AKASALIMU AMRI

 

 Adeladius Makwega-MAKOLE

Mwaka 2001 nilijiunga na chuo cha Ualimu Kasulu kwa kozi ya stashahada kwa masomo ya Kiswahili na Kiingereza na kwa wakati huo chuo hiki kikitoa mafunzo ya ualimu wa masomo ya Biashara, Historia Jiografia na Astashahada ya Ualimu.

Kipindi hicho Serikali ya Rais wa Awamu ya Tatu ya marehemu Benjamin Mkapa ilianzisha mpango wa elimu ya msingi kwa walioikosa, hii ikiongeza idadi kubwa na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, kwa hiyo kusudio hilo la serikali lilikuwa na ongezeko la wanafunzi na lilitakiwa liende sambamba na ongezeko la walimu na kweli vyuo kadhaa vilipata walimu tarajali (Wakurufunzi)

Maisha ya chuoni yalikuwa mazuri sana, japokuwa wilaya ya Kasulu ilikuwa haina umeme, usiku mji huo ulikuwa giza kwa mbali vilionekana vijinga vya moto vya walina asali, vibatari na taa za chemli lakini chuoni kulikuwa na jenereta kubwa za kuzalisha umeme likiwashwa mara moja moja huku likisambaza umeme kwa baadhi ya taasisi na makazi yaliyohitaji huduma hii kwa malipo kidogo.


 

Maisha ya Chuo yaliendelea vizuri, Mwaka 2002 wenzetu wa mwaka pili wa stashahada na astashahada walikaribia kumaliza, kwa hiyo uongozi wa wanachuo nao ulikuwa unamaliza muda wake. Kwa hiyo ulifika wakati wa kuchagua viongozi wapya wa serikali ya wanachuo; mwenyekiti na makamu mwenyekiti na wengineo. Huku baadhi ya rafiki zangu walinishawishi wakisema Mwanakwetu tunakuomba uingie katika mchakato huo, mimi nikisema kuwa suala hilo ni gumu kwa kuwa sikuwa na pesa ya kuchapisha vipeperushi na gharama zingine.


 

Rafiki zangu hawa walizungumza na ndugu mmoja aliyekuwa akisoma Stashahada ya Biashara mwaka pili, Mboka Mwambusi(Mnyakyusa wa Mbeya) wakieleza kuwa,

“Sisi tunataka Makwega awe mwenyekiti lakini ndugu yetu hana pesa.Mboka wewe ni mwenyeji hapa Kasulu tunapata wapi pesa? Jamaa akigombea tutashinda mapema.”

 

Mboka Mwambusi akajibu ,

 

“Sawa nitawasaidia kila kitu na mtapata, lakini mkichaguliwa muwasaidie watu, siyo muende huko mkayafanye mambo yenu alafu watu wawe wanaonewaonewa, huku wakifukuzwa fukuzwa.”

 

Majibu yalikuwa hatuwezi kuwa watu wa hovyo namna hiyo.

Kwa kifupi msomaji wangu nakuomba umfahamu Mwalimu Mboka Mwambusi yeye alisoma Shaycom, mimi nilisoma Ndanda sasa kufahamiana naye kwa karibu ni kwa kuwa Mboka alinichagua kuwa miongoni mwa waandishi mahiri wa gazeti la wanachuo, huku tukifanya propaganda za chuoni, habari zilikuwa zinaandikwa kwa mkono na mwanachuo mwenye mwandiko mzuri, nakubandikwa katika ubao wa matangazo ya wanachuo kwa wiki mara moja.

Huko Shaycom Mboka Mwambusi alisoma na rafiki zangu kadhaa akiwamo Seralini Sawa (Mpogolo), Stanley Nkambwe (Mhaya) na Said Mhando(Mzigua wa Morogoro ) na tulipokuwa tunazungumza nayeye, hawa niliombatana nao, pia alikuwepo Mwalimu Hija Mashaka(Msukuma wa Mwanza) na Rashidi Ali (Mmakonde).

Mwalimu Mboka Mwambusi akasema,

 

“Pesa ipo na pahala pa kuchapisha karatasi nitawapeleka, nyinyi chukueni fomu.”

