Adeladius Makwega-MBAGALA.
Uchaguzi wa Baba Mtakatifu umekamilika huko Vatikani mapema Mei 2025 na kuchaguliwa Baba Mtakatifu Leo wa XIV, huku Jumapili ya Mei 11, 2025 baada ya uchaguzi huo imekuwa ni Jumapili ya nne baada ya Pasaka, Jumapili ya Mchungaji Mwema.
Katika mchakato huu wa kumpata Baba Mtakatifu wa sasa Mwanakwetu amekuwa katika lindi la tafakari kubwa ambayo leo hii inayajenga makala haya ya Mwanakwetu. Kwanza kabisa juu ya namna Baba Mtakatifu anavyochaguliwa, huku kura zikipigwa na Makadinali peke yao, ambapo kwa Tanzania Japokuwa tuna makadinali wawili; Mzee wetu Mwadhama Kadinali Polcarp Pengo na Kaka yetu Mwadhama Kadinali Protase Rugambwa, uchaguzi huu wa mwaka 2025 ni Mwadhama Kadinali Rugambwa peke yake ndiyo alionekana katika mchakato wa kumpata Baba Mtakatifu Leo wa XIV.
Kwa utaratibu wa Kanisa Katoliki japokuwa Makadinali wanapiga kura ya kuchagua Baba Mtakatifu lakini mamlaka ya Kadinali katika Taifa analotokea ni ya Kijimbo tu, mathalani Kadinali Protase Rugambwa ni wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, huku Kadinali Pengo ni wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Kwa ukweli wa mambo, historia inadokeza kuwa katika mchakato huu awali alituwakilisha vizuri Kadinali Laurean Rugambwa na Baadaye Kadinali Pengo kwa uchaguzi wa Wababa Watakatifu kadhaa.
Kwa mamlaka ya Kanisa Katoliki la Tanzania, japokuwa misimamo ya Kanisa katika mambo kadhaa ya Kitaifa huwa inatolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki ya Tanzania (TEC) chini ya Rais wake ambaye huwa miongoni mwa Maaskofu wakifanya kazi kwa karibu na Katibu Mkuu wa TEC. Ili kulifahamu jambo hili ambalo lipo katika tafakari ya Mwanakwetu ni vizuri nikayataja majukumu kadhaa ya Kadinali katika Kanisa Katoliki.
“Makadinali katika Kanisa Katoliki ni washiriki wakuu wa makasisi, hasa washauri wa Baba Mtakatifu, na wana jukumu la kumchagua Baba Mtakatifu mpya wakati nafasi hii ikitokea kuwa wazi. Wanashiriki pia katika usimamizi wa Kanisa, kwa pamoja na kwa mtu mmoja mmoja, wakimsaidia Baba Mtakatifu katika kazi mbalimbali za kiutawala na za kichungaji.
Kimsingi,UKADINALI ni daraja kati ya Baba Mtakatifu na Kanisa Katoliki Ulimwenguni, wakifanya kazi kama washauri na watekelezaji wa maelekezo ya Baba Mtakatifu.
Uchaguzi wa Baba Mtakatifu, hapa ni kwa Makadinali walio chini ya umri wa miaka 80 wanaunda kitu kinachofahamika kama Chuo cha Makadinali na kushiriki katika kongamano la kumchagua Baba Mtakatifu mpya, wakati huyu wa sasa anapokufa au kujiuzulu. Jukumu lingine ni la kumshauri Baba Mtakatifu. Hapa pia Makadinali wanatoa ushauri na usaidizi huo kuhusu masuala ya utawala wa kanisa, sera na mambo ya kimataifa: Makadinali wengi wanashikilia nyadhifa za juu ndani ya Kanisa, na wanaweza pia kuwa maaskofu au maaskofu wakuu wa majimbo makuu, wakihudumu kama wajumbe wa Baba Mtakatifu na kusimamia maeneo muhimu ya Kanisa. Kazi nyingine ni Huduma ya Kichungaji hapa Makadinali wanatarajiwa kuwaongoza waamini ndani ya maeneo waliyopangiwa wakitangaza ujumbe wa Injili na kutumikia utume wa Kanisa.”
