Adeladius Makwega-Musoma MARA TANZANIA.
Haya yalikuwa majira ya asubuhi ya Juni 29, 2025 Mwanakwetu yu nyumbani anapoishi akilini mwake akiwa njia panda ya kuchagua je leo hii nisali misa ya kwanza au nisali misa ya pili? Baadaye alikata shauri kuwa akasali misa ya pili ambayo huanza saa tatu kamili ya asubuhi katika Kanisa la Mtakatifu Augustino, Parokia ya Mwisenge Jimbo Katolilki la Musoma.
Akiwa nyumbani kwake akaamua kusikiliza mahuburi ya Kadinali Luis Antonie Tagle , Mkuu wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki inayojihusisha na Uinjilishaji wa watu Ulimwenguni, mara baada kusikiliza homilia hii tu laula wa la kwata umeme ulikatika, hivyo kwanza alidhani umeme umeisha katika mita yao , hilo hakupata majibu na hadi anatoka nyumba anapoishi kwenda kusali hana jibu . Duu! ile tu anaingia Kanisa umeme hakuna, hivyo basi alibaini kuwa umeme umekatika katika mji huu aliyozaliwa na kuzikwa Mwenye Heri Julius Kambarage Nyerere.
Akiwa katika Kanisa hili la Mtakatifu Augusino misa ilianza vizuri, msomaji wa somo la kwanza kijana alisoma vizuri lakini msomaji wa wimbo wa Katikati ambaye alikuwa ni Kiongozi wa Kwaya na mtu wa makamo pia ni muongozaji wa kwaya katika misa hii alishindwa kuyasoma mashairi ya zaburi kwa dakika karibu tatu , baadaye ilipatikana simu janja moja yenye tochi na kumsaidia kuyaona mashairi ya mzaburi, kisha kuimbwa vizuri sana na hapa kutoa nafasi ya msomaji wa somo la pili na hata Injili iliyosomwa na Padri Julius Ogolla mwanga kutoka simu janja ukituongoza.
Kwa hakika kanisa hili lilikuwa mwanga wa mishumaa kadhaa ya mbele ya altare na mwanga wa mshumaa wa tabelenakulo ambayo haikuweza kufua dafu kumsaidia msomaji wa maandishi mwenye umri mkubwa kuyaona maandishi haya.
Katika mahubiri ya misa hii iliyoongozwa na Padri Julius Ogolla, homilia ilifanywa na mtu mwingine ambaye mtayarishaji wa makala haya hakuweza kumfahamu lakini alikuwa mtawa wa kiume. Wakati wa mahubiri Mwanakwetu aliyasikiliza yote yaliyohubiriwa na huyu mtawa na kijana na pia Mwanakwetu aliyakumbuka yale mahubiri ya Kadinali Luis Antonie Tagle kwa dominika hii na muhtasari wake ni huu,
“Wakristo katika maisha yetu ya duniani , tuwe tayari kila siku inayokwenda kwa Mungu, kwa kushika na kuheshimu misingi ya imani yetu, maana kila mtu anayo siku yake anayooondoka duniani, huku tukijifunza namna mitume wa Yesu Kristo walivyofariki.”
Kumbuka msomaji wangu haya maelezo ni ya homilia ya kanisani hapa Parokia ya Mwisenge na ile ya Kadinali Tagle kwa pamoja Jumapili ya Juni 29, 2025.
Mahubiri haya yanaongeza na hili;
“Mitume Petro na Paulo kila mmoja aliuwawa; mmoja kwa kusulubiwa msalabani na mwingine kwa kukatwa kichwa. Matukio haya ni ya mwaka 66 na 67 baada ya Kristo, chini ya Mtawala wa Rumi Kaisari Nero. Ukifuatilia Kaisari baada ya mauwaji haya aliuliza jamani vipi je haya mauwaji yanawafurahisha mayahudi? Alijibiwa ndiyo na hili liliongeza kasi ya uonevu dhidi ya Ukristo. Huku Mtume Yohane peke yake ndiye aliyefariki kwa uzee yaani kifo cha kawaida. Wakristo hili ni darasa kubwa la kujifunza katika maisha ya mitume.”
Mtoa mahubiri kijana anaendelea na homilia yake , Mwanakwetu anamsikiliza kwa umakini mkubwa na hapa hapa akakumbuka maelezo haya ya Kadinal Tagle aliyoyasikiliza asubuhi akiwa kwake;
“Hebu tumtazame Yesu neno, aliyefanyika mwili akijifunua kwetu katika masomo ya Jumapili, leo ni sherehe ya watakatifu Petro na Paulo, katika injili ya dominika ya leo, Yesu anaonekana akiuliza. wanafunzi wake ‘Watu husema kuwa mwana wa Adamu ni nani, ninyi mnasema mimi ni nani?’ Kimsingi Bwana alikuwa akiwauliza ‘Je! mnanifahamu kiasi gani, nina jukumu gani katika maisha yenu, mnawaambia nini watu kuhusu mimi?’Yesu anawauliza wanafunzi wake maswali lukuki ambayo mimi na wewe tunaulizwa leo hii tunavyoendelea na maisha yetu.
Katika somo la kwanza na la pili tunajifunza kwamba, imani katika Yesu na kumshuhudia ndani usumbufu uliopo , upinzani na mateso tele waliyoyapata Petro na Paulo yaliwasogeza karibu na mateso ya Bwana ambaye hakuwaacha, malaika alimwokoa Petro kutoka kwa mkono wa Herode, Bwana alisimama karibu nao kama Paulo alivyoshuhudia, hivyo tunapoadhimisha kifo cha imani ya mitume wakuu wawili wa Kristo, na tumwachie Yesu Kristo chini ya nguzo zao. mwana wa Mungu aliye hai, hii ndiyo imani ya Petro na mitume, juu ya imani hii Bwana aliijenga na anaendelea kulijenga kanisa lake na milango ya kuzimu haitalishinda.”
Ibada hii ya misa iliendelea, huku Padri Julius Ogolla akiongoza misa akimulikiwa kwa kutumia simu janja iliyotolewa na mwanakwaya mmoja wa sauti ya nne na simu hii ilifanya kazi hadi misa hii inakamilika.
Misa ilipokamilika Mwanakwetu alitoka nje na akiwa anarudi nyumbani kwake kando ya kanisa hili alisikia sauti ya jenereta moja ikiunguruma ambayo ndiyo iliyotoa nishati ya umeme kuongeza sauti za spika ndani ya Kanisa la Mtakatifu Augusitino, Parokia ya Mwisenge Jimbo Katoliki la Musoma.
Mwanakwetu alipofika kwake aliyatayarisha makala haya akiwa na kompyuta yenye umeme kidogo sana, Mungu bahati majira ya saa 6. 27 adhuhuri umeme ulirejea na kuyakamilisha makala haya ya dominika ya 13 ya mwaka C wa Kanisa.
Mwanakwetu upo ?
Kumbuka
“Tujifunze Katika Maisha ya Mitume.”
Nakutakia Jumapili Njema.
0717649257
Post a Comment