MGOGORO WA AZANIA NA TAMBAZA IX

 

Adeladius Makwega–Mtoni Kijichi

Katika makala iliyotangulia nilieleza namna Gwaride la Utambulisho lilivyofanyika na namna wanafunzi kadhaa walivyokamatwa na kupelekwa mahabusu, mahakamani Kisutu na baadaye gerezani Segerea. Labda kwa siku ya  leo msomaji wangu nitumie wasaa huu kwa kiasi kupata maoni ya mdau mmoja anayeitwa Peter Ambrose Ngasa ambaye wakati huo alikuwa mwanafunzi wa Forodhani Sekondari, pia alikuwa mchezaji wa Timu ya Sekondari ya Forodhani wakati wa michezo hiyo ya UMISETA mwaka 1993, yeye aliyasema haya,

“Mechi kati ya Tambaza na Jitegemee ilikuwa fainali, kwa sababu nusu fainali ilikuwa baina ya Tambaza na Forodhani hapa Tambaza ilishinda mabao matatu kwa mawili. Nayo Jitegemee ilingia fainali baada ya kuifunga St Antony ya Mbagala Sabasaba.”

Hapa ndipo fainali ilizua ugomvi mkubwa na mshindi hakupatika hadi leo hii. Ndugu sasa anaendelea kusimulia kuwa,

“Mimi niliondoka nyumbani mapema baada ya kuona kuwa vurugu zilipokuwa zinaanza.”

Mwanakwetu binafsi kabisa namshukuru sana ndugu Peter Ambrose Ngassa kwa kumbukumbu hiyo ila jambo hili la Nusu Fainali au Fainali nitalijibu siku nyengine.

Kwa kuwa ndugu Ambrose Ngassa amezungumzia Shule ye Sekondari Mtakatifu Antony wa Padua ya Mbagala iliyoingia nusu fainali naomba msomaji wangu kwa hisani yako nieleze kidogo jambo moja juu ya historia ya shule ya hii ya nyumbani kwa akina Mwanakwetu –Mbagala ambapo historia hii nadhani hata Kanisa Katoliki la Jimbo Kuu la Dar es Salaam hawana.

“Shule hii ilianzishwa na Parokia Mbagala katikati ya miaka ya 1980 ambapo ikipokea wanafunzi bila ya kujali dini kama ilivyokuwa Kinondoni Musilimu. Wakati huo walitumia majengo yaliyokuwa yalikitumiwa kama Chekechekea Parokiani Mbagala (Sasa ni Mbagala Spritual Centre-Walipo Shirika la Dada Wadogo) yale majengo yasiyo ya ghorofa ambayo yanatumika kama vyumba vya vikao na jiko jirani mkono wa kushoto kama unaingia Mbagala Spritual Centre hivi sasa. Shule hiyo ilihamishiwa Mbagala Zakhem ambapo Parokia ilihamishiwa huko lakini baadaye Kanisa Katoliki liliomba eneo kwa Kijiji cha Mbagala kwa viongozi wa Kijiji hicho akiwemo Diwani wa Mbagala wakati huo aliyefahamika kama Dianakile.

Kwa msaada wa karibu wa Balozi Paul Rupia na Peter Pinda waliwezesha kupatikana eneo hilo na kuanza ujenzi wa shule hii chini ya usimamizi wa Padri Fidelis (Padri Muitaliano). Kwa kuwa hapa ametajwa ndugu Peter Pinda huyu jamaa aliwahi kuwa mwalimu wa kwaya ya Kanisa la Mtakatifu Antony wa Padua Parokia ya Mbagala miaka ya 1970, akiwa kijana sana. Nadhani Padri Fidelis walifahamiana na Peter Pinda wakati huo. Huyu Padri Fidelis wakati huo iliaminika kuwa alitoka mataifa ya Pembe za Afrika, kama Siyo Ethiopia, Elitria basi Somalia ambapo alikuwa akifanya utume wake awali akitokea kwao Italia. Peter Pinda(Mizengo Pinda) ambaye baadaye alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya Edward Lowassa kuachia ngazi na mjomba Jakaya Kikwete kumchagua ndugu Peter Pinda kuziba pengo hili.

Kwa hiyo shule hii ilibadlishwa majina mengi awali ilikuwa inaitwa AMET Sekondari na baadaye ikawa St Antony (Padua) ambaye ndiye aliyekuwa Mtakatifu wa Parokia ya Mbagala wakati huo.

