
Adeladius Makwega-MBAGALA
“Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini. Hawa akasema, ‘Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!’ Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima. Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani, naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na sadaka yake, lakini hakupendezwa na Kaini wala na sadaka yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana. Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, ‘Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana? Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.’ Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, ‘Twende nje shambani’ Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, ‘Ndugu yako Abeli yuko wapi?’ Kaini akamjibu, ‘Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?’ Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Umefanya nini? Damu ya ndugu yako yanililia kutoka udongoni. Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua. Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.”
Mwanzo 4,1-12.
Mwanakwetu katika kisa hiki yapo maswali mengi , Je Kaini baada ya Kumuuwa Abeli alikuwa anamuhofia nani? Katika Mwanzo 4: 13-14, muda mfupi baada ya kumwua ndugu yake Abeli,
"Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imekuwa kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua."
Mwanakwetu anajiuliza je ni nini hasa Kaini alikuwa anahofia?
Watu pekee ambao kitabu cha Mwanzo kilichowataja hapa ni Adamu na Hawa (wazazi wa Kaini) na Abeli (ambaye alikua amekufa sasa). Je nani angeweza kuwa tishio kwa Kaini? Hapa msomaji wangu ni muhimu kutambua kwamba Kaini na Abeli walikuwa ni watu wazima wakati Kaini akimuua Abeli. Wote wawili Kaini na Abeli walikuwa wakulima ambao walikuwa wanatunza ardhi yao na kundi la mifugo yao rejea Mwanzo 4: 2-4. Biblia haituambii umri wa Kaini na Abeli, lakini kuna uwezekano mkubwa kuwa walikuwa katika miaka yao ya 30 au 40 yaani vijana wenye nguvu ya kufanya uzalishaji mali.
Biblia haitaji kwa uwazi Adamu na Hawa kuwa na watoto kati ya Abeli na Seti rejea Mwanzo 4:25.
Hata hivyo, haiwezekani kwamba watu wawili kamilifu katika historia ya dunia, Adamu na Hawa, hawakuwa na watoto zaidi ya miongo kadhaa. Mwanakwetu anaamini kuwa Adamu na Hawa walikuwa na watoto wengi baada ya Seti rejea Mwanzo 5: 4, kwa nini hawakuwa na watoto wengine kati ya Abeli na Seti?
Biblia haisemi kwamba Seti alikuwa mtoto wa kwanza wa Adamu na Hawa, au hata mwana wa kwanza, baada ya Abeli kuuawa. Badala yake, inasema kwamba Seti alizaliwa kama "mbadala" kwa Abeli. Mwanzo sura ya 5 huelezea ukoo wa Seth. Kabla ya kifo chake, Abeli alikuwa mwana "aliyechaguliwa" ambaye hatimaye hatakuzaa Masihi rejea Mwanzo 3:15. Kwa maana hii Seti "amechukua nafasi" ya Abeli. Kwa hiyo, Kaini alikuwa anamuhofia nani?
“Kaini alikuwa na hofu ya kaka zake, dada, wapwa wake ambao walikuwa wamekwisha zaliwa na walikuwa na uwezo wa kulipiza kisasi na walitambua kilichotokea. Ukweli kwamba Kaini alikuwa na mke rejea Mwanzo 4:17 ni ushahidi zaidi kwamba Adamu na Hawa walikuwa na watoto wengine baada ya Kaini na Abeli, lakini kabla ya Seti.”
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Tanzania ya sasa inashuhudia matukio ya kutekwa, watu kuumizwa, watu kudhalilishwa na hata watu kuuwawa, Swali lile lile lililoulizwa kwa kaini tujiulize hapa, wale wanaoshiriki matukio haya wanahofu yoyote? Jibu lake lazima wawe na hofu? Tena hofu kubwa.
“… hofu ya kaka zake, dada, wapwa wake ambao walikuwa wamekwisha zaliwa na wana uwezo wa kulipiza kisasi na wanatambua kinachotokea…”
Kwa hali hii ya sasa Watanzania wana hofu ya kutekwa, na watekaji wana hofu ya kujulikana, hali ikoje je wao watakuwa salama? Iwe leo, iwe kesho. Mtekaji hofu na Mtekwaji hofu, katika hali kama hii ni vigumu watu kuwa wamoja, kuwa pamoja na kufanya shughuli za maendeleo, kila mmoja anamuhofia mwenzake. Watu wenye hofu hawawezi kushiriki vizuri shughuli za maendeleo na ndiyo maana Mwanakwetu kama mwanaCCM bado anashauri CCM itazema kwa sasa hasa jina la Mgombea wake wa Urais bado CCM inayo nafasi maana kwa tathimni ya utekelezaji wa ilani juu ya Utawala Bora na Ulinzi na Usalama kuna kasoro tele,.kasoro kubwa.
Kwa hakika nchi inaumwa , inaumwa hofu , CCM ndiyo daktari, tusimuogope Jakaya Mrisho Kikwete maana yeye ndiye kiongozi mkubwa aliyebaki kwa ngazi ya juu, leo Mwanakwetu ninamwambia nchi inaumwa, inahitaji dawa, ili mgonjwa apone ili ipone na makala haya ni sehemu ya ushauri, ili taifa letu lipone, watu tuna hofu, CCM ndiyo tabibu.
Jakaya Kikwete ni ndugu yetu, tunamueleza ukweli hili suala umekuwa kimya, haulizungumzii baba kabisaaa , watu tunalia mioyoni. .Jakaya Kikwete hajapingua udugu na sisi maana wewe anayo nafasi nzuri ya kushauri zaidi yetu sote iwe kwa Serikali na iwe kwa CCM.
“Shida ni kutoa majibu juu ya watu wasiojulikana, kuwakamata wahusika na hata kuzuia vitendo hivi vyote, imeshindikana?”
Kwa hakika shida ya dunia ya leo siyo kwa wale wanaoteka watu , shida siyo kwa wale wanaodhalilisha watu, shida siyo kwa wale wanaowaua binadamu wenzao , Mwanakwetu shida ni moja tu kwa wale wanaoshuhudia vitendo hivyo na kukaa kimya.
Ndiyo maana Mwanakwetu bado anatoa pongezi tele kwa Baba Askofu Gwajima kwa kuona uovu na kuupigia kelele, wapo wanaoadhani kuwa Baba Askofu Gwajima anasema hayo kisa anataka ubunge tena kisa labda anautaka Urais , Mwanakwetu anaheshimu jamii ya watu wneye misimamo isiyoyumba kama wa Baba Askofu Gwajima tangu wakatia ya KOVIDI 19 maana ni Heri Mtu Yule Anayeuona Ubaya na Kuukemea.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya Mwanakwetu ayape kichwa gani? Mtekaji Hofu Mtekwaji Hofu? Au Heri Mtu Yule Anayeuona Ubaya na Kuukemea? Mwanakwetu siku ya leo anakuachiwa wewe msomaji wake uchague. Kumbuka tu Mtekaji Hofu na Mtekwaji Hofu.
Nakutakia Siku Njema
0717649257
Post a Comment