UKIJA NITAKUPISHA


Adeladius Makwega-MBAGALA

Ilikuwa wakati wa Likizo ya mwezi wa sita mwaka wa 1991, Mwanakwetu na rafiki yake mmoja(MGAZA) waliyokuwa wanasoma naye Tambaza Sekondari, siku hiyo waliamua waiwashe Daladala ya Wakati huo (Chai Maharage) waende nayo Mtongani wapakie abiria hadi Kimanzichana wapate pesa kwa kubeba abiria, maana mifuko yao ilikuwa haina kitu. Kweli walifanya hivyo na kupakia abiria hadi Kimanzichana Mwanakwetu akiwa utingo kwa kubabia, walipofika hapo wakawa wanasubiri abiria wa kurudi nao Mtongani.

Wakati wapo stendi, Mama LILANGA (MKE MKUBWA) Mama mmoja wa Kimakonde alishuka katika gari lingine linalotokea Dar es Salaam akamsalimu Mwanakwetu akasema,

“Wewe mkina Makwega , huku unafanya nini? Hujui kwenu kuna msiba? Binti Makwega amefariki, rudi nyumbani kwenu haraka ukazike, nimesikia kwenye taarifa ya habari.”

Mgaza akampa Mwanakwetu pesa kiasi ili Mwanakwetu arudi nyumbani Mbagala kwa basi zinazotoka Kibiti, Lindi na Mtwara ili awahi msiba ili awahi kuzika.

Nakuomba msomaji wangu ufahamu ili , utoaji wa taarifa wakati huo ulikuwa wa mtu na mtu au mtu na barua na ndiyo maana redio ilifanya kazi nzuri sana, japokuwa Simu za mezani zilikuwepo lakini kwa watu wachache mno waliyokuwa na uwezo, kwa Mbagala Sabasaba nyumba iliyokuwa na simu ni kwa akina Nkunga jirani na Chura Hana Mbavu-Sabasaba Magegeni kando na George Bush Baa. Mwanakwetu akapanda Basi la Akida na akafika kwao Mbagala salama salimini na kuelezwa aliyefariki, Msiba upo Kichanga Chui(Msasani) na mazishi yatakuwa kesho yake Makaburi ya Kinondoni awali yatatanguliwa na Misa itakayofanyika Kanisa la Mtakatifu Petero Oysterbai.


 

Maelekezo kutoka kwa akina Makwega yalikuwa wale wote watoto/wanafunzi/vijana wote wa huu Ukoo ambao wanasoma wakati wa likizo, siku ya mazishi wasiende shuleni, wawepo nyumba yenye msiba na wale wanaofanya kazi waombe ruhusa waende kumzika ndugu yao. Siku ya kuzika ilifika nayeye Mwanakwetu alifika Kichanga Chui msibani. Watu walikuwa wengi, hapa msibani kililika chakula vziuri, kisha wakawa wanafika viongozi wengi wa Chama, Serikali na Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mwanakwetu kafiwa, jamaa wanaosoma na Mwanakwetu Mgaza kawaambia Makwega kafiwa , wengine wanasema Makwega kafiwa na dada yake, wengine wanasema yule siyo dada yake, yule shangazi yake, sisi Kazimbaya tunamjua , yule bwana mdogo anazaliwa tunamjua tangu anasoma Shule ya Msingi Mnazi Mmoja. Vijana wa Tambaza wakakusanyana na ile cha Chai Maharage yao naambiwa wakaja Kichanga Chui Msibani, wakapaki jirani na nyumba ambayo alikuwa anakaa Jaji Augustino Ramadhani wakati huo. Mwanakwetu hajui kama hawa jamaa wamekuja na inavyoonekana walizuiwa huko kwa kuwa hapa msibani magari yalikuwa mengi, njagu(askari) wengi viongozi wengi wakubwa kwa wadogo wanakuja kuzika, hawa jamaa na Chai Maharage wakazuiliwa.Mwanakwetu yu msibani kasimama kakunja mikono, hajuia kama jamaa zake wamekuja, katika viti walikuwa wamekaa ndugu wengi, wakubwa na wadogo. Baba yake Mwanakwetu Mwalimu Francis Makwega akasema kwa ukali,

“Nyie watoto wadogo kwanini mnakaa katika viti wakati kaka yenu Adeladius (Mwanakwetu) kasimama?”

Miongoni mwao aliyeambiwa maneno haya alikuwa ni Modestus Makwega mdogo wa Mwanakwetu anayemuachia ziwa, hapo Mode akasimama na kumpisha Mwanakwetu kuketi kitini. Gafla kundi la vijana wa Tambaza wamefika wale waliokuja na Chai Maharage, wamevaa kaptura zao za Polista grei juu mashati na wengine fulan, wakafika wengi wakampa pole Mwanakwetu na Baba yake maana wengine walikuwa wanamfahamu mwalimu Francis Makwega ambaye aliwasomesha Shule ya Msingi Bunge.

“Mwalimu Makwega pole sana, huyu Kazimbaya tunasoma naye.”

Mwanakwetu ikabidi aamke katika kiti na kurudi nyuma kabisa kabisa ili aongee na hawa rafiki zake aliyokuwa anasoma nao kidato cha Kwanza Tambaza Sekondari wakati huo wakiongozwa na Edwin Kachenji. Mwanakwetu wakati anasimama Modestus Makwega akakaa tena kitini akasema,

“Kaka Adeladius Ukija  Nitakupisha.”