 

Fomu ikachukuliwa vizuri na kurudishwa na mchujo ukafanyika, Mungu bahati jina langu na la ndugu Majondo Miligwa yakarudishwa kugombea Uenyekiti wa Serikali ya wanachuo.Mwalimu Mboka Mwambusi akatuunganisha na wafanyakazi wa taasisi za Umoja wa Mataifa (UN) na UNHCR wakati huo kwani Kigoma ilikuwa na kambi nyingi za wakimbizi, kwa hiyo vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania, wengi walikuwa ni marafiki wa Mboka Mwambusi, Mboka akaniungasha na dada mmoja aitwaye Salama dada mmoja mrembo sana wa Kimatumbi akifanya kazi UNHCR ya Bi Sadako Ogata. Binti Salama akanihakikishia usalama wa kushinda akanipa pesa na pahala pa kuchapisha karatasi hizo, huku akitusaidia kutengeneza viperushi bora bure.


 

Katika watumishi hao wa taasisi za kimataifa nilikutana na mwalimu wangu wa Tambaza aliyenifundisha kidato cha kwanza Physics aitwaye Gemino alitufundisha mada moja tu ya Vernier Caliper Reading mwaka 1991, tukiwa Tambaza Mwalimu Gemino aliacha kazi ya ualimu na kusomea masuala ya fedha na mwaka 2002 akawa anafanya kazi na GTZ kama mtaalamu wa masuala ya fedha na yeye alinisaidia zaidi, Mwanakwetu nikawa Lodi.

Mwalimu Gemino akisema,

 

“Huyu bwana mdogo ni mwanafunzi wangu msaidieni maana nimemsomesha Tambaza.”

 

Uchaguzi ulipofanyika Mwanakwetu alishinda kwa kura nyingi tu. Uongozi huo tulijitahidi kufanya kazi huku tukikumbana na changamoto kadhaa lakini tukipambana nazo, tukafunga chuo na kurudi nyumbani, baada ya likizo kwisha tulirudi chuoni tena kuendelea na masomo na kumalizia chuo na uongozi wetu ili kuwakabidhi wengine.

Uongozi wowote haukosi changamoto,

 

“Tuliporudi chuoni mwanafunzi mmoja alipata changamoto ya ujauzito na kwa utaratibu wa vyuo vya ualimu wakati huo ilikuwa ni kosa kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi na japokuwa baadhi ya wanachuo walikuwa mafunzo kazini walikuwa na ndoa wapo wanafunzi wachache waliokuwa wameolewa nadhani walikuwa wanapaswa kujizuia kupata ujauzito wakiwa chuoni, sikujaliwa kuwaona wakiwa wajawazito kwa kuwa wanachuo wote walivaa sare kama wanafunzi wa shule za msingi au sekondari na sheria ya chuo ilikataza ujauzito. Mwanachuo huyu wa ujauzito aliubaini baada ya kukaa chuoni, je anafanyaje? Je anakimbia chuo alafu aseme anaumwa alafu aje kurudia mwaka mwingine, angoje kufukuzwa chuo? Au anautoa ujauzito huo?”

 

Jambo hili alishirikishwa Mwanakwetu kama kiongozi wa serikali ya wanachuo na yeye akazungumza na mwadili wa wanachuo ambaye alikuwa mwanamke. Mwadili alisema maneno haya,

“Kwa kumsaidia mama huyu basi achague kurudi nyumbani kwa kuwa hawezi kuingia akili mwalimu tarajali anasoma huku akiwa amebeba mimba na amevalia sare zake za chuo?Huku sheria za chuo zinakataza hilo, Je wanachuo wengine mabinti wanajifunza nini? Huku mwezi mmoja umepita wanachuo kadhaa walifukuzwa kwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi?”

 

Jambo hilo lilikuwa gumu na mzigo huo ni wa Mwenyekiti wa Serikali ya wanachuo, nyuma ya pazia mwadili alimshirikisha Mkuu wa Chuo huku mwadili akieleza msimamo wa Mwenyekiti wa Serikali ya wanachuo kuwa mwanachuo huyo asifukuzwe, amalize masomo yake.

 

“Hali ilikuwa tete huku bwenini rafiki wa Mwanakwetu anayefahamika kama yangu Stanley Nkambwe ambaye sasa ni Afisa Mkubwa wa Benki moja ya Biashara nchni Tanzania akisema haiwezekani dada yake huyu akafukuzwa chuo kwa kuwa mjamzito na sisi ni watu wazima na ameolewa.”

Utaratibu ulikuwa kabla yakufukuzwa mwanachuo kwa kosa lolote kamati ya nidhanu ya Serikali ya Wanachuo inakaa kulijadili na kuandika mapendekezo ya kamati hiyo na kabla ya kuketi Mwanakwetu alizungumza na mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye alikuwa Waziri wa Nidhamu na Sheria wa Serikali ya Wanachuo Symphorian Morandi(Muha wa Kigoma).


