Adeladius Makwega-Musoma MARA
Ni majira ya asubuhi ya Jumatano ya Juni 25, 2025 Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi anaupokea ugeni wa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Afande IGP Camilius Wambura na kumkaribisha ofisini kwake kando ya Mlima Mkendo uliofunikwa na miti yenye chanikiwi mlima mzima.
Kanali Mtambi anamuongoza Afande IGP Wambura ofisini kwake na kufanya neya mazungumzo ya karibu dakika 38 katika Ofisi hii iliyoegemea Mlima Mkendo ikiwa jirani na Mwalo wa Ziwa Victoria.
Afande IGP Wambura akiwa amevalia sare za jeshi lake analoliongoza, akionekana kuwa askari mchangamfu na mazungumzo yake yakiwa ni vicheko vya hapa na pale . Hili likitoa tafsiri nzuri kwa anayemtazama kwa umakini Afande IGP Wambura.
Kwanza kitabu cha wageni kinasainiwa kisha kuanza mazungumzo haya yaliyokuwa yakiutazama Usalama wa Mkoa wa Mara kwa kina.
Akifungua mazungumzo haya, Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Mtambi alizungumzia ushirikiano wake anaupata kutoka Kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara, huku akigusia juu ya kazi nzuri inayofanywa na Polisi Jamii.
“Niliwaagiza wezangu wafanye uchambuzi wa tabia fulani fulani na kwanini kunakuwa na hali fulani kwa vipindi fulani? Hili limetusaidia sana kujua hali ilivyo na ndiyo maana sasa tumeweza kukabiliana na changamoto zote zinazotokea na tunafanya kazi vizuri.”
Pia Kanali Mtambi alitumia fursa hii kumkaribisha Afande IGP Mkoani Mara.
Kwa upande wake Afande IGP Wambura kwanza alipuliza mbiu yake ya mgambo juu ya Ukatili wa Kijinsia.
“Kwa upande wetu, hivi sasa vijana wangu wa Jeshi la Polisi Tanzania wamepata mafunzo maeneo mbalimbali ulimwenguni, wamezunguka mataifa kadhaa kuona wenzetu wanapambana vipi na hali hii. Kwa sasa ukatili ni sehemu ya uhalifu mkubwa duniani, Jeshi la Polisi Tanzania tunashirikiana na taasisi zingine tunapambana na hali hii vizuri, nia ni kubadilisha akili za watoto wadogo na vijana, shabaha ni kuukataa ukatili huu. Wenzetu huko wameshuka hadi katika ngazi ya familia na sisi kwa sasa tunafikia huko. Kwa sasa tunaweza kuona suala la Ukatili wa Kijinsia kama umekuwa mkubwa lakini hapana kwa kuwa sasa watu wanayasema sana mambo haya na yanafanyiwa kazi na kwa sasa ukatili wa kijinsia unapungua na ninao mwanga mkubwa wa kuwa na Tanzania Isiyo na ukatili wa Kijinsia.”
Akizungumza kukamilisha mazungumzo haya ya dakika karibu arubaini Afande IGP Wambura aliupongeza sana Mkoa wa Mara kwa hali iliyofikia kuleta utulivu, huku akisema kuwa hali ya usalama awali kwa Mkoa wa Mara ilikuwa eneo hatari duniani lakini sasa hali ni nzuri.
Katika kikao hiki cha ndani pia kilihudhuriwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mara ndugu Gerald Msabila Kusaya na viongozi wengine wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara .
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanya kutoka Ofisi ya Mkoa wa Mara zinadokeza kuwa ujio huu wa IGP Camilius Wambura ni safari yake ya pili kuutembelea Mkoa wa Mara wakati Mkuu wa Mkoa ni Kanali Evans Alfred Mtambi.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Ukatili wa Kijinsia Unapungua.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257

Post a Comment