Adeladius Makwega-Musoma MARA
Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Mwalimu Gerald Msabila Kusaya amesema kuwa walimu nchini Tanzania ni kiungo muhimu katika maendeleo ya taifa hili, hivyo Serikali ya Awamu Sita itaendelea kuwa begabega na walimu wote nchini Tanzania kutoka shule Binafsi na za Umma ili kufikia shabaha yake ya kumuinua Mtanzania na kumuuongoza mwanafunzi kufikia ndoto zake.
Haya yamesemwa Wilayani Musoma, Mkoani Mara na Mwalimu Kusaya wakati akifungua Kikao cha Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) kwa Kanda ya Ziwa kilichojumuisha mikoa mitatu; Mwanza, Geita na Mara Mei 29, 2025.
“Muda wote walimu mpo shuleni, mnawalea watoto wetu, kikao hiki mkitumie kubadilishana uzoefu wenu hasa kwa madarasa ya mitihani ili Kanda ya Ziwa Ifanye vizuri.”
Mwalimu Kusaya aliongeza kuwa kuinua taalama ndilo kusudio letu katika shule Binafsi na za Umma maana Wakuu wa Shule ndiyo wasimamizi wazuri wa walimu na kufanya vizuri kitaaluma na hata kimichezo siyo kwa ngazi ya kanda tu bali shabaha yetu sote iwe katika ngazi ya kitaifa.
Akijibu risala ya TAHOSSA Mwalimu Kusaya alisema kuwa shule nyingi zina changamoto ya uhaba wa walimu akisema tatizo la uhaba wa watumishi siyo la walimu peke yao mathalani Mkoa wa Mara una upungufu wa watumishi 15,441 lakini Serikali italitatua jambo hili lakini Wakuu wa Shule muwe wabunifu kukabiliana na uhaba walimu kwa kutumia walimu wa muda mfupi wakati tatizo la uhaba wa walimu wakati linafanyiwa kazi kwa wamiliki wa shule iwe binafsi au za umma.
Akilichambua suala hili la uhaba wa walimu alisema changamoto kubwa ni idadi ya watu inapoongezeka na uhaba wa watumishi unaibuka hatuwezi kusema Watanzania tusizaliane ndiyo maana sisi Serikali tunakabiliana nalo kwa kutoa ajira mpya kila mwaka.
Katika hili Serikali ya Dkt .Samia Suluhu Hassan inajitahidi mno, maana sasa miradi ya elimu ni mingi ambapo wananchi hawachangii chochote.
“Pongezi tele tumpatie Rais wa Awamu ya Sita Dkt. .Samia Suluhu Hassan.”
Mwalimu Gerald Msabila Kusaya sambamba na hayo yote aliagiza yafuatayo;
“Kuhakikisha kila shule watoto/wanafunzi wale chakula cha mchana shuleni kwa ushirikiano wa Kamati za Shule, Wazazi na Viongozi na kufanikisha hili zitumike sheria ndogondogo. Pia ninahimiza wazazi kuwatunza watoto wao maana ni matunda ya wazazi kuwa pamoja,
Wadhibiti ubora wa Elimu wafanye kazi vizuri ili kuboresha elimu, ninawaomba mpambane na utoro shuleni ni haki ya mtoto kuhudhuria masomo kila siku, ninaomba msimamie mazoezi ya kujifunza ya wanafunzi yanafanywika vizuri na kwa wakati walimu wezangu msahihishe kazi zote za wanafunzi ikiwamo mitihani ya wiki, mwezi na mihula ili kusaidia wanafunzi wafaulu na mwisho Wakuu wa Shule za Serikali simamieni miradi yote kwa umakini, ninawapongezi maana sasa Wakuu wa Shule wengi mnafanya vizuri na mmekuwa mahiri sana katika kuisimamia miradi hii.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAHOSSA Kanda ya Ziwa alisema kuwa anaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa Maboresho ya Elimu kwa kutoa Posho ya Madaraka na Kutoa Elimu Bure tangu Shule ya msingi hadi Sekondari alinadi kuwa ,
“Kumekuwa na ongezeko la walimu wanaopata kazi, kulipwa madai mbalimbali, kumetengenezwa mazingira mazuri kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu na maboresho kadhaa ya mitaala . “
Mwenyekiti huyu wa TAHOSSA Kanda ya Ziwa alikula kiapo mbele ya Katibu Tawala Mkoa wa Mara kuwa wataongeza nguvu ya kuhamasisha umma juu ya upatikanaji wa Chakula cha Mchana shuleni ili kuongeza ufaulu na kupunguza utoro.
