MWENYEKITI MAISHA NI WATU

 




Adeladius Makwega-MBAGALA

Nilikuwa na utaratibu niliyojiwekea kuwa kila siku ya Jumamosi, Jumapili mchana na siku za mapumziko nashinda katika biashara hiyo ambayo ilikuwa inatazamana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Katika hiyo biashara mmliki alikuwa mdogo wangu wanne mdogo anayefahamika kama Samwel Makwega, huku kukiwa na mdogo wangu mwingine anayenifuata ambaye ananyonya ziwa la mama baada yangu.

Nikiwa nashinda hapa biashara kubwa ilikuwa ya samani kama; viti , meza, makabati na makochi hasa masofa ya kisasa ya gharama kubwa.

Kushinda katika biashara hii kulikuwa kunanipa nafasi ya kukaa na ndugu zangu, kuongea nao , kusaidiana kutatua changamoto za hapa na pale, kula chakula pamoja na hata kukutana na watu wengine wapya wanaofika kununua samani hizo. Samani hizp zilikuwa zinatengenezwa na vijana kadhaa akiwamo Samweli Makwega mwenyewe na wenzake, huku kukiwa na kundi la vijana wanaofanya biashara ya kuzinadi na kundi la mwisho wao walikuwa na jukumu la kuzibeba hadi nyumbani kwa mnunuzi na kuzipanga vizuri.

Hapa katika biashara hii kila kundi lina maana kubwa, huyu muuzaji (dalali) yeye alitakiwa kuvaa vizuri na kupendeza, lazima awe nadhifu, yeye alitaja bei ya sofa au samani yoyote iliyoopo sokoni kama milioni mbili na laki tano pesa inalipwa na kisha anamkabidhi sofa na wabebaji wanabeba kupeleka mzigo huo hadi katika lori husika. Huyu dalali pengine kakika milioni mbili na nusu pesa yake ni elfu sabini tu huku mwenye mali Samweli Makwega pesa yake ni milioni mbili na laki nne na huku elfu thelathini ni ya wabebaji.


 

Wale watengenezaji sofa walikuwa wanalipwa na mwenye ofisi ambaye ndiye Samweli Makwega kwa utaratibu waliojiwekea na Wabebaji wanalipwa muda mwingine na mwenye mzigo au mwenye Show Room maana wateja wengine wanalialia sana.

“Kazi ya kubeba ni nzito maana kazi kubwani ni kulipenyeza sofa kuingia ndani ya mlango wa nyumba au chumba,jukumu hili linahitaji uzoefu mkubwa.”

Kando ya hili banda kulikuwa na akina Mama Ntilie, wao wanapika chakula tangu chai , cha mchana hata cha jioni wanawauzia hawa mafundi, hapa Mama Ntilie wakati wa chai analeta chai, wakati mchana analeta chakula na wakati jioni analeta chakula cha jioni. Pesa yote ya huduma hii Mama Ntilie analipwa jioni.

Jioni utaisikia,

“Wewe mwanamke wa Kimakonde nipe hesabu yangu ya jana na leo.”

Mama Ntilie atajibu ,

“Wewe mpogolo hesabu yako ni elfu thelathini, unataka nirudi Ntwara mapema nini? Nimepanga  nirudi Ntwara nikiwa maiti siyo nikiwa hao, nilipe pesa yangu kwa wakati.”

Hizo ni Tambo za Maneno za Makabwela na Siyo Tambo za Maneno za Mabwenyenye.

Maisha yaliendelea, siku moja nimetoka nyumbani kwangu Mbagala hadi Uwanja Ndege, nikafika katika banda hili nikakaa huku tunapiga stori ilipofika mchana tukataka kula, vijana wakajibu mama muuzaji kafiwa, hivyo chakula hakipo inabidi tufunge safari kwenda kula kwa mbele jirani na kituo cha mabasi ya kwenda mjini kinachotazamana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam. Hapa tukawa tunakwenda kula kwa zamu huku wengine wanabaki golini kulinda goli tusipigwe bao. Msomaji wangu kupigwa bao hapa kuna maana mbili kwanza kuibiwa na pili mteja kufika hapa na kumkosa muuzaji.


 

Zamu ya Mwanakwetu kwenda kula ilifika, nikafika mkahawani nikala na kisha kuanza kurudi kwa miguu, wakati narudi zangu njiani kuna mtu akawa anaita.

“Chairman, Chairman, Chairman, chairma Makwega, Chairman Makwega, Chairman Adeladius Makwega”

Nikasema kumbe naitwa mimi! Huyu ananifahamu. Nikaitika labeeka huku nikigeuka, nikamuona huyo jamaa nikamsalimia vizuri.Tukaongea mengi, huku huyu jamaa nilipomuuliza unatoka wapi? Akajibu kaka natokea Ukonga Mombasa kufanya kazi na narudi nyumbani Kurasini jirani na Shimo la Udongo ambapo nimepanga.

“Haya vipi Chairman huku unafanya nini?”

Mwanakwetu akajibu kuwa hapa mbele tuna banda letu la fenicha kuna mdogo wangu anafanya biashara hiyo, huwa anaokota senti moja mbili, kwa hiyo mimi huwa nafika kushinda nao mara moja moja.

Hapa msomaji wangu tunaongea tunakwenda kwenye banda na huyu jamaa anatembea kwa mguu kurudi nyumbani kwake Kurasini Shimo la Udongo Huku Akiendelea Kuipunguza Safari.


 

Mwanakwetu akamuuliza huyu jamaa ,

“Yaani umetoka Ukonga kwa Miguu na unakwenda Kurasini kwa Miguu?”

Jamaa akajibu ndiyo maana tajiri leo hakulipa pesa yoyote ile.

Tukafika katika banda lile la samani nikamtambulisha huyu jamaa ndugu zangu wote na vijana wengine waliokuwapo kazini siku hiyo, nakumbuka vijana wawili wa Kipogolo ambao hawakuwa akina Makwega, Kijana Mmoja wa Kiluguru na kijana mmoja wa Kigogo na ndugu zangu wawili Modestus Makwega na Samwel Makwega.

Mwanakwetu akamwambia huyu jamaa tukae hapa kisha tutaondoka wote hadi Kurasini wewe utashuka uhasibu kisha mimi nitakwenda Mbagala, jamaa akajibu sawa.

Hawa jamaa katika biashara wakauliza huyu ni nani? Hapa hapa nikajibu,

“Huyu jamaa anaitwa fulani bin fulani alikuwa Mtumishi wa TBC ajira za mikataba yeye ni mtaalamu wa masuala ya usafi na bustani baadaye TBC waliipa kandarasi kampuni nyingine, wao wakaondolewa, hapa anatokea Ukonga Mombasa kufanya kazi.”

Hapa zikawa simulizi zingine zinaendelea huku wateja wanakuja kununua samani na kuondoka zao.

Mara likaja gari moja zuri na mzee mmoja mfupi tu akashuka, akaja katika banda akatusalimia akakagua kakagua na kuchagua sofa moja nzuri la gharama kubwa, kisha akalipa na akaomba lisiti, hapa akaitwa Samweli Makwega akatoa vitabu vyake akaandika na kusaini vizuri, yule mzee akapewa lisiti, akawa amekaa katika makochi tunayouza huku ukisoma lisiti, kisha akauliza huyu Makwega aliyesaini hapa ni wewe ? Kijana kando akajibu ndiyo, wewe ndiyo mwenye hii biashara? Samweli akajibu ndiyo. Makwega mtangazaji unamfahamu? Samweli akajibu ndiye ni kaka yangu mkubwa na tena yule pale. Samweli akawa ananisonda kidole pale nilipo na yule jamaa mtaalamu wa usafi na bustani.


 

Hapa hapa Mwanakwetu akamwambia huyu jamaa wa usafi na bustani

“Kaka hapa pana pesa ndogo ndogo- Hapa Pana Pesa Mara Mbili, wewe leo hauna kitu nakuomba kwa hisani yako nenda kapandishe zile sofa na nenda kashushe huko inapokwenda hii canter utapata pesa.”

Huyu jamaa wa usafi na bustani akawa anapakiza sofa zile na wale jamaa wengine, kisha Samweli Makwega akaita

“Broza njoo umsalimie huyu mzee wangu na mteja wangu...”

Nikaamka nilipokaa nikaenda kumsalimu huyu mzee, kisha akaniambia mambo mengi dhidi yangu, nikafurahi sana, huyu huyu mzee akaingia garini na canter ikamaliza kupakia na mimi kumuomba Samweli amruhusu huyu jamaa wa usafi na bustani aenda na canter ili akashushe hapa Kijana Mmoja akapungua ili kumpa nafasi huyu jamaa wa usafi na bustani.

Kwa hiyo Mwanakwetu sikumpa pesa huyu jamaa wa usafi na bustani lakini alipata kazi ile ambayo ilimpatia zaidi ya shilingi Elfu Kumi na Tano siku hiyo na kufika nyumbani kwa yule mzee huku mimi kurudi zangu Mbagala.Hapa msomaji wangu haya sasa ninasimuliwa ya yule jamaa wa usafi na bustani siku nyengine kabisa.

Walifika nyumbani kwa yule mzee kushusha sofa zile vizuri na kumpangia yule mzee sebuleni kwake na kuondoa sofa za zamani kisha huyu mzee akaongea sana na huyu jamaa wa usafi na bustani akimuuliza unawafahamu vipi akina Makwega?

Jamaa akajibu,

“Mimi nilikuwa nafanya kazi redioni, Makwega alikuwa mtangazaji, kwa hiyo mimi nilikuwa sina ajira ya kudumu mkataba ulipokwisha tukaondolewa, kazi zile walipewa kampuni , pale ulipotukuta yaani ndiyo ndiyo nimekutana na Makwega mkubwa nilikuwa sijamuona muda mrefu sana, yeye alikuwa Mwenyekiti wetu wa Wafanyakazi, pale alikuwa ndiyo anatoka kula akanipa hii kazi ya kupakia na kushusha hizi sofa ili nipate pesa.”

Huyu mzee akacheka sana, kisha akamuomba huyu jamaa wa usafi na bustani namba yake ya simu na akamwambia awe anakwenda nyumbani kwake kila Jumatano.


 

Jamaa wakalipwa pesa yao ya gari na ya kupakia na kushusha kisha kurudi Uwanja wa Ndege lakini kwa huyu jamaa wa usafi na bustani alishuka Bibi Titi Mohammed na kutafuta mabasi ya Posta Temeke kurudi zake Kurasini. Jamaa wa usafi wa bustani akawa kila jumatano anakwenda nyumbani kwa yule mzee anafanya kazi za bustani na za usafi na mazingira anakula chakula cha mchana na cha jioni kisha analipwa pesa yake na kurudi nyumbani kwake Kurasini.

Huyu mzee alimzoea sana huyu kijana wa usafi na bustani na baadaye kijana huyu alikuja kufahamu kuwa huyu mzee alikuja Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania na siku ile walipokuja kununua sofa alikuwa anatokea nje ya nchi kwa matibabu. Katika kufanya nae kazi hiyo kwa muda Jaji huyu alimwabia huyu kijana maneno haya,

“Nyumba yangu hapa inaupweke mno, niko mimi na mlinzi na wahudumu, mke wangu alishafariki, mimi ni mpweke sana, ukiwa na nafasi uwe unakuja tunaongwa.

Kazi zetu hizo ni nzuri sana lakini mwisho wa siku unakuwa mwenyewe, unakaa mwenyewe mwenyewe, unasikiliza redio hadi unawafahamu akina Makwega, ni tofauti kama ningekuwa Mwalimu ningekuwa nakaa mtaani hata katika vijiwe vya kahawa kuongea na wezangu, unapokuwa jaji au hakimu unahukumu makesi mengi mengi, makubwa makubwa, mwisho unaishi kwa uwoga uwoga, ukidhani kila mtu ni hatari kwako, kumbe walaa, unaishi hivyo hadi unafariki dunia.”

Kweli kila siku aliyokuwa anakwenda kufanya usafi kwa jaji, jaji alikuwa anatoka anakaa jirani na huyu kijana huku akifanya usafi wanaongea mambo mengi.


 

Huyu jamaa wa usafi na bustani amefanya kazi na huyu jaji hadi amefariki dunia. Huku akimwambia Mwanakwetu maneno haya,

“Cheameni Maisha ni Watu.”

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Kwa hakika rafiki zangu Majaji, Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Mawakili na wote miliosoma sheria makala haya ni yenu, tumieni hii taaluma kuhakikisha inajenga furaha yenu ya kudumu maishani mara baada ya kumaliza kazi, kila jambo lina mwanzo na mwisho wake na maisha ni watu.

Kwa hali ya sasa ya Tanzania serikali imefanya mambo makubwa mawili, kwanza kupitia Wizara ya Katiba na Sheria inatoa kinachoItwa msaada wa kisheria wakizunguka nchi nzima lakini pia kuna jambo la pili kuliundwa tume ya maboresho ya nafuu ya Kodi, nadhani wajumbe wake akiwamo Profesa Musa Assad, Profesa Luoga na wengineo wakizunguka nchi nzima. Lakini katika mashtaka yanayopelekwa mahakamani kwa sasa je yanasadifu shabaha ya serikali katika haya mambo makubwa makubwa mawili? Tume ya maboresho ya kodi na Leseni na hili la msaada wa kisheria?

Mwanakwetu ninachokiona hii inakuwa sawa na viatu vya kulia kushoto na kushoto kulia, inakuwa lugha gongana.

Yule yule anayetoa ushauri wa Kisheria

anapotengeneza mashitaka kwa  mwananchi anaingiza makosa yaleyale huyu hana leseni huyu hajalipa kodi , sawa hilo ni kosa swali ni moja ni je uliwahi kuwasiliana naye hata mara moja? Huyu ni ndugu yetu, huyu Mtanzania mwenzetu je tulimuuliza kwa nini hana leseni? Je alijibu nini?

Je upo ushahidi wa maandishi au hata simu ya mazungumzo ya kidugu ya pande hizo mbili? Mpaka wakashindana na hadi kutengenezwa shitaka mbele ya mahakama yetu tukufu?

“Mathalani kodi au luseni inaweza kuwa 500,000/ kwa mwaka, mawasiliano ya simu na ya kidugu ya pande mbili yanaweza kusaidia kujua huyu mtu anashida gani na anaweza akajitahidi kulipa hata laki 200,000/ hapa nchi itakuwa imepata pesa na itaokoa muda wa kupoteza mahakamani.”

Hapa msajili wa mahakama husika wawe na moyo kizalendo , mahakamani iwe makini na hili na hata hao wanaoleta mashauri haya watambue hili na huo ndiyo uzalendo wenyewe.

Kama pakiwa na umakini wa haya mambo, kesi zinazokwenda mahakamani na kupangiwa mahakimu na majaji ziwe zile ambazo mashauriano ya nje ya mahakama yawe yamegonga mwamba na hili litaondoa mitazamo kuwa mahakama inatumika vibaya na itaoondoa mtazamo mawakili wa serikali wanatumika vibaya maana hata hiyo mahakama inaendesha kwa fedha za Watanzania.

Kama mtazamo huu utabadilika utasaidia hawa mahakimu na majaji wetu na hata waendesha mashtaka kuwa sehemu ya jamii ya Watanzania, Watanzania watawapenda kama walivyo walimu wakishastaafu kazi.

“Jamii iseme Jaji fulani, hakimu fulani alikuwa ni mtu wa Haki, Jamii iseme Hakimu A alikuwa akisimamia ubinadamu ndani ya kuta za mahakama, Wakili fulani alikuwa akisimamia utu wa Mwanadamu.”

Kwa siku ya leo msomaji wangu inatosha sana na kwa siku ya leo nimeamua kumkumbuka rafiki yangu wa usafi na bustani na kisa hiki nilichokusimulia lakini kubwa mifumo yetu ya sheria na ya kimahakama lazima irejee mifumo ya kimahakama ya kijadi ambapo hakimu/jaji hakuwa adui wa jamii bali alikuwa sehemu ya hiyo hiyo jamii aliyoopo.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka

“Mwenyekiti Maisha ni Watu.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


 

0/Post a Comment/Comments