Hii ni tafakari fupi ya ndugu Mwanakwetu wakati makadinali wakipiga kura kumchagua Baba Mtakatifu Mpya Mei 2025.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Uchaguzi wa wa Baba Mtakatifu Leo wa XIV umefanyika huku Kanisa Katoliki la Tanzania na Baraza lake lake Maaskofu Katoliki Katibu Wake Mkuu Padri Dkt. Charles Kitima akiwa Kitandani Hospitalini akiuguza vidonda baada ya kushambuliwa na jamaa baada ya wahuni , mafedhuli hawa hawa watu wasiojulikana kumshambulia.
Ndugu yetu, kaka yetu Mwadhama Kadinali Protase Rugambwa akiwa anaipiga kura huko Vatikani huku Padri Kitima akiwa anapokea matibabu baada ya mashambulio hayo ya mabedui, maharamia , wahuni waliomvamia katika kituo chake cha kazi hapo TEC Makao Makuu Kurasini Dar es Salaam.
Mwanakwetu anapoyatazama majukumu ya Kadinali yoyote Ulimwenguni miongoni mwao ni kumshauri Baba Mtakatifu katika masuala mbalimbali ya kanisa na ndiyo kusema Japokuwa Kadinali Protase Rugambwa Siyo Rais Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, siyo Katibu wa TEC lakini yeye ni mtu muhimu sana kwa taifa letu katika kumshauri vizuri Baba Mtakatifu juu ya hoja kadhaa za Kanisa la Tanzania.
Kwa Utafiti wa Mwanakwetu, anakumbuka hali ya siasa ya Tanzania wakati wa Chama Kushika Hatamu ilikuwa tofauti Kidogo lakini nyakati za awali za Mfumo wa Vyama Vingi Mwadhama Kadinali Polcarp Pengo kwa nafasi yake alijitahidi mno kwa nafasi yake, kwa nafasi yake kutoa baadhi ya matamko ambayo kwa hakika yalikuwa yanatoa matumaini sana kwa waamini na Kanisa Katoliki la Tanzania, japokuwa pia Baraza la Maaskofu Katoliki la Tanzania na lenyewe kupitia Rais wake na Katibu wake Mkuu halikusita kuandika Nyaraka zake kadhaa.
Kwa sasa Kadinali Pengo ni Mzee jukumu hilo sasa halikwepeki kwa Kadinali Protase Rugambwa na Jimbo lake Kuu Katoliki la Tabora.
Mwanakwetu anaamini japokuwa hulka ya Kadinali Rugambwa ni mtu mtulivu sana, mkinywa lakini kuna wajibu wa yeye mwenyewe kama mpiga kura wetu wa kumchagua Baba Mtakatifu pale Vatikani anapaswa kuukimbia ukimya wake ili atoe neno katika baadhi ya mambo hayo na huko kuukimbia ukimya wake itakuwa na manufaa makubwa kwa Kanisa Katoliki la Tanzania hasa kwa kila mwanakondoo akiwamo Mwanakwetu.
Mwanakwetu anapoyatayarisha makala haya anaikumbuka Mathayo 8, 8 inayosema haya,
“Yule akida akamjibu, akasema, Bwana, mimi sistahili wewe uingie chini ya dari yangu; lakini sema neno tu, na mtumishi wangu atapona.”
Mwanakwetu anaamini kusema neno wakati mwingine huwa ni dawa ya magonjwa kadhaa yanayomkabili mwanadamu na kukaa kimya ni kumuacha mwanadamu abaki na magonjwa yanayomkubali. Inawezekana Jimbo Kuu Katoliki la Tabora halikutarajiwa kuwa na Kadinali kwa nyakati za sasa , haya ni mawazo ya Mwanakwetu tu na ukitegemea Mzee wetu Baba Askofu Mkuu Paul Luzoka ni mzee sana lazima Jimbo Kuu Katoliki la Tabora lina deni kubwa la kuwa chachu kwa kila mwanakondoo anayehangaika katika hii dunia hasa Tanzania ya leo.
