ANACHEZA YOYOTE YULE ILI MRADI NAMBA HIYO ANAMUDU

Adeladius Makwega-MBAGALA

Huu ni wakati mwingine na siku nyingine ninayokualika tena katika Makala ya Katuni, kumbuka haya ni Makala ya Uchambuzi wa Katuni kama zilivyochorwa na kuzingatiwa na wachoraji wa katuni hizo kutoka vyanzo mbalimbali ambapo katuni nne zinateuliwa, zinaelezewa kwa namna zilivyo, kisha kuchambuliwa kwa jicho la Mtayarishaji Wetu.

Kuyaanza makala haya siku ya leo Mwanakwetu anaikamata katuni moja hii ni katuni namba akiwa kidhahania katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ali Possi na bado Mwanakwetu akiwa mlangoni kwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Alice Mtulo akibisha hodi hodii hodiiii…


 

Mwanakwetu anaikamata katuni ya namba moja iliyochorwa na Said wa Michael wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani DW KISWAHILI ambapo Ijumaa ya Juni 13.2025 ilikuwa ni siku ya kimataifa ya uelewa kuhusu watu wenye ualbino, siku hiii ilipambwa na kauli mbiu ya mwaka 2025 inayopiga debe hitaji la dharura la kuzuia saratani ya ngozi kwa watu wenye ualbino kupitia uhamasishaji, uchunguzi, na ufikiaji wa jua. 

Said wa Michael alichora katuni inaonesha vijana wawili wenye ualbino mvulana akivaa mavazi ya Timu ya Yanga ya Dar es Salaam naye msichana akiwa amevaa jezi ya timu ya Simba ya Dar es Salaam, huku huyu binti akipiga danadana na akisema maneno haya Linda Ngozi Zetu, nayeye mvulana hakuwa kimya akisema Hifadhi Maisha Yetu.

“Linda Ngozi Zetu; Hifadhi Maisha Yetu.”

Kwa hakika katuni hii ya DW Kiswahili inajieleza vizuri, kikubwa wenye jukumu la kuwapatia dawa na vifaa vya kulinda ngozi ya ndugu Alibino watimize wajibu na vifaa hivyo vitolewe bure na hili liwekwe katika bajeti za Wizara zetu za Afya na vifaa hivyo vitolewe bure, Mwanakwetu narudia na kwa hili la Linda Maisha Yao, serikalia zetu zitimize wajibu huu ipasavyo.


 

Mwanakwetu sasa anaikamata katuni ya pili iliyochorwa na jamaa mmoja anayetambulika kama Msamba, yeye amechora picha ya jamaa mmoja anatuma pesa zake kutoka simu yake kwenda kwa mtu mwingine katika hatua hizo jamaa mtandaoni wanaibuka na kukwapua pesa hizo ambazo zinaonekana vibunda vya fedha

Katika katuni hii Mwanakwetu anaona wazi kuwa mchoraji wake anakerwa na tabia ya wizi  mtandaoni hapa akipaza sauti yake kuwa wizi huo ukomeshwee.

Mwanakwetu anaendelea kulipiga Gwaride la Makala ya Katuni akiwa Ofisini ya Wakili Mkuu wa Serikali kidhahania, akisisitiza Naibu Wakili Mkuu wa Serikali akumbuke kuitikia hodi ya Mwanakwetu,hodiii hodiii hodiii... akiwa hapa hapa anaikamata katuni ya tatu iliyochorwa na GADO huko nchini Kenya akionesha dubuwana moja kubwa huku likipita katika njia yenye vitu vya hatari kama vile mawe, nyundo, visu, mapanga, nyembe, misumari, shoka na mabumu huku jamaa hili likivuka salama kabisa likiendelea kuchanja mbuga. Huyu jamaa amepewa kibandiko Lissu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA ambaye  yupo Korokoroni akitwishwa mzigo mzito wa kesi ya uhaini. 

Katuni hii ya Mchoraji Gado inaibua matumaini kuwa Tundu Lissu hata kama ana kesi ya uhaini kuwa hata katika hili atavuka salama maana ni mtu hodari, aliyejaliwa uwezo wa kuvuka vihunzi vya kila namna.

Mwanakwetu anaona kuwa haya ni matumaini ya kutia moyo yanayoibuliwa na  mchoraji katuni hii kwa hadhira yake hasa ile ya Tanzania na wapenda Demokrasia ya haki na kweli akiwamo Mwanakwetu mtu mdogo kutoka Mbagala Sabasaba.

