MAVUNDE ATEKELEZA AGIZO LA KATIBU MKUU CCM

Adeladius Makwega-Nyamongo MARA

Waziri wa Madini wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mhe. Anthony Mavunde amezitaka kampuni za madini kuwa na Kibali cha Mahusiano baina yao na wanajamii maana hicho ni kibali kikubwa kinachoweza kuzisaidia kampuni zinazomiliki migodi kufanya kazi vizuri na kuondoa migogoro baina yao na jamii kando ya migodi.

Hayo yamesemwa Mei 3, 2025 katika Mji wa Nyamongo Tarime Mkoani Mara ambapo Waziri Mavunde alikuwa akizindua mradi wa Uchimbaji wa Madini kwa Vijana zaidi ya 1736.

“Wapo baadhi ya wachimbaji walikuwa na leseni wanamiliki eneo kubwa vibali hivyo, vingi tumevifuta nia ya serikali ni kuvipanga vizuri kugawia vijana , akina mama, akina baba na watu wenye ulemavu.”

Akizungumza katika hadhara hii Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwalimu Mwita Waitara alimshukuru Waziri Mavunde kwa kufika Nyamongo, japokuwa alikuwa na majukumu mengi ya huko Wizarani Jijini Dodoma.

“Vijana wa Tarime Vijijini mliopata fursa katika vikundi hivi mtumie fursa hii vizuri, hata kama mtapata changamoto msirudi vijiweni changamoto hizo serikali itazitatua , msikate tamaa maana tulipotoka ni mbali.

Vijiji vinapata bilioni mbili za fedha za dhahabu, ninaomba fedha hizi mzitumie vizuri zisitumike  kuleta migogoro maana vipo vijiji havipati fedha hizo, viongozi wa vijiji tumieni fursa hii vizuri kwa kutumia mikutano halali ya vijiji.”

Akimalizia maelezo yake Mh Waitara alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi kwa kutatua kero kadhaa za watu wa Mkoa wa Mara ikiwamo katika Afya , Miundombinu , Elimu , Barabara na sekta zingine.


 

Akisoma risala ya mradi huo Mhandisi Amini Msuya ambaye ni Afisa Madini wa Kanda hii alisema kuwa Mkoa wa Mara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wamepangiwa kukusanya Bilioni 210 na wanahakika lengo hilo litafikiwa na shabaha ya mradi huu ni kuwapa vijana uwezo wao kuchimba madini wao wenyewe na kuondoa tatizo la vijana kuvamia mgodi ambalo hili lilikuwa linahatarisha amani ya Wilaya ya Tarime na Mkoa wa Mara.

“Mradi huu unawanufaisha vijana 1736 kutoka vijiji 13 ambapo leseni 106 zimetolewa, huku ugawaji wa leseni utaendelea kulingana na hali itakavyoendelea kwa kuwa mradi huu ni endelevu huku tukishirikiana na taasisi zingine, tunaipongeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara kwa kutupa ushirikiano mkubwa kwa hatua zote hadi leo hii yamekamilika.”

Hoja ya Mgodi mingi hapa Tanzania imekuwa ikiwekewa fensi jambo hilo liliibua hoja kuwa suala la mahusiano mazuri baina ya wamiliki wa migodi na jamii husika kando ya mgodi, katika mataifa mengine migodi haina fensi.


 

Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Alfred Mtambi akizungumza katika hadhara hii alisema kuwa anapokea pongezi zote zilizotolewa hapa kutoka kwa wananchi wa Tarime wakiongozwa na Mbunge wa Tarime vijijini lakini pongezi hizo zote ni za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ninawapongeza vijana wa mkoa wa Mara kwa kuwa wastamilivu na leo hii ndoto yenu imekamilika na mabilionea wapya Nyamongo wanakuja kupatikana hivi punde, kikubwa nakuomba Waziri tusiishea kutoa leseni bali tutoe na ujuzi wa kuchimba madini haya kwa tekinolojia ya kisasa. Huku ninaomba niwe mlezi wa hawa vijana maana nitatoa msukumo kwa pande zote zinazohusika, vijana msishiriki uhalifu.”

 

Uzinduzi wa Mradi wa Uchimbaji wa Madini kwa vijana unafanyika sambamba na Waziri Mavunde akitekeleza agizo la Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi alilolitolea Nyamongo Tarime Vijijini wakati wa ziara yake mkoani Mara kuwa waziri husika afike katika Mji huu na asikilize na kujibu baadhi ya hoja za wananchi wa Nyamongo ikiwamo mgawanyo wa mirahaba. Katibu Mkuu Nchimbi alitoa agizo hilo wakati akielekea katika maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26, 2025 Serengeti Mkoani Mara.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 













 



0/Post a Comment/Comments