Kundi hili la wanafunzi wa Tambaza likarudi nyuma kabisa na Mwanakwetu kwenye fensi jirani na nyumba aliyokuwa anakaa Kanali Nsa Kaisi ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa katika mikoa mingi ya Tanzania Bara. Tukiwa nyuma pale Mwanakwetu akaenda jikoni kuwaombea chakula hawa jamaa wakaletewa chakula kingi katika sufulia kubwa wakala vizuri walipomaliza dada mmoja mfipa aliyekuw anasoma Jitegemee Sekondari akachukua sufulia akabeba na kurudi nalo jikoni, vijana wa tambaza wameshiba wali wakawa wanapiga stori gafla likaji gari moja hadi jirani na Uwanja wa Msiba akashuka Jamaa mmoja na jamaa wengine wawili huku akasalimiana na watu kadhaa walio mbele msibani huyu jamaa akawa anaongea na Segera Mswima na jamaa wengine kando. Kundi la Mwanakwetu wale vijana wa Tambaza kijana mmoja mkazi wa Kinondoni akasema mnamjua Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa?Jamaa wakawa na shuhuku ya kumjua.


 

Jamaa wakawa wanamuonesha kidole, yule, yule pale, yule bwana, Yule ndiye ndiye Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa(wanasema kwa sauti ya chini). Vijana wa Tambaza wakawa wanaendelea Kumsonda Kidole Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, kando huyu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa alikuwepo Jamaa mmoja Bonge kava shati hajachomekea kavaa na tai juu. Vijana wa Tambaza wanacheka , hapo hapo huyu Kijana Yule wa Kinondoni akasema ngoja niwape stori,

“Siku moja Imrani Kombe- Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa alikwenda kikaoni, hapo kikaoni watu walikuwa hawamjui, alipofika hapo mmoja wa msaidizi wake bonge akashuka na Briefkesi kisha akaingia ukumbini, ukumbi mzima ukasimama, kumbuka jamaa hawamjui wakaisi msaidizi bonge ndiye Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa. Huu ukumbi kwa bahati mbaya haukuwa na milango ya pembeni, yaani unaingia ukumbini kama vile mtu anayeingia Kanisani kwa mlango mkubwa wa kanisa, huyu msaidizi kuimbuka kaingia Briefikesi , jamaa ukumbi wakasimama wakijua Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa anaingia ukumbini, jamaa kafika mbele akaweka Briefkesi akawa anatoka kumfuata bosi, hapo ndipo ukumbi ukatambua kuwa huyu jamaa bonge hakuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, baadaye Afande Imrani Kombe ndiyo akaingia ukumbini kuendelea na kikao chake.”

Msomaji wangu kumbuka Mwanakwetu yu msibani, baadaye tukasikia Ving’ora akafika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati huo marehemu Ali Hassan Mwinyi akatoa pole kwa wafiwa wote akaaga mwili nayeye kisha kuondoka zake. Baadaye watu wengine wakaaga mwili kisha mwili kubebwa hadi Kanisa la Mtakatifu Petero Oysterbai .

 


Mwanakwetu na jamaa zake wa Tambaza wakasema sisi twende moja kwa moja makaburi ya Kinondoni Mkwajuni, tusipite Kanisa maana tukipita kanisani makaburini tutafika wamwisho viongozi wako wengi, kweli ilikuwa hivyo.Tulifika Kinondoni Mkwajuni mapema sana, tukapaki Chai Maharage yetu na baadaye waliokuwa kanisani walifika makaburini na kuanza ibada ya mazishi, ambapo Waziri maarufu Msibani alikuwa ni marehemu Augusitine Lyatonga Mrema.


 

Tukazika kisha kurudi zetu Mbagala.

Mwanakwetu siku ya leo anasema nini?

Makala haya yametayarishwa na Mwanakwetu kwa sababu nyingi sana lakini siku ya leo nakupa sababu tano, tano tu; kwanza kwa heshima ya Afande Imrani Kombe ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa wakati huo maana wengi wanamkumbuka Imaran Kombe na tukio lake lile la kudunguliwa na risasi na Askari kutoka Kituo cha Oystebai na ndipo alipofariki dunia. Pili makala haya yametayarishwa na Mwanakwetu kwa heshima ya Bi Honesta Fidelis Makwega, tatu makala haya yametayarishwa kwa nia ya kubaki kama Kumbukumbu ya familiam na nne maana huyu Binti Makwega mwaka huu anatimiza miaka 34 kaburini Raha ya Milele Uupe Ee Bwana na Mwanga wa Milele umuangzie, Apumzike kwa Amani Amina na sababu ya mwisho Mwanakwetu anaudhihirishwa umma wa Watanzania kuwa simulizi juu ya Idara ya Usalama zinaweza kuandikwa na jamii ikajifunza mengi kutoka Idara hii muhimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wakati wa harakati za ukombozi wa Bara la Afrika Idara hii ilifanya kazi nzuri sana ikishirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi la Usalama vya Tanzania na mataifa mengine yaliyounga mkono harakati hizo.


 

Mwanakwetu anapongeza Watanzania wote waliowahi kufanya kazi na idara hii na wale wanaofanya kazi na idara hii hivi sasa lakini. lakini lakini wale wazalendo tuu.Mwanakwetu upo? Je makala haya niyaitaje? Sonda Kidole Mkurugenzi Wa Idara au Kaka ukija nitakupisha,? Mwanakwetu anachagua Kaka Adeladius Ukija Nitakupisha.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257 




 


 







 

 

 

 

 



0/Post a Comment/Comments