 

Tulijadili jambo hilo wawili na kukubalina kuwa huyu dada ameolewa na ana watoto wawili katika ndoa yake, shida ni kanuni na sheria za chuo mwanachuo hawezi kuingia darasani na sare za chuo akiwa mjamzito na nia ilikuwa kulinda maadili na kuwalinda wale wanachuo wengine wanaosoma chuoni hapo ikitarajiwa kila anayesoma chuo hicho alikuwa akitokea aidha kidato cha nne au kidato cha sita. Mjadala ulikuwa, huyu mwenzetu lazima atafukuzwa na kamati ya nidhamu ya serikali ya wanachuo lazima kulinda kanuni hizo viongozi wa wanachuo wote wamekula kiapo mbele ya hakimu wa wilaya kuzilinda sheria na kanuni hizo kuzipinga ni kujifukuzisha chuo mwenyewe.

Tulikubaliana kamati ikikaa iandike kwa kuwa mwanachuo huyu muda umekaribia wakufanya mtihani abaki kufanya mtihani huo na nakala ya cheti cha ndoa alichotuma mumewe kwa EMS kikiambatanishwa. Mwanakwetu na Morandi tukakubaliana zaidi kwa kuwa Morandi alikuwa na kaka zake mapadri katika Jimbo Katoliki la Kigoma tutakwenda kumueleza Baba Askofu Paul Ruzoka wa Jimbo Katoliki la Kigoma wakati huo kama maji yakizidi unga. Lakini tutaenda kwa Baba Askofu kwa hoja gani? Majibu yalikuwa haya,

 

“Huu utaratibu unashawishi wasichana wanaopata ujauzito ambao hawajaolewa na hata waliolewa wakiwa chuoni watoe mimba na kwa kuwa mkuu wa chuo alikuwa mkatoliki tutamshinda tu na kwa hilo na chuo tutamaliza salaam, tulijitia moyo.”

 

Mapendekezo yalipelekwa kwa mkuu wa chuo na yeye kumuita Mwanakwetu ofisini kwake, tukiwa wawili tu akisema,

“Kweli mwenyekiti umefanya kazi vizuri, sasa tunakuja kushindana mwishoni? Kweli mnatetea hili wakati sheria na kanuni zetu na maadili ya vyuo vya ualimu ndiyo hayo. Mimi Mkuu wa Chuo ninaposhindana na Mwenyekiti wa Serikali ya Wanachuo tafsiri yake katika uongozi siyo nzuri, hata tukiwafukuza viongozi wote wa Serikali ya wanachuo kwa msimamo huu katika hili tafsri yake ya kiutendaji kwa wanaokipima chuo chetu kitapata alama mbaya, kweli tunamfukuza Rais wa Serikali ya wnachuo? Nyinyi ninawaombeni mrudi mkauandike muhtasari huu upya.”

Kweli nilitoka na kumshirikisha Symphorian Morandi, sasa tunafanyaje ? Wakati tunajadli hilo mara nilipewa taarifa kuwa ninahitajika kwa Mkuu wa Chuo. Nilifika ofisini kwake ambapo ni mara chache mno kwa wakufunzi au wanakurufunzi kuingia humo.

“Mwenyekiti tunakufukuza kabisa, utarudi nyumbani kwenu Dar es Sa Salaam, mwenyekiti tunakupoteza …ehee muhtasari mmeshauandika upya?”

Nilijibu kuwa bado lakini tunauandika, akanimbia kaundike haraka sana.Hapo tukaitana watu kama saba hivi na kuelezana kilichopo na msimamo wa mkuu wa chuo na kuwaeleza msimamo wetu , huku hali ilizidi kuwa tete na sasa muda wa kumshirikisha Baba Askofu Paul Ruzoka uliwadia.

Chuo cha Ualimu Kasulu ilikuwa ni taasisi mojawapo kubwa ya serikali kwa mkoa wa Kigoma na kwa Jimbo Katoliki la Kigoma wakati huo. Tukifikiria kumuona paroko wa Kasulu Mjini au Padri Gaspa Balimkumtwa ambaye mimi nilikuwa namfahamu wakati akiwa Paroko Msaidizi Parokia ya Makere ili atuombee kwa Baba Askofu Ruzoka tukamuone.

