndugu wa MwAnAkWeTu akasema jamani eee mbona mmevaa mashati meusi, pamoja? Maneno haya yakawasitua MwAnAkWeTu na huyu ndugu yake na kusema kweli kumbe kweli. Hapa hapa MwAnAkWeTu akavuta kiti na kukaa katika meza hii mkahawani ambayo ilikuwa sasa na jamaa watatu. Huyu ndugu kavaa shati jeupe na suruali nyeusi, lakini hawa jamaa wawili yaani MwAnAkWeTu na nduguye wamevaa mashati meusi na suruali zinazotafautiana.
Jamaa aliyesema juu ya mashati meusi, akasema ebu hesabuni hapa mkahawani watu wangapi wamevaa mashati na blauzi nyeusi? Huu mkahawa ulikuwa na watu kama 20 karibu watu 15 wamevaa mashati na blauzi nyeusi , huku watu watano tu walivaa nguo za juu za rangi nyingine akawamo huyu muibua mada na jamaa huyu kando muibua mada akasema,
“Nyinyi mna mambo sana, inawezekana mnamuunga mkono Balozi Humphrey Polepole, maana Watanzania wana mambo sana.”
Tukawa tunacheka huku tunasimama ili turudi tulipotoka , hawa akina mama na akina dada kando wakawa wanafuraha sana wakisema,
“Ahhhh tunawaona wakaka na wababa mpo na MwAnAkWeTU! Msalimieni sana MwAnAkWeTu !”
Hawa jamaa wanajibu huku MwAnAkWeTu yu kimya, akitafakari ile hoja ya waliovaa nguo nyeusi wanamuonga mkono Balozi Polepole? Tukiwa tunatoka hapo kurudi tulipotoka nguo za rangi nyeusi zimetamalaki njiani hesabu inaendelea kufanyika, huyu kavaa blazi, huyu kavaa fulani na yule kavaa shati la mikono mifupi, mwingine la mikono mirefu pia wapo waliovaa mikono mieusi.
Huku huyu jamaa akawa anasema angalieni sana, isiwe ikawa kuna chama kipya kimeanzishwa sare zao nguo nyeusi maana Balozi Polepole alipokuwa akizungumza kwa mara ya kwanza alivaa fulani ya rangi nyeusi, ile ina maana kubwa, ile Fulani ina maana sana.
MwAnAkWeTu na ndugu zake hawa walifika waliponuia , kisha kila mmoja kushika 50 zake.
MwAnAkWeTu anasema nini siku ya leo?
“Maana ya rangi nyeusi ina sura nyingi, ikijumuisha maana chanya na hasi. Inaweza kuashiria nguvu, ustadi, na hali ya juu, lakini pia kifo, maombolezo, na uovu.
Rangi nyeusi inaweza kuchochea hisia za fumbo fulani, giza, na hata kulikataa jambo fulani. Kwa ujumla wake maana ya rangi nyeusi hubadilika kulingana na hali na tafsiri ya mtu binafsi, hii ni rangi yenye nguvu inayoweza kuchochea hisia na maana nyingi tofauti.”
MwAnAkWeTu anapohitimisha makala haya bado anajiuliza je watu hawa aliypkutana nao wakiwa wamevalia blauzi na fulana nyeusi walipanga kufanya hivyo? Jibu lake hapana kila mmoja alivaa hivyo akitoka nyumbani kwake, akiwa na hisia yake, wengine hatuna sabuni, wengine maji hayatoki, wengine kauka nikuvae,wengine wamefiwa na wapendwa wao, lakini lakini hoja inakuja kwa yule anayewatazama kama huyu jamaa alivyowatazama MwAnAkWeTu na nduguye.
Swali linabaki je huvaaji wa fulani nyeusi ya Balozi Polepole siku anazungumza na Watanzania kwa mara ya kwanza, mara baada ya kubwaga manyanga ya Ubalozi wa Tanzania nchini Cuba, je una maana yoyote kwa Watanzania? Je jambo hili limevutia hisia za Watanzania katika maisha yao kwa sasa ? Je kwa kiasi gani?Au Balozi Polepole katwanga maji kati kinu. Hapana hapana Balozi Polepole katimiza wajibu wake, katoa sadaka kazi yake, wewe jeee? KIla mmoja atimize wajibu wake. Kwanini Balozi Polepole siku ile akuvalia nguo za rangi nyingine?
Kwa leo inatosha sana maana kesho nayo ni siku.
MwAnAkWeTu upo?
Kumbuka
“FULANI NYEUSI YA BALOZI POLEPOLE .”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment