Adeladius Makwega-ARUSHA
Katika matini iliyotangulia nilimalizia kwa maswali kadhaa juu ya mwanafunzi bora wa taaluma wa Azania na Tambaza wakati huo Abdil Rashid Mohamed. Ninawashukuru mno wasomaji wangu wengi kwa kuyajibu maswali hayo. Nianze na ndugu Christopher Mwakyusa huyu alisoma Tambaza tangu kidato cha kwanza hadi sita na ni miongoni mwa walisoma na Abdil Rashid.
“Mimi nimesoma naye na kumaliza naye mwaka mmoja, Abdil Rashid alikuwa na wenzake wawili waliokuwa wakifanya vizuri sana kitaaluma nao ni Fredric Peter na Emmanuel Mmari.”
Kwa maelezo ya ndugu Mwakyusa msomaji wa matini hii nakupa ahadi ya kuwasaka hawa ndugu hao wawili yaani FREDRIC PETER na EMMANUEL MMARI walipo.
“Abdil Rashid yupo, ni rafiki yangu sana, tulimaliza pamoja mwaka yeye PCM na mimi PCB. Pia Dkt Zaitun, siku kadhaa zilizopita amezika mtoto wake wa miaka 10. Kikazi yupo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Idara ya upasuaji kwa watoto wadogo.”
Dkt Edmund Eliezer Ndalama, huyu ni kaka yangu anayefanya kazi MNH aliniuma sikio hayo. Kwa kuwa dada yetu Dkt Zaitun amefiwa na mtoto wake binafsi ninatoa pole kwake na familia yake kwa msiba huo na mwenyezi Mungu ampitishe salama katika kipindi hicho kigumu.
Kapu langu la maoni lilipokea majibu mengi juu ya jambo hili, Aliyefunga kapu langu la maoni ni Mwanahabari mahiri ambaye amefanya kazi na vyombo vingi ya Kitaifa na Kimataifa hapa Tanzania ambaye sasa amekita kambi na AZAM media groups, huku awali alifanya kazi na Star TV na RFA na TBC akibobea katika kufanya kazi za Runinga na Redio naye ni Baruani Mhuza.
Ndugu Mhuza wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Azania sekondari, anasema kuwa maisha ya Azania sekondari wakati huo akiyakumbuka anapata furaha tele.
“Nilikuwa natoka zangu Reli Gerezani hadi Azania na siku ya ugomvi wa Azania na Tambaza ulipotokea shuleni ulihamishiwa Kariakoo na pia nakumbuka kuwa miongoni mwa wanafunzi wapenda kusoma alikuwa ni Abdil Rashid ninaambiwa sasa ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitengo cha Kompyuta.”
Nawashukuru sana kwa wote waliotuma maoni yao kwa leo.
Hali ya shule ya Tambaza iliendelea kufungwa huku wanafunzi wake wakibakia majumbani, wapo ambao waliweza kujisomea majumbani kwa mbinu mbalimbali na wengine walibakia nyumbani kufanya kazi za familia zao.
Serikali iliamua kuifungua shule hiyo baada ya Wizara ya Elimu ya wakati huo kutangaza kupitia RTD.
“Serikali imeifungua shule ya Tambaza lakini wanafunzi ambao wamebainika kushiriki katika fujo kadhaa za shule hiyo wataondolewa na wanafunzi wengine wote watarudi kwa masharti maalumu baada ya kusaini mkataba wa kutokushiriki katika vitendo vyovyote vya kuipa Tambaza jina baya.”
Kweli wanafunzi wote tulifika shuleni na kukusanyika katika uwanja mdogo wa mpira wa miguu na kukaa chini huku walimu wa madarasa husika wakitupatia fomu ya kusaini makubaliano hayo ambapo kila mmoja alijaza fomu hiyo maalumu.
Kabla yakujaza fomu hiyo kila mmoja alitakiwa kuyataja majina ya wanafunzi wakorofi shuleni hapo.
Tukiwa katika zoezi hilo la kujaza fomu maalumu wanafunzi wote walitakiwa kuelekea madarasani kwao, wakiwa katika harakati hizo za kuingia darasani walipita katika stoo moja ambayo ilikuwa na milango wazi, kundi la wanafunzi waliingia kwa nguvu na kuchukua vitabu kadhaa na kurudi navyo majumbani.
Huku wakisahau kuwa shule hiyo ilifungwa kutokana na vurugu. Jambo hilo lilikuwa sawa na kuweka sindano ya moto katika kindonda kibichi, kazi iliyobaki ilikuwa ni kuwasaka waliofanya hivyo na walipatikana na kufukuzwa shule.
Pia majina ya wanafunzi ambao inadaiwa walitajwa katika orodha maalumu na walifukuzwa na wengine kuhamishwa. Wanafunzi wengine wakiachwa na kuendelea na masomo.
Zoezi hilo la kuifungua shule hiyo lilifuatwa na hatua ya kuwahamisha walimu wote wa shule hii na kuwapeleka shule zingine za sekondari Jijini Dar es Salaam. Huku zoezi hilo likiambatana na kumuhamishia Wizara ya Elimu, mkuu wa shule hii wakati huo marehemu Julius Mushi.
Uhamisho huo ulisababisha Tambaza kupata mkuu wa shule mpya akitokea Pugu sekondari, walimu wapya ambao walikuwa hawana uzoefu wowote na shule hii. Jambo hilo likiwaumiza mno wanafunzi wa Tambaza. Bodi ya shule ya Tambaza mpya iliundwa angalau kuendana na mabadiliko mapya ya shule hii ambapo wajumbe wengi walikuwa wakitoka katika vyombo vya ulinzi na usalama.
Je kipi kitaendelea?
Subiri matini ijayo.
Kumbuka,
“Mgogoro wa Azania na Tambaza XVII.”
Nakutakia siku njema.
makwadeladius@gmail.com
0717649257
Post a Comment