Hapa ikitoa nafasi kwa watu wa Mbagala kusoma shule hii kwa kujilipia chini ya Mkuu wa Shule Mwalimu John Emanuel Laurent Sagara (John. E. L Sagara), Mwalimu Robert Mfugale, Mwalimu Komba sasa ni PHD anaitwa Dkt. Komba na wengine wengi.”

Najua hapa pana maswali mengi sana hasa hasa Mwanakwetu alijuaje ushiriki wa Balozi Paul Rupia na Peter Pinda katika kufanikisha shule hii kupata eneo?

“Binafsi Mbagala ni nyumbani kwetu na ukoo wetu upo katika eneo hilo tangu mwanzoni mwa miaka 1950 hii ni mosi. Wakati Padri Fidelis (Muitalino) anazikwa mwaka 1993/1994 nilikuwepo katika maziko yake nikiwa mwanafunzi wa Tambaza wakati huu, hili ni la pili. Balozi Paul Rupia ambaye nadhani alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi wakati huo alikuwepo katika mazishi ya Padri Fidelis huku majina kama Peter Pinda yalitajwa kama shukurani msibani pale Mbagala Spritual Centre.”

Nakumbuka kuwa eneo la sasa ilipo shule hii lilikuwa na miembe mingi,


 

tukiwa wadogo tulikuwa tukienda okota embe na kucheza mpira maana ni eneo tambarare sana.

“Unapoingia shuleni hapo kuna sanamu moja kubwa ya Mtakatifu Antony wa Padua ambayo binafsi siku inapachikwa hapo juu nilishirika kuipachika hapo juu mwaka 1989, wezangu wengine walioshiriki kuifanya kazi hiyo ni mzee mmoja wa Kimakonde anaitwa Mzee Emmanuel(alikuwa mhudumu), Robert Sinna (sasa ni Mtaalamu wa Uchumi na Fedha), piaalikuwepo fundi seremala wa parokia ya Mbagala, Dereva mmoja wa Parokia ambaye jina lake silikumbuki, Padri Fidelis(Padri Muitaliano), Benson Masonoro, Dickson Masonoro na Adeladius Makwega (Mwanakwetu).”

Siku hiyo ninakumbuka,

“Sanamu hiyo ilitolewa katika koontena moja maalumu Mbagala Misheni (sasa ni Mbagala Spritual Centre) na kuondolewa karatasi zake nailoni mbili na kupakiwa katika gari ndogo kibanda wazi na kwenda kuipachika katika shule hiyo umbali kama wa kilometakati ya mbili na tatu hivi. Sifahamu kama sanamu hio bado ipo hapo shuleni Mbagala kwa maana mara ya mwisho kuingia hapo ilikuwa ni mwaka 1989 hadi leo ni miaka mingi mno.”

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Siku ya leo Mwanakwetu alijaribu kusafiri nawe hasa kuifahamu zaidi Shule ya Mtakatifu Antony wa Padua Mbagala wakati ikianza na hii inatokana na swali la ndugu Peter Ambrose Ngasa ambaye alikuwa mwanafunzi wa Forodhani Sekondari wakati huo.


 

Kwa sasa Adeladius Makwega, Robert Sinna na hata Watoto wa marehemu Mzee Emmanuel walioshiriki kuipachika sanamu la Mtakatifu Antony wa Padua mwaka 1989 shuleni hapa wakifika shuleni hapa hakuna anayeweza kuwafahamu na pengine hata wakiatka nafasi ya vijana wao kusoma itakuwa kazi, maana Padri Fidelis amefariki labda kidogo kidogo Mwanakwetu ana matumaini maana amemuona Sista Maria Goleti Sisiani ambaye sasa ni makamu Mkuu wa shule kutoka Shirika la Dada wa Wadogo wakati huo alikuwa ndiyo binti anaingia utawa , akiwaona akina Mwanakwetu vijana wakorofi  na watukutu Sista Maria alikuwa mdogo, huku tukimchokoza  akiwa binti mdogo, mwembamba, mrefu, mweupe akiwa na kilemba kifupi.

“Sista Maria Goleti Sisiani usihofu, siku hizi sisi ni maafisa wakubwa siji kuomba nafasi ya wanangu kusoma hapo maana wanangu wote wanasoma shule za umma na za bure lakini nimekukumbuka tu nitakuja kukutembelea siku moja, kikubwa ni kuyakumbuka haya maisha ya watu wa Mbagala wa wakati huo ukiwamo na wewe ukiwa ndiyo unaingia utawa.”

Mwanakwetu upo?


 

Kumbuka,

“Mgogoro wa Azania na Tambaza IX.”

Naomba kwa leo niishie hapo. Je kipi kitaendelea? Subiri Makala Ijayo

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 

0/Post a Comment/Comments