MKURUGENZI BUNDA VIJIJINI APONGEZWA

 


Adeladius Makwega-BUNDA MARA

Ni Majira ya Jioni ya Mei 20, 2025 sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara; Mary Daniel, Marwa Mathayo na Rhobi Samweli wakiwasili Wilayani Bunda kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Mara kwa Wilaya ya Bunda Vijijini.

Wageni hawa wanafika hapa na kukutana na wataalamu kutoka idara mbalimbali za Mkoa wa Mara wakiongozwa na wenyeji kutoka Halmashauri ya Bunda Vijijini na viongozi kutoka RUWASA ambayo ni Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini .

Mradi huu wa Maji upo ufukweni kabisa na Ziwa Victoria, wageni hawa wanakaribishwa na ripoti ya mradi inayosomwa na Injinia Leo Respicious ambaye ni Meneja wa RUWASA Wilaya ya Bunda.

“Mradi huu ni wa karibu shilingi za Kitanzania Milioni 557. 92 ambapo mpaka sasa mkandarasi amelipwa shilingi milioni 307.6. Mradi huu ulianza rasmi Januari 24, 2023 na unatarajiwa kukamilika Julai 24, 2025.”

Baada ya ripoti hii, wajumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mara walikuwa wakali kidogo na kuagiza Mkandarasi aongeze spidi kuhakikisha mradi huu unakamilika mapema na Chama cha Mapinduzi kitapitia tena kuukagua mradi huo Julai 2025, huku wakiagiza Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Bunda kufuatilia hili kwa karibu.


 

Kwa hakika Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara ilifarijika mno na miradi yote ya elimu iliyokaguliwa katika Wilaya ya Bunda Vijijini huku madiwani waliokuwepo katika miradi hiyo hii wakitoa pongezi kubwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Bunda George Stanley Mbilinyi, Watendaji wote na pongezi tele kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa pesa hizo na kuhakikisha pesa zote za miradi hiyo zinatumika vizuri kwa faida ya jamii kubwa ya Watanzania na sasa Watanzania wanapata manufaa.

Kwa hakika mwandishi wa makala haya alivutiwa mno na jiografia ya Wilaya ya Bunda Vijijini ambapo ilionekana kuwa ni eneo lote lililotembelewa na Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Mara hapa Bunda jioni hii ni kama sehemu ya ardhi iliyoingia ndani ya Ziwa Victoria.

Mjadala ndani ya gari alilopanda mtayarishaji wa makala haya ulikuwa sasa umefika wakati wa kurejesha huduma ya meli ambayo itakuwa inazunguka Ziwani Victoria kwenda Uganda, Kenya na Tanzania na ni lazima ifika Musoma na meli hii inaweza kuwa kivutio kikubwa cha utalii ndani ya Ziwa Victoria.


 

Msafara huu wa Kamati ya Siasa ulifika Bunda Mjini kupumzika ili Mei 21, 2025 kuendelea na ukaguzi wa miradi ndani ya Bunda Mjini.

Kumbuka;

“Pongezi Tele kwa Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257







 


0/Post a Comment/Comments