Adeladius Makwega-MBAGALA
“Bila ya kuathiri sheria zinazohusika za Jamhuri ya Muungano, kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari ya mtu ya binafsi, nahughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
Juni 16, 2025 Mwanakwetu anaipitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ile ya 19 ambapo kipengele cha pili anakutana na maelezo hayo. Akilini mwa Mwanakwetu zinamjia sauti za waamini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima wakipiga kelele, wakiongea na polisi huku wakiwa na mabango wakilalamikia kuminywa kwa uhuru wao wa kuabudu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, taifa aenye Katiba yake, yenye maneno hayo.
Mwanakwetu akawa anajiuliza shida ni Katiba kusema hivyo au shida ni ya wafanya maamuzi kutokutaka na kutokutoa nafasi ya pande kadhaa kusikilizana? Au huko kote ni kuminya uhuru wa kujieleza?
“Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombochochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wamawasiliano yake kutoingiliwa kati. Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi.”
Mwanakwetu akakumbuka ibara mbili za Katiba ya Jmahuri ya Muungano wa Tanzania ile ya 18 na hii ya 19 kwa wakati mmoja.
Mwanakwetu mwingi wa simulizi akiwa na Katiba hiyo mkononi mwake alikumbuka kisa kimoja cha kweli kabisa.
“Kwa hakika migogoro ni jambo la kawaida kwa binadamu wanapokuwa pamoja. Kwa hakika katika wilaya nyingi migogoro inaweza kuwa baina ya Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala wake, hapa chanzo kikubwa inaweza kuwa ni mahusiano mabaya baina yao hasa juu ya fedha.
Mkuu wa Wilaya anaweza kuomba fedha na pengine anaweza kunyimwa kulingana na fedha ilivyo kidogo, nayeye kuona kuwa kama anafanyiwa mizengwe,
‘Mimi ni mteule wa Rais mnanyimaje fedha hizo?’
Katibu Tawala yeye ni mtu wa utaratibu, mara nyingi wako makini kukwepa hoja za ukaguzi, haya mambo yanatokea sana. Mgogoro wa pili unaweza ukawa baina ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji na hoja ile ile ya maslahi, maana pesa ni uchawi wa kizungu.”
Katika Wilaya moja nchini Tanzania kuna wakati fulani kulikuwa na mgogoro baina ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji.
Kwa hiyo siku ya leo makala haya yanajikita katika mgogoro baina ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kuhusianisha na hali ya siasa ya sasa ya Tanzania.
Mgogoro huu ulikuwa mkubwa na jambo hili kusababisha Mkurugenzi Mtendaji kuanza kuwekewa mitego, vihunzi na Vikwazo tele na mashauri kadhaa. Mwisho wa siku ikafikia hatua kutaka kumpachikia shauri.
Panapokuwa na ugomvi wowote katika wilaya baina na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi, kiongozi ambaye lazima mgogoro huu atashindwa ni Mkurugenzi Mtendaji , maana Mkuu wa Wilaya ameshika mpini na huku Mkurugenzi Mtendaji kashika makali.
Mkurugenzi Mtendaji maji yakawa ya shingo anafanya nini kunasuka mtegoni?
“Wakati huo Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Taifa alikuwa Balozi Humphrey Polepole. Mkurugenzi Mtendaji akampigia simu Balozi Polepole akamuueleza namna hali ilivyo kwa kina, Balozi Polepole akalipokea aliloambiwa vizuri na kisha akazungumza na watu wa Chama cha Mapinduzi (CCM)wilaya husika usiku huo huo, akapata picha halisi.
Kisha Balozi akatoa ushauri kwa Mkurugenzi Mtendaji usiku huo huo kuwa amtafute Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wamtafute Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati ni huyu huyu Waziri wa Fedha 2025 Mhe Mwigulu Nchemba wajue yupo wapi na wamueleze kinachoondelea ili yeye aingilie kati kulitatua hili.
Kweli Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM Bungeni akawasiliana na Mhe. Mwigulu na yeye kujibu kuwa yu Dar es Salaam. Safari ilifungwa hadi Dar es Salaam na kumuona Mh Mwigulu na majibu ya Mhe. Mwigulu akasema ngoja nione.”
Mh Mwigulu Nchemba hakujua kuwa safari hiyo iliandaliwa kwa ushauri wa Mhe. Polepole. Huku Mkuu wa Wilaya husika hajui haya yote yanayofanyika na mwisho wa siku suala hilo lilikwisha kwa msaada wa Balozi Polepole na Mhe. Mwigulu Nchemba. Mkuu wa wilaya na Mkurigenzi Mtendaji waliishi kidugu na vizuri mno baada ya changamoto hii kutatuliwa.