Kikao hicho ambacho kilikuwa na wajumbe wa kamati ya nidhamu ya serikali ya wanachuo Mwanakwetu siyo mjumbe bali nilikutana nao kuwaeleza msimamo wangu kama mwenyekiti wao na tukakubalina tukutane jioni kuyamaliza mazungumzo haya.Tulipotoka tukala chakula cha mchana majira ya saa 11 jioni Mkuu wa Chuo akaniita akaniuliza, akisema,

“Mwenyekiti inaonekana mnagoma kuandika upya muhtasari na mnajipanga kumuona Baba Askofu Ruzoka? Hii siyo taasisi dini hii ni taasisi ya umma.”

Hapo Mwanakwetu nikatambua kuwa katika kikao kile yupo mmoja wetu anafikisha taarifa kama zilivyo kwa Mkuu wa Chuo, Mkuu wa Chuo akasema,


“Nahitaji muhtasari sasa hivi.”

 

Nilipotoka tu kumbe muda huo huo Mkuu wa Chuo Alphonce Mbonigaba aliagiza dada mjamzito aitwe kwa mwadili wa wanachuo na kuambiwa atasoma tu na kufanya mtihani, asiwe na shaka yoyote na asome kwa amani. Baadaye nilijulishwa kilichotokea na mwadili wa wanachuo, Mkuu wa Chuo Akasalimu Amri.

Tuliendelea na masomo vizuri sana na wakati wa mahafali ya Wanachuo Wakatoliki Baba Askofu Paul Ruzoka alifika Chuo cha Ualimu Kasulu na kufanya misa nasi huku tukipiga naye picha za kumbukumbu, naye Mkuu wa Chuo akishiriki misa hiyo, akidhani fika kuwa wafitini akina Mwanakwetu walishamuona Baba Askofu Ruzoka kumuelezea kilichotokea kumbe sisi tulikuwa ndiyo tunajipanga kwenda kumuona Baba Askofu Paul Ruzoka.

Mwanakwetu tulimaliza chuo hiki sote na dada huyu alirudi kwa mumewe na kujifungua salama na mtoto wake sasa anakaribia miaka 20. Mwanakwetu anatambua kisa hiki mtoto huyu anaweza akakisoma, akidhani anasimuliwa mtu mwingine kumbe ni yeye, nina hakika mama wa mtoto huyu hawezi kumsimulia mwanae tukio hilo labda katika hali ya hasira. 


 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Katika maisha ya binadamu kila mmoja ana udhaifu wake lakini ni jambo la msingi sana kwa kila binadamu kuwa na hofu ya Mungu kwanza, ndipo mambo mengine yafuate iwe kanuni au sheria kwa kuwa na hofu ya Mungu ni zaidi ya vyote ambayo Mkuu wetu wa Chuo alikuwa nayo na ndiyo ikawa salama yetu sisi akina Mwanakwetu kinyume chake leo hii mimi, wezangu wote na huyu dada mjamzito tusingekuwa hata na cheti cha ualimu.

Mwanakwetu pia mkumbuke Mboka Mwambusi, Symphorian Morand, Stanley Nkamwe, Said Mhando, Hija Mashaka, Rashidi Ally , Seralini Sawa na dada yetu Salama (UNHCR), Mwalimu Gemino (GTZ), Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu wakati huo Alponce Mbonigaba, Padri Gaspa Balikumtwa, Paroko wa Kasulu Mjini na hata Baba Askofu Paul Ruzoka tulivyolitumia jina lake na cheo chake kukamilisha ajenda yetu na tukafanikiwa.

Katika maisha namna yalivyo inawezekana huyu kijana wa dada yetu mwenye miaka 20, sasa anaweza akakutana na mmoja wa hao au hata ndugu za hao wote hapo juu akawafanyia kitu kibaya sana bila ya kufahamu kuwa yeye amezaliwa kwa kuwa hawa ndugu hawa walifanikisha jambo kwa mzazi wake akiwa mjamzito akiwa tumboni kwa mamaye.

Jamani tuhifadhi kumbukumbu ya matukio tunayopitia. Nimalizie pia kwa kusema kuwa usione unazaliwa tu tambua wazazi wako wamepitia magumu mengi hadi wewe ukazaliwa duniani, waheshimu mno wazazi wako na kila unayemuona katika dunia. Kwa wale wanaopata uongozi kwa kupigiwa kura wabebe mizigo ya wapiga kura wao wasikwepe hilo kama wanakwepa hilo basi hakuna haja ya wao kugombea nafasi hizo.

Mwanakwetu upo?

Kumbuka,

“Mkuu wa Chuo Akasalimu Amri.”

Nakutakia Siku Njema.

makwadeladius @gmail.com

0717649257


 

 

0/Post a Comment/Comments