Kwa sasa maamuzi ya Vatikani yalishafanyika lakini kwa sasa Jimbo Katoliki la Tabora linatakiwa kutambua hilo, kwenda sambamba na hali ya sasa ya Tanzania ili tuweze kusikia Kadinali wetu anasema nini katika mahubiri yake na anasema nini katika changamoto ambazo Watanzania wanazipitia ikiwamo utekaji, mashambulio na mauwaji ya watu wasio na hatia nchini Tanzania, kama alivyokuwa Kadinali Pengo wakati wake akiwa mwenye nguvu tele.
Mwanakwetu anakumbuka japokuwa alikuwa mdogo lakini anakumbuka fika hata Kadinali Laurean Rugambwa alikuwa mkali sana, hakuwa na tabia ya kukaa kimya katika jambo ambalo dhahiri lilionekana na dosari waziwazi alikaripia hadharani.
Kwa kuwa pia Mwanakwetu anakumbuka wakati Kadinali Protase Rugambwa akipewa Upadrisho Misa ya Septemba 2, 1990 pale Jangwani, Mwanakwetu nilikuwepo na kando yangu alikuwepo Babu yangu Mzaa Baba mwalimu Fidelis Makwega, eneo tulilopangiwa Wakristo wa Parokia ya Mbagala, babu yangu mzaa baba alinunua Bendera ya Vatikani na aliibeba Bendera ya Vatikani huku akiipepea angani wakati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II akitusalimia akipita katika gari la Kibanda Wazi waamini wake.
Nakumbuka Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II katika mahubiri yake aliyasema maneno haya;Nawasalimia kwa upendo washiriki wa Kanisa la Tanzania! Salamu zangu za pekee ziwaendee Kardinali Laurean Rugambwa na Askofu Mkuu Polycarp Pengo wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam, na Ndugu zangu Maaskofu wa Jimbo la Arusha, Dodoma, Mahenge, Mbulu, Morogoro, Moshi, Same, Tanga na Zanzibar.Nawasalimu viongozi wa dini na dini kutoka Tanzania nzima ambao ni viongozi wenu katika imani, matumaini na upendo. Pia natoa shukrani zangu za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na viongozi wa serikali waliohudhuria katika Misa hii, na wale wote walionisaidia kwa namna yoyote ile katika kupanga na kuandaa Ziara yangu ya Kichungaji katika ardhi yako.
Kwa namna fulani, salamu yangu inawaendea wale wanaotawazwa kwa ukuhani. Kutoka kwa familia zao na parokia, vijana hawa wameitwa kusimamishwa kwa Kristo, Kuhani Mkuu wa milele, ili wao nao wawe wachungaji wa watu wake, wahubiri wa neno lake na wahudumu wa sakramenti zake Yesu anawapa sehemu ya ukuhani wake mwenyewe ili waweze kutenda katika nafsi yake kutoa dhabihu ya Agano Jipya katika Liturujia ya Ekaristi, ili kutekeleza huduma ya upatanisho na kuwasaidia waamini wote kuishi katika utakatifu na amani, kadiri ya wito ambao kila mmoja ameupata kama kiungo cha Mwili wa Kristo, yaani Kanisa .
Haya Mwanakwetu anayakumbuka tu kwa maana alikuwepo wakati Kadinali Protase Rugambwa akipewa daraja la Upadri pale Viwanja vya Jagwani Dar es Salaam.Baba Mtakatifu awali katika mahubiri yake alianza na maneno haya; Yesu asema: ‘Mimi ndimi Mchungaji Mwema... autoaye uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wanijua mimi.’ Maneno haya yanarudiwa kwa Kadinali Protase Rugambwa mwenyewe kama Mbiu ya Mgambo akumbuke maneno haya ambayo Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa II aliyatumia kama ufunguo wa mahubiri yake pale Jangwani Septemba 2, 1990.
Mwanakwetu upo?
Je makala haya niyaitaje ? Nawajua walio wangu, Nao Walio Wangu Wanijua Mimi , Kadinali Protase Rugambwa Anajukumu Zito Kufikia Viwango Vya Watangulizi Wake, Ni Kadinali AliyEzungukwa. na Vigugumizi vya Vilio au Mwanakondoo Anayechechemea?
Mwanakwetu Anachagua Mwanakondoo Anayechechechemea.
Nakutakia Siku njema
0717649257
Post a Comment