Balozi Polepole akisema maneno haya,
“Nyinyi mpo Wilayani pamoja, kila mmoja ametokwa kwake, nyinyi hapo Wilaya ni wageni tu, lazima mkae pamoja ,huku mkizungumza mambo yote, ili serikali iyafikie malengo yake, CCM iyafikie malengo yake, nyinyi mnyafikie malengo yenu na wananchi wayafikie malengo yenu, ishini kidugu , kuweni makini.”
Kwa nini Mwanakwetu anasimulia kisa hiki?
Kwa hakika shabaha ya kisa hiki ni kuonesha kuwa CCM kama inaamua kuutatua mgogoro wowote ule inaweza.
Hata hili la Baba Askofu Dkt. Josephart Gwajima na Kanisa lake ya Ufufuo na Uzima linaweza kutatulia vizuri kwa kuwa kilichosemwa na Baba Askofu Dkt. Gwajima ndiyo ukweli wenyewe, ukweli mchungu na kichungu huonjwa, maana watu wanauwawa na hakuna majibu lakini suala la kufungwa Kanisa la Ufufuo na Uzima limeongeza jambo lingine la pili juu yake la kuingilia Uhuru wa Kuabudu kama inavyoonekana hivi sasa waamini wa Kanisa hili wanavyotanga tanga je Tanzania inataka kuwa Nicaragua/ Au tuwe Afghanistani? Awali hoja ilikuwa ni matukio ya udhalilishaji, utwekaji na mauwaji.
“Kwa sasa taarifa za kidunia zinadokeza kuwa yapo mataifa kadhaa ambayo yananyima uhuru wa kuabudu kwa Wakristo mathalani Libya, Afghanstan, Somalia na Korea ya Kusini. Taarifa zinadokeza kuwa miongoni mwa dini na madhehebu mengine yanayokumbwa na Changamoto hizi ni Mashahidi wa Yehova ambayo wanajitambulisha kuwa na wao ni Wakristo huku wakipingana na baadhi ya mafundisho ya Ukristo. Dhehebu lingine ni Bahai ambao wanahubiri umoja kwa binadamu na wao pia wamekumbwa na hali hii na pia Ahmadia na wao wanakumbwa na changamoto hii ambao ni sehemu ya Dini ya Kiisilamu.”
Kwa Kanisa Katoliki hakuna taifa ambalo limepiga marufuku lakini historia inadokeza kuwa huko Japan Karne ya 16 Ukristo wote ulipigwa marufuku. Hata wakati wa Vita vya Pili vya Dunia mataifa kama vile Ukraine, Lithunia, Albania na Yugoslavia waliminywa uhuru wa kuabudu. Nako huku Norway ilipiga marufuku kabisa dini ya Kiyahudi na Ukatoliki hasa dhehebu ya Ujesweti. Huku taifa ambalo linarekodiwa kwa kuwabana viongozi wa dini hasa Wakatoliki ni Nicaragua Mapadri na hadi Maaskofu waliwahi kufungwa hadi miaka 26 Gerezani.
Hii ndiyo hali ya Uhuru wa Kuabudu duniani.
Kwa nafasi ya Askofu Dkt Josephart Gwajima, yeye kama Mjumbe wa Mkutano Mkuu na Mjumbe wa Halmashauri wa CCM Taifa, vikao viwili vya juu vya CCM, je Serikali inashindwa kuzungumza na Baba Askofu Dkt .Gwajima? Je CCM inashindwa kuyachukua maneno yaliyozungumzwa na Askofu Dkt Gwajima na kuyafanyia kazi?
Je hali inakuwaje kama Mtanzania wa kawaida anaingia katika changamoto kama hizi? Je Viongozi wa CCM wanapokuwa pamoja maana yake hawazungumzii? Zaidi ya kujadili ajenda rasmi zinazoingizwa katika vikao? Je kama CCM inashindwa kuzungumza na Mjumbe wake wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa Je inashindwaje kuyachukua mawazo yalitolewa na mwanahabari mmoja? Je huko siyo kuziathiri ibara mbili za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa ibara ya 18 na 19? Je CCM itaweza kuzungumza na mwananchi wa kawaida kama kunatokea sintofahamu?
Mbona CCM imekuwa na desturi ya kuzungumza yenyewe kwa yenyewe pale jambo linapoibuka? Kama hiki kisa cha Mkuu wa Wilaya , Mkurugenzi Mtendaji , Utingo, na kondakta, Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa na baadaye kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi? Je sasa ni Fasheni ya Kukwepa Kuongea Wenyewe kwa Wenyewe! Tutoe nafasi ya kuongea wenyewe kwa wenyewe.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka
“Pale tunakwepa Kuongea Wenyewe Kwa Wenyewe.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
Post a Comment