Kikao hiki kiliambiwa kuwa TAHOSSA Kanda ya Ziwa itahakikisha wanaendeleza ushirikiano baina yaoa na serikali na kuongeza mafanikio zaidi ya kielimu na michezo ambapo kanda hii inafanya vizuri katika michezo ya Shule za Msingi na Sekondari.
Katika kikao hicho Wakuu wa Shule walipata nafasi ya kuwakumbuka Wakuu wa Shule waliopandisha ngazi mbalimbali na wengine waliofariki katika kipindi cha hivi karibuni. Kikao hichi kiliwakutanisha Wadau mbalimbali wa elimu hasa wale wa mifumo ya elimu, Wakuu wa Shule kadhaa, Maafisa Elimu kutoka Halmashauri zote Kanda ya Ziwa, Maafisa Elimu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na viongozi wengine wa Elimu wa Mkoa wa Mara, Mwanza na Geita
Uzoefu ulitolewa na Walimu ambao ni Wakuu wa Shule kwa Muda mrefu ambapo ulitolewa ushauri namna bora ya Wakuu wa Shule kuwalea vizuri walimu wageni ili wasiijiingize katika mambo mabaya, pia wakuu wa shule walikumbushwa kupambana na tabia mbaya ya mahusiano ya kimapenzi baina ya walimu na wanafunzi wakisema hilo siyo sahihi huku Wakuu wa Shule waishi vizuri na walimu wanaowaongoza,
“Mkuu wa Shule lazima ajenge mahusiano mazuri kazini lazima muwe na malengo ya pamoja.”
Kwa upande wake mwalimu mzoefu Manyansi Rupia alisema,
“Mkuu wa Shule ni kiongozi wa Serikali na anaiwakilisha Serikali , kwa hiyo kila unalolitenda lazima kuzingatia nyaraka na miongozo ya Serikali, jitahidi kupokea wageni vizuri na Mkuu wa Shule awe makini na kauli zake zote zinazotolewa . Huku Mkuu wa Shule ni kiunganisha baina yake na jamii na viongozi.”
Katika kikao hicho pia ilitolewa mada ya matumizi mazuri ya lugha na kuacha kutoa lugha za kihuni ambazo zinakera, hilo linaweza kuleta shida kwa walimu na wanafunzi, tutumie lugha ya unyenyekevu.
“Unapotumia lugha ya kushauri shauri, unapokemea kemea na kila Mkuu wa Shule awe na lugha ya utaratibu na upole, baadhi ya lugha zinavunja moyo maana mwalimu ni mlezi na mwalimu ni kiongozi , ukiwa na lugha nzuri zinajenga na kuwalea walimu wenzako waweze kuja kuwa viongozi wazuri hapo baadaye, huku Wakuu wa Shule mkubali kupokea ushauri.
Kikaoni Mkuu wa Shule kuwa mzungumzaji wa mwisho baada ya walimu wako na watumishi chini yako kuongea ndipo na wewe uongee.”
Jambo ambalo liliibua mjadala mkubwa katika mkutano huu wa TAHOSSA ilikuwa bei ya Mfumo wa Kietroniki ya Elimu ambapo mtoa mada alisema kuwa mfumo wao unauzwa shilingi za Kitanzania milioni 20, kelele za Wakuu wa Shule zilionesha kuwa bei ya mfumo huo ni kubwa lakini taafifu ya bei ya mfumo huo ipo maana waliambiwa wanaweza kushusha kwa mdau kununua sehemu ya mfumo huo tu, mathalani mfumo wa matokeo peke yake.
Kikao hiki kiliwakutanisha Viongozi wa Elimu Karibu mia tano.
Mwanakwetu upo?
Kumbuka,
“Tumuongoze Mwanafunzi Kufika Ndoto yake.”
Nakutakia siku njema.
0717649257
Post a Comment