Katuni hii ya Gado inatoa nafasi ya Mwanakwetu kuikamata katuni ya nne na ya mwisho ambapo kunaonekana jamaa mwenye sura kama ya marehemu John Pombe Magufuli akiwa amembeba mtoto mapajani mwake, huku akipiga kelele na kwa kando kuna chupa kunyonyeshea mwana lakini mtoto aliyelazwa katika mapaja ya John Pombe Magufuli anapiga kelele tu. Jamaa mwenye sura ya John Pombe anapatwa mambo mawili kwanza anastaajabu na pili anashangaa hii ni nini?

Mwanakwetu anapoitazama vizuri katuni hii kwanza inaonekana ni ya zamani, kwa hiyo Mwanakwetu anaitazama kwa taswira ya mwaka wa 2020 na pili anaitazama kwa sura ya mwaka huu wa 2025. 

Kwa Mwaka wa 2020 inaonesha kuwa John Pombe Magufuli alikuwa akiwajali mno Watanzania kwa kuwapa kila kitu wavitakavyo kama mwana na baba yake , lakini waliendelea kulalamika. Jambo hilo likamchanganya mno na ndiyo maana anaibuka na alama hizo mbili kustajabu na kujiuliza.


 

Kwa mwaka huu wa 2025 taswira iliyopo katika katuni hii ni kuwa John Pombe amefariki dunia lakini bado hata wale waliyokuwa nao akiwafundisha siasa sana sana kuwalea bado wanapiga kelele akiwamo Askofu Dkt. Josephart Gwajima na wengine wengi. John Pombe Magufuli akiwa huko alipo anashangaa jamani mambo bado yale yale tu ?


 

Mwanakwetu upo?

Kwa hakika makala ya katuni siku ya leo imetayarishwa na Mwanakwetu akiwa kidhahania katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambapo amepiga hodi hodii hodiiii...

Hapa hapa Mwanakwetu amekutana na picha moja nzuri waliyopiga Viongozi wa Wakili Mkuu wa Serikali na Viongozi wa  Tanganyika Law Society (TLS) chini  ya Wakili Msomi na Rais wa  TLS Bruda(Kaka Mkubwa) Mwambukusi. 

Picha hii Mwanakwetu kaipenda mno maana mahusiano kama haya yakukutana na hata kufanya kazi pamoja ni muhimu na ndiyo yanayotakiwa, inawekezana TLS wakawa na mawakili wazuri ambao hawapo Serikalini , hapa hapa Wakili Mkuu wa Serikali anaweza kuwaalika katika mashauri kwenda kupambana pamoja kwa kuongeza  nguvu kuitetea nchi yetu, hata MAWAKILI binafsi wapo Watanzania wenye uwezo mkubwa  mbona tunawateua MAJAJI tuwatumie.

Msomaji wnagu nakuomba nikunong’oneze katika picha hii naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi Alice Mtulo yupo, yupoo yupooo...Kumbuka hodiii hodiii hodiiii za Mwanakwetu zinazokosa majibu.


 

Niseme tu,

“Wakili Mkuu wa Serikali ni Timu ya Taifa Anacheza Mtu Yoyote Yule ili Mradi tu Namba hiyo Anaimudu.”

Basi msomaji wangu siku ya leo Makala ya Katuni yalikuwa na Katuni Nne, ile ya wizi wa fedha katika simu, katuni ya pili ni ile ya kuwalinda Albino, katuni ya tatu ni ile ya Tundu Lissu namna anavyoruka vigingi mbele yake na katuni ya nne ya mwisho ni hii ya John Pombe Magufuli akiwa na mshangao tele na hali inavyoendelea nchini Tanzania.

Basi Kwa katuni hizo nne, ndiyo na mimi natia nanga ya Makala ya Katuni Siku ya Leo. 

Swali ni je makala haya siku ya leo niyaitaje? 

Tundu Lissu Mruka Vihunzi? Au Wakili Mkuu wa Serikali Ni Timu ya Taifa Anacheza Yoyote Ili Muradi)Mradi) Namba Hiyo Anaimudu.Msomaji wangu  jukumu lako wewe ni kuchagua kichwa kimoja tu.

Nakuaga kwa heri  kwa hodiii hodiiiii hodiiiiii....Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257




 



0/Post a Comment/Comments