MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA VIII

 


Adeladius Makwega KICHANGA CHUI

Katika sehemu ya iliyotangulia ya matini haya nilieleza kikosi cha timu ya soka ya shule ya Sekondari Jitegemee kilivyokuwa huku kikiwa na wachezaji kadhaa ambao walisoma Tambaza kidato cha kwanza hadi cha nne na nilieleza namna mimi binafsi nilivyoweza kufika nyumbani kwetu Mbagala.

Kwa hakika tukio hilo lilleta taharuki kubwa Jijini Dar es Salaam wakati huo, huku kila mwanafunzi wa Tambaza akifika nyumbani kwa tabu sana nao wanafunzi kadhaa wa Tambaza walikamatwa na Jeshi la Polidsi na kulala korokoloni siku hiyo.

Wapo wanafunzi kadhaa waliokamatwa na kuweka katika mahabusu kadhaa za vituo cha polisi Dar es Salaam, walikusanywa pamoja na kupelekwa Segerea wakati huo lilifahamika kama Gereza Jipya lilikuwa ndiyo linaanza kazi maana majengo yake yalikuwa yamekamilika. Huku vijana wa Tambaza walisema kuwa wewe ndiyo wamelibikiri Gereza la Segerea na kutokana na walikamatwa kuwa wengi hivi vituo vya polisi vya Katikati ya Jiji havikutosha, ndipo safari ya Segerea iliwadia.


 

Hapa. kazi kubwa ilifanywa na Jeshi la Polisi katika siku hiyo. Nayo Ijumaa yake tukiwa shuleni Tambaza hali haikuwa imetulia kwani Jeshi la Polisi liliwabana vilivyo wanafunzi wote wa Tambaza waliokamatwa na jambo hilo lifanya wanafunzi wengine wafuatwe majumbani kwao na wengine shuleni Tambaza huku majina kadhaa ya Kihuni yakitajwa.

Jeshi la Polisi lilikita kambi shuleni Tambaza huku Makarandinga ya Polisi yakiwapo mbele ya shule hii kuwakusanya wanafunzi waliotajwa na wenzao na hata wengine waliotambuliwa katika Gwaride la Utambulisho.

Kumbe katika magari haya ya polisi kulikuwa na wanafunzi kadhaa wa Jitegemee, walimu na baadhi ya Askari wa JKT ambao waliambatana nao shuleni Tambaza wakisindikizwa na mitutu ya bunduki kuwafuata hapo waliotuhumiwa kufanya fujo hizo ndani ya gwaride la utambulisho, majina kama KANARUZA, MZEE OLE ODINGA OGINGA , VIMTO, ASKOFU, BUCHIZA, MZUKIZI, BAKHRESA na wengine wengi yakitajwa.

Kuogopa kutokea vurugu zingine hapo shuleni, tuliambiwa wanafunzi wote tuingie madarasani mwetu, alafu tukaambia wote tupande ngazi katika ghorofani ya juu na tupange mistari. Kila mwalimu wa darasa na daftari ya maudhurio yakisoma majina waliokuwepo na baadaye wote tulitoka nje na kuchuchuma huku polisi wakipita na wanafunzi wa Jitegemee kuwatambua waliofanya vurugu.


 

Sasa ilikuwa ngumu kwa majina hayo ya utani watu kupatikana maana watu wanafunzi wengi wenye majina ya kutisha walikuwa majina yao mazuri tu mathalana BAKRESA alikuwa jina zuri na Kanisa Katoliki Simon Mabega.

Gwaride hilo halikuwagusa wanafunzi wa kidato cha tano na sita japokuwa polisi waliingia huko na kuwakuta akina Christopher Mwakyusa na vitabu vyao vikubwa wakijisomea kana kwamba hawakuwapo uwanjani siku hiyo, kumbe walikuwepo maana chama SAMBUKILE lilikuwa uwanjani. Shida ya Gwaride la Utambulisho ni moja tu mtu akikutaja tu iwe kwa kubahatisha ama kufananisha ndugu yangu hadi uonekane siyo wewe hapo utakuwa umeshapata tabu mno.Wako watu wengi walilala segerea kwa muda kosa lilikuwa kutambulia katika Gwaride La Utambulisho, Gwaride lilizidi kuwatia homa wanafunzi wengi na masomo hayakusomeshwa tena. Ukishatambuliwa hadi mahabusu, Unasomewa mashtaka alafu Segerea. Wanafunzi kadhaa walikamatwa na kusomewa mashtaka Mahakama ya Kisutu na baadaye Segerea lakini baadaye mashauri hayo yalifutwa na wanafunzi wengi waliokuwa na mashauri hayo walihamishiwa mikoani katika shule za umma.

Naomba msomaji wangu ifahamike kuwa maisha ni hatua, wapo ambao ni Wachungaji wakubwa sana hii leo, wapo ambao ni mashekhe wakubwa sana wanatoa dawa na mawaidha misikitini,na kwa makala haya wanayasoma, huku wakisema moyoni astghafulai huku Makwega asije kuleta balaa akafichua siri zetu Misikiti na Makanisa yakakosa waamini.

Ndugu zangu tuliyosoma wote Tambaza msihofu, huku sitofika, mwingine ni Mkuu wa Wilaya, mie namuangali yeye anajifanya kasahau ngoja siku nitamkumbusha, siku hizi kawa mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.

 

Msomaji wangu wapo wanahabari, wapo madaktari leo hii,viongozi wa taasisi za umma na hata wengine wapo katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama mgogoro wa Tambaza uliwasaidia wakapata kazi, ambao walikuwa wanafunzi wa shule sasa wanalijenga taifa. Yale yalikuwa ni maisha ya shule tu.

Msomaji wangu tambua jambo moja katika simulizi hii, nakuwa mvivu kutaja majina ya watu wengi kwa hoja hii ya leo, baadhi yao nawasiliana nao na wanakubaliana niwataje majina yao.Natoa ahadi kuwa kila unapoliona jina la mtu nimelitaja humu na kusimulia kwa kirefu tambua kuwa nimewasiliana naye vizuri lakini bado nafanya mawasiliano kadhaa na ndugu zangu hawa kwa karibu.Pia nimebaini kuwa napata ushirikiano mkubwa wakiwamo wanafunzi kadhaa wa Azania wakati huo, Jangwani Girls wakati huo Zanaki Girls wakati huo, Kisutu Girls, Forodhani na hata Jitegemee. Nimejitahidi zaidi kuwa makini hasa kwa akina mama kwani pengine kulitaja humu jina lake linaweza kuleta utata katika familia zao ndiyo maana baadhi ya majina mengine siyataji kabisa.


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Siku hii ya Gwaride la Utambulisho nakuomba msomaji wangu ufahamu Mwanakwetu alikaguliwa lakini hakutambuliwa kwa wale waliofanya vurugu , yote haya ni maisha ya shule tu.

Je kipi kitaendelea subiri matini ijayo. Mwanakwetu upo?

Kumbuka

“Mgogoro wa Azania na Tambaza VIII.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 


 











 

 

0/Post